Mitaala FETA kuandaa wahitimu watakaojiajiri

MOROGORO: KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Profesa, Riziki Shemdoe ameutaka Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA),kuandaa wahitimu watakaoweza kujiajiri na kuajiri wengine badala ya kusubiria kuajiriwa. Profesa Shemdoe ametoa kauli hiyo mjini Morogoro wakati akifungua kikao kilichokutanisha wadau wa kujadili rasimu ya mitaala mitano inayohuishwa na mitaala 12 mipya …
MOROGORO: KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Profesa, Riziki Shemdoe ameutaka Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA),kuandaa wahitimu watakaoweza kujiajiri na kuajiri wengine badala ya kusubiria kuajiriwa.
Profesa Shemdoe ametoa kauli hiyo mjini Morogoro wakati akifungua kikao kilichokutanisha wadau wa kujadili rasimu ya mitaala mitano inayohuishwa na mitaala 12 mipya iliyoandaliwa na wakala huo.
“Ni lazima tubadilike katika utoaji wetu wa elimu ili kuzingatia mafunzo yanayojikita kwenye ujuzi wa vitendo zaidi ili wahitimu wetu waweze kujiajiri na baadaye waajiri wengine,” amesema Profesa Shemdoe.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo pia ameutaka wakala huo kutengeneza mitaala itakayozalisha wataalam wanaozingatia mabadiliko ya tabia nchi kwenye utekelezaji wa shughuli za uvuvi na ukuzaji viumbe maji.
Profesa Shemdoe ameutaka wakala huo kuhakikisha mitaala mipya hiyo izingatie teknolojia za kisasa ikiwa na matumizi ya zana mpya za uvuvi, ukuzaji viumbe maji, na pia izingatie matumizi ya Akili Mnemba.
“…Lazima mitaala hii izingatia pia matumizi ya akili mnemba kwa sababu tusipoliangali hili tunaweza kujikuta siku za usoni tunasahihisha kazi iliyofanywa kutokana na matumizi ya teknolojia hiyo,” amesema Profesa Shemdoe.
Naye, Mtendaji Mkuu wa FETA, Dk Semvua Mzighani amesema kuwa Mitaala inayotarajiwa kuanzishwa itasaidia kutengeneza wataalamu waliobobea katika sekta ya uvuvi ambao watasaidia katika kukuza uchumi wa buluu.
” Serikali inakamilisha ujenzi wa bandari za uvuvi za Kilwa na Bagamoyo hivyo tunataka wataalamu watakaozalishwa kutokana na mitaaala hii mipya waende kusaidia katika usimamizi wa Bandari hizi” amesema Dk Mzighani.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Rais ,Sekretariati ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Rehema Ndahani, amesema mitaala hiyo mipya itawawezesha vijana kupata maarifa yatakayowasaidia kuleta mageuzi chanya katika sekta ya uvuvi ili kwenda na mabadiliko ya teknolojia ya kisasa.
Kikao hicho cha kuhuisha mitaala ya zamani na kuanzisha mitaala mipya kitafanyika kwa muda wa siku 10 ambapo kimeshirikisha wadau kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Wizara ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Sekretarieti ya Ajira na Shirika lisilo la Serikali la Sustainable Agriculture Tanzania (SAT).