Mavunde kuongoza kongamano la Madini Geita

Habari Leo
Published: May 09, 2025 13:38:06 EAT   |  Sports

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde anatarajiwa kuongoza kongamano la wachimbaji wadogo nchini linatalorajiwa kufanyika kitaifa Mei 11, 2025 katika Mamlaka ya mji mdogo wa Katoro wilayani Geita. Kongamano hilo limeandaliwa na Shirikisho la Wachimbaji Wadogo mkoa wa Geita (GEREMA) chini ya usimamizi wa shirikisho la Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA). Mwenyekiti wa Gerema, Titus Kabuo …

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde anatarajiwa kuongoza kongamano la wachimbaji wadogo nchini linatalorajiwa kufanyika kitaifa Mei 11, 2025 katika Mamlaka ya mji mdogo wa Katoro wilayani Geita.

Kongamano hilo limeandaliwa na Shirikisho la Wachimbaji Wadogo mkoa wa Geita (GEREMA) chini ya usimamizi wa shirikisho la Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA).

Mwenyekiti wa Gerema, Titus Kabuo amebainisha hayo Mei 08, 2025 wakati akizungumzia maandalizi ya kongamano hilo mbele ya waandishi wa habari mkoani Geita.

Kabuo amesema kongamano hilo linatarajiwa kukutanisha wachimbaji wadogo kutoka ndani na nje ya mikoa ya kanda ya ziwa huku ajenda kuu ikiwa ni kumshukuru na kumpongeza rais Dk Samia Suluhu.

Amesema kongamano linalenga kujadili, kutangaza na kusherehekea maendeleo ya sekta ya madini kwa wachimbaji wadogo chini ya serikali ya awamu ya sita ambayo imeweka sera rafiki kwa wachimbaji.

Kabuo amesema hayo ni matokeo ya juhudi kubwa zilizofanywa na serikali kuboresha mnyororo wa thamani ya kwa wachimbaji wadogo kuanzia mchakato wa uchimbaji, uchakataji na usafishaji wa madini.

“Haya ni mapinduzi makubwa, haya yote yanasababishwa na utulivu uliopo nchini, amani tuliyonayo lakini pia na sera rafiki zinazotujali sisi wachimbaji”, amesema Kabuo.

Katibu wa Wachimbaji Wadogo Wilaya ya Geita, Agnes Kihamba amesema kongamano hilo litajumuisha pia wachimbaji wadogo wanawake ambao wamepata fursa kubwa chini ya serikali ya awamu ya sita.

Amesema hapo awali haikuwa rahisi kwa wanawake kumiliki leseni kutokana na mfumo dume kwenye sekta ya madini lakini kwa sasa mabadiliko yamefanyika na kufungua milango kwa wanawake.

“Leseni zilivyotoka kwa uwingi, imefanya wachimbaji wadogo kuonekana tuna nguvu zaidi kuliko hapo mwanzo, hapo mwanzo tulikuwa hatuna nguvu kwa sababu tulikuwa tunaishi kwa kuvamia maeneo” amesema Kihamba.

Meneja wa Mgodi wa Msasa wilayani Geita, James Matimba amesema kwa sasa wachimbaji wadogo wananufaika moja kwa moja kwa moja na biashara ya madini tofauti na hapo awali walitegemea madalali.