Mradi wa Nourish waleta mageuzi Babati

Habari Leo
Published: May 27, 2025 14:09:26 EAT   |  General

MANYARA: MRADI NOURISH unaosaidia wakulima wadogo kulima kwa tija ili kuwa na usalama wa chakula na kipata kipato umeleta mageuzi wilayani Babati kwa kusaidia kaya kujiunga kwenye vikundi vya kilimo na kuwasaidia kupambana na udumavu kwa watoto wadogo. Katibu Tawala wa Wilaya ya Babati, Khalfan Matipula amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha …

MANYARA: MRADI NOURISH unaosaidia wakulima wadogo kulima kwa tija ili kuwa na usalama wa chakula na kipata kipato umeleta mageuzi wilayani Babati kwa kusaidia kaya kujiunga kwenye vikundi vya kilimo na kuwasaidia kupambana na udumavu kwa watoto wadogo.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Babati, Khalfan Matipula amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Endanoga Wilaya ya Babati katika hafla ya kufunga maadhimisho ya Wiki ya Wakulima wa NOURISH yaliyoendeshwa kwa wiki nne katika  halmashauri za wilaya 10 Tanzania.

Katika Wilaya ya Babati mradi wa NOURISH ulianza utekelezaji mwaka 2024 na hadi sasa 2024 na hadi sasa umefanikiwa kuanzisha vikundi vya kilimo 75 vikiwa na jumla ya wanachama 2,346.

Aidha kupitia mradi huo mashamba darasa 57 yameanzishwa, mbegu za viazi lishe  vimesambazwa kwa wakulima kwa lengo la kuzalisha mbegu kwenye ngazi ya kata ambapo jumla ya pingili 40,000 zimetolewa.

Alisema tangu mradi huo upokelewa wilayani humo  umewaongezea ujuzi wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambao wamekua chachu katika kutoa elimu ya afya na lishe kwa jamii inayowazunguka.

Alisema kupitia elimu hiyo imesaidia kupunguza tatizo la utapiamlo haswa udumavu kwa watoto na kutaka wakulika washiriki mradi huo kwani ni chachu ya maendeleo kwenye kaya zao kupitia yale waliyojifunza katika vikundi.

“Maisha bora yanapatikana kwa kila mmoja kufanya kazi kwa bidii na kwa kutumia utaalamu. Nishauri tena wataalamu wa ugani hakikisheni mnawajibika kuleta maendeleo hasa kwa kwenda na hili wimbi la mradi huu ambao umeonyesha njia ya kweli ya maendeleo vijijini.” amesema Matipula.

Awali Afisa mradi wa NOURISH kutoka katika shirika la RECODA Salome James,alisema mradi wa NOURISH wilayani Babati unatekelezwa katika vijiji 42 vilivyoko katika kata 10 ambapo utekelezaji wake umetumia maafisa ugani, wahudumu wa afya ngazi ya jamii na wakulima viongozi wa ngazi ya kijiji ambao walichaguliwa na serikali za vijiji na kupewa mafunzo juu ya utekelezaji wa kazi zao kabla ya kuanza kufanya kazi za mradi.

Mradi huo pia unashughulikia changamoto za usalama wa chakula kwa wakulima wadogo kupitia njia tatu kuu za mafanikio ambazo ni kuongeza uzalishaji kupitia mafunzo ya kilimo kinachozingatia tabianchi, upatikanaji wa pembejeo bora, na rasilimali za kifedha.

Pia,kuimarisha masoko ya chakula kwa kushirikisha wadau wa biashara kutumia suluhisho za kidijiti na kuwawezesha wakulima wadogo na kati.