Mpango aagiza mambo matano mageuzi benki

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amesema sekta ya benki nchini inakabiliwa na mageuzi ya haraka ya teknolojia, ushindani wa kimataifa na mahitaji mapya ya wateja. Ametaka benki zizingatie mambo matano muhimu, ikiwemo kuendelea kufanya mageuzi ya teknolojia kwa kuongeza matumizi ya huduma za kimtandao ili kuongeza ufanisi, usalama na ushindani. Amesema hayo jijini Arusha …
MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amesema sekta ya benki nchini inakabiliwa na mageuzi ya haraka ya teknolojia, ushindani wa kimataifa na mahitaji mapya ya wateja.
Ametaka benki zizingatie mambo matano muhimu, ikiwemo kuendelea kufanya mageuzi ya teknolojia kwa kuongeza matumizi ya huduma za kimtandao ili kuongeza ufanisi, usalama na ushindani.
Amesema hayo jijini Arusha wakati akifungua semina ya wanahisa wa Benki ya CRDB, Mkutano Mkuu wa 30 wa Wanahisa wa benki hiyo 2025 pamoja na kuzindua shule maalumu ya sekondari ya CRDB itakayojengwa Ilala, Dar es Salaam.
Dk Mpango alisema mageuzi ya teknolojia ni muhimu katika sekta ya fedha na jambo linalohitaji ushirikiano na wadau wa teknolojia ya fedha ili kubuni bidhaa na huduma zenye ubora, kuwekeza kwenye teknolojia ili kutapunguza gharama za uendeshaji kutawezesha kuwafikia wateja wengi zaidi kwa muda mfupi.
Alisema ni muhimu kuwa na rasilimaliwatu yenye ustadi katika Tehama kwa kuwa katika miaka ijayo matumizi ya akili mnemba katika tasnia ya benki yataleta mageuzi makubwa na kufungua fursa mpya.
Dk Mpango alisema kukua kwa matumizi ya teknolojia kumeleta pia, wimbi la matukio ya uhalifu wa kimtandao unaohatarisha mitaji ya benki duniani.
Kutokana hilo, alisema udhibiti wa tishio la uhalifu wa kimtandao unapaswa kuwa kipaumbele cha benki ili kujenga imani ya wateja na kulinda heshima yao.
Alisema usimamizi wa vihatarishi na hitaji la kuzingatia kanuni za kifedha za kimataifa ni eneo linalohitaji kuangaliwa kwa makini ikizingatiwa kuwa matumizi makubwa ya teknolojia yanaondoa mipaka ya kijiografia na kuunganisha huduma za fedha duniani.
Alizitaka Benki Kuu na Jumuiya ya Mabenki nchini (TBA) kupitia sheria na kanuni zinazosimamia sekta ya fedha kimataifa na kinchi ili kulinda na kuepuka hatari ya kupoteza rasilimali.
Kuhusu ulinzi na uhifadhi mazingira hususani katika kupunguza uzalishaji wa gesijoto ni ajenda ya kidunia inayohitaji nguvu za pamoja.
Alisema benki zimekuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa Mkataba wa Paris kwa kuwezesha upatikanaji wa rasilimali muhimu katika jitihada hizo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema azma ya benki yao katika kipindi cha miaka 30 iliyopita na miaka 30 ijayo ni kuboresha maisha ya watu na kukuza uchumi kwa ujumla kwa kuweka mkazo kwenye matumizi ya teknolojia ya kisasa na mikakati madhubuti inayowawezesha kuwafikia wananchi mijini na vijijini kwa ufanisi zaidi.
Alisema tangu mwaka 1996 benki hiyo ilipoanza safari yake mpya ikiwa na matawi 19 pekee, wameendelea kupanua mtandao wao hadi kufikia matawi 260 nchini, mageuzi yaliyoambatana na uwekezaji mkubwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dk Ally Laay alisema jitihada za bodi hiyo zimeiwezesha benki yao kupata ukuaji endelevu wa kifedha jambo ambalo limeongeza thamani ya uwekezaji wa wanahisa wao huku thamani ya hisa za benki kwenye soko imekuwa ikipanda mwaka hadi mwaka.
Alisema kutokana na mafanikio ambayo CRDB imeyapata mwaka jana kwa kurekodi faida baada ya kodi ya Sh bilioni 551, Bodi ya Wakurugenzi imependekeza gawio la Sh 65 kwa hisa sawa na ongezeko la asilimia 30 ikilinganishwa na gawio la Sh 50 kwa hisa kwa mwaka 2023.