Mji Mkongwe Mikindani na fahari ya historia muhimu

“Mikindani ni moja ya miji mikongwe inayopatikana katika pwani ya Afrika Mashariki, yenyewe tunaizungumzia hata kabla ya ujio wa wageni. “Hapa tunazungumzia miaka mingi iliyopita, wakati wa jamii za Kiafrika kabla ya ukoloni. Hapo, tunazungumzia chini ya miaka 200 kabla ya Kristo.” Ndivyo mazungumzo yanavyoanza baina ya HabariLEO na Meneja Mafunzo katika Hoteli ya Mafunzo …
“Mikindani ni moja ya miji mikongwe inayopatikana katika pwani ya Afrika Mashariki, yenyewe tunaizungumzia hata kabla ya ujio wa wageni.
“Hapa tunazungumzia miaka mingi iliyopita, wakati wa jamii za Kiafrika kabla ya ukoloni. Hapo, tunazungumzia chini ya miaka 200 kabla ya Kristo.”
Ndivyo mazungumzo yanavyoanza baina ya HabariLEO na Meneja Mafunzo katika Hoteli ya Mafunzo ya Old Boma, Mji Mkongwe Mikindani, Lucas Navilongo anapoelezea kuhusu historia ya Mji Mkongwe Mikindani.
Navilongo anasema mji huo ulianza kupata umaarufu tangu wakati huo kwa kuwa ndiyo mji wa kwanza kuendelea kabla ya Mtwara Mjini.
“Wakati huo tunazungumzia mji wa Mikindani ukiwa unatambulika kama Kimbuli ama Chimbuli,” anasema.
Anaongeza: “Hapo ni wakati wa makabila ya wenyeji ambao walikuwa wakiishi kwa kuhama, tunazungumzia watu kutoka Msumbiji ambao ndiyo hao akina Chimbuli.
“Wakaishi Mikindani miaka mingi iliyopita. Walipoishi hapa, wakafanya jina la mji huu kupitia jina la ule ukoo maarufu wa Chimbuli waliohama kutoka Msumbiji wakafanya huu mji ujipatie umaarufu wa jina la Chimbuli,” anasema.
Historia ya jina Mikindani
Navilongo anasema wakiwa wanaendelea na shughuli za uzalishaji zikiwemo za kilimo, uvuvi, uchongaji na uzalishaji chumvi, wana Chimbuli walijiwa na ugeni kutoka Asia (Waarabu na Wahindi) waliokwenda katika eneo lile kufanya biashara.
Anasema kwa mujibu wa hadithi za mababu walioishi eneo hilo, nadharia za jina la Mikindani zinaanzia kwenye historia ya kuingia kwa wageni hao, ingawa ni nadharia moja ya mwisho pekee iliyokubalika na kutumika mpaka sasa.
Anasema iko nadharia ya kwanza ambayo ilieleza neno la Mikindani lilitokana na wageni waliokutana na wenyeji baharini na kutaka kuelezwa iliko nchi kavu wenyeji wakawajibu, ‘Nchi iko ndani’.
“Mababu waliokuwa wanatusimulia walikuwa wanasema waliuliza nchi iko wapi ingawaje walikuwa hawaelewani kwa lugha, lakini ni sehemu ya nadharia na mitazamo ambayo iliibuka na kusema kwamba labda ndiyo sababu ya kutokea jina la Mikindani.
“Kukua kwa lugha na usanifishaji wa lugha ndiko kunadaiwa kusababisha kutokea neno Mikindani. Sasa huo ukawa ni mtazamo tu ambao haukupata mashiko,” anasema Navilongo.
Anaongeza: “Lakini kupitia wageni haohao, wanasema mtazamo mwingine ni ule ambao walisema wamama au wadada katika maeneo ya pwani, watoto wa kike walikuwa hawaruhusiwi kutoka nje… walikuwa wakitumia msemo uliokuwa unasema ‘mtu ndani’ yani yule mama haruhusiwi kutoka nje wakasema huenda ndiyo ilisababisha kutokea kwa jina la Mikindani. Lakini bado na yenyewe haikuleta mashiko.”
Anasema nadharia ya mwisho ambayo ndiyo inayotumika kwa sasa ni ile inayohusisha Waarabu na kilimo cha nazi na kwamba lilitokana na minazi midogo waliyoiita Mikinda.
“Hapo sasa tunaanza kupata nadharia yenye mashiko hapo tuko kati ya Karne ya Nane na 14 tuko sasa na uhusiano na waarabu wameanza kuishi, wamejenga lakini wanafanya biashara ya watumwa na Mikindani ni moja ya sehemu ambayo watumwa walipita wakitokea Tunduru lakini pia maeneo ya Umakondeni,” anasema.
“Sasa wale kupitia zao la nazi ambalo lililimwa eneo kubwa la Mikindani… ile minazi inapokuwa midogo wakaiita mikinda kwa hiyo walivyoiita mikinda ukiwa umeenda kwenye lile shamba la mikinda unasema unaenda mikindani wakasema huenda hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya eneo hilo kuitwa Mikindani.
“Sasa nadharia hiyo ndiyo ikapata mashiko na kukubalika kwamba ina uhusiano wa moja kwa moja na kutokea kwa jina hilo. Kwa hiyo watu wakajikuta wanaacha kutumia jina la Chimbuli na kutumia jina la Mikindani.”
Ujio wa David Livingstone na kukoma biashara ya utumwa
“Sasa hao ni Waarabu na biashara yao ya watumwa na kilimo cha nazi. Hapo tunazungumzia Karne ya 14.
“Baadaye tunakuja kuona nchi za Ulaya zinaanza kupanuka, hapo tunaanza kuona vitangulizi vya ukoloni… Mikindani pia inaanza kujipatia umaarufu wa kupokea wageni wengine tofauti na Waarabu,” anasema Navilongo.
“Wapelelezi kama, Dk David Livingstone anakuja Mikindani miaka ya 1850, 60… aliweka hema. Akaishi hapa wakati huo alikuwa anajaribu kwenda akaone chanzo cha Mto Nile, lakini alipofika Mikindani akakuta biashara ya utumwa bado inaendelea.
“Akalazimika kubaki pale kwa muda, akaandika ujumbe kwenda kwao England, akaandika ripoti akaipeleka kwao.”
Maelezo ya historia hiyo yanakaziwa pia, na Mhifadhi Kiongozi Mji Mkongwe Mikindani, Brigthon Kawiche ambaye anasema kwa kuona umuhimu wa kile kilichofanywa na Livingstone, Shirika la kujitolea la Trade Aid la Uingereza liliamua kuweka Makumbusho ya Livingstone hapo Mji Mkongwe Mikindani.
“…Imewekwa hapo kutokana na historia ya Dk Livingstone, alifika huku mwaka 1866 katika shughuli zake za upelelezi alifika… baada ya kufika alichangia kumalizika kwa biashara ya utumwa huku Kusini, alinunua baadhi ya watumwa akawaachia huru na baadaye akaandika barua kwao ambayo ilisaidia kusitishwa kwa biashara ya watumwa hapa Mikindani na eneo la Kusini lote,” anasema.
Anasema nyumba hiyo ya makumbusho ndani yake inaeelezea utamaduni wa makabila ya eneo hilo.
Wageni kuingia Mikindani
Navilongo anasema baada ya Livingstone kupita, ukoloni ukaanza kwenye makoloni ya Afrika, kwa hiyo Wajerumani walipochukua koloni la Tanganyika wakianzia Bagamoyo, baadaye Dar es Salaam wakapanuka mpaka Kusini, Mikindani ikawa makao makuu yao kwa upande wa Kusini, wakajenga jengo la boma hapa (eneo la Kilimani) ambalo lilijengwa kimkakati kuelekea upande wa baharini iliko bandari kwa sababu za kiusalama.
Anasema Wajerumani walilitumia jengo hilo kwa shughuli za utawala, ulinzi na usalama.
“Ndiyo maana utaona na ule mnara walioutumia kwa ulinzi wa eneo hilo la bahari, kwamba adui yeyote atakuja kwa kupitia mlango bahari wa Mikindani na watamuona,” anasema.
Anasema pia, walilitumia kama sehemu ya kufanya mikutano na kubadilishana mawazo kuhusu mambo mbalimbali ya kazi na baadaye kila mmoja anarejea kwao.
Hadithi iliyofichwa
Navilongo anasema ipo hadithi iliyofichwa kuhusu boma la Wajerumani ambayo wao waliigundua baada ya ndugu wa Mjerumani mmoja aliyewahi kuishi na kuzikwa Mikindani walipokwenda kutafuta kaburi la ndugu yao wakatoa hadithi ya kwamba boma la awali la Wajerumani lilijengwa na kuanguka kabla ya kujengwa tena hili lililopo sasa.
“Majengo haya yalianza kujengwa mwaka 1890, hapo ukoloni ndio umeanza Afrika Mashariki na hili jengo likajengwa, lakini likabomoka.
“Hii historia inaonekana Wajerumani hawajaieleza sana kwa sababu waliona wanaonekana wamefeli kwa hiyo wakalirudishia tena mwaka 1895,” anasema.
“Sisi tulijua baada ya mzee mmoja (sikumbuki jina lake) ambaye ni Mjerumani alikuwa hapa Mikindani wakati wanajenga na alikuwa anafanya shughuli za kilimo kwa hiyo kuna wajukuu zake walikuja mwaka jana (2024) wakiwa na vitabu, wanasema wanatafuta kaburi la babu yao ambaye aliishi Mikindani na kuzikwa Mikindani, kwa hiyo vile vitabu mzee alivituma kule kwao na kwenye hivyo vitabu alieleza kuhusu hilo boma na shughuli nyingi zilizofanyika Mikindani.”
Anasema wageni hao walizunguka Mikindani na kufanikiwa kupata eneo ambalo wanahisi babu yao alizikwa na waliondoka kwa ahadi ya kurejea kufanya utafiti zaidi wa kujua mahali alipozikwa babu yao kwa kufata taratibu husika za vibali ili wajue alizikwa wapi na kama wanaweza kupata mabaki yake.
ITAENDELEA…