Masaka, Frida Amani kuongeza thamani ya wasichana

Habari Leo
Published: May 16, 2025 14:12:09 EAT   |  Entertainment

MCHEZAJI  wa Timu ya Taifa ya Wanawake Tanzania anayecheza nchini England, Aisha Khamisi Masaka kwa kushirikiana na msanii wa Hip Hop, Frida Amani kupitia taasisi zao wamezindua  kampeni maalum kumwezesha msichana kuitambua thamani na kutimiza ndoto. Kampeni hiyo, iitwayo “Amka Malkia – Jiamini, Jiongeze,” inalenga kuchochea ushiriki wa wasichana katika michezo, hasa soka, pamoja na …

MCHEZAJI  wa Timu ya Taifa ya Wanawake Tanzania anayecheza nchini England, Aisha Khamisi Masaka kwa kushirikiana na msanii wa Hip Hop, Frida Amani kupitia taasisi zao wamezindua  kampeni maalum kumwezesha msichana kuitambua thamani na kutimiza ndoto.

Kampeni hiyo, iitwayo “Amka Malkia – Jiamini, Jiongeze,” inalenga kuchochea ushiriki wa wasichana katika michezo, hasa soka, pamoja na kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyoo salama na rafiki kwa wasichana katika shule za mikoa mitano nchini, ikianzia Mkoa wa Lindi.

Akizungumza leo Mei 16,  jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi, Aisha amesema: “Nilianza kucheza mpira nikiwa shuleni. Leo hii narudisha fadhila kwa kusaidia wasichana wanaokuja nyuma yangu watambue mchango wao katika jamii na taifa.”

SOMA ZAIDI: Aisha Masaka atua Ligi Kuu Wanawake England

Aisha aliongeza kuwa atashirikiana na wachezaji wa ndani na nje ya nchi, watakaopata nafasi ya kushiriki katika kampeni hiyo ambayo kilele chake ni mechi maalum ya soka itakayofanyika Juni 8, 2025, katika viwanja vya KMC Mwenge, Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Frida Amani amesema, “Uwepo wa mwanamichezo kama Aisha ni ushahidi kuwa mtoto wa kike anaweza kufika mbali. Tunataka kuonyesha wasichana kuwa ndoto zao ni halali na zinawezekana.”

Meneja wa Amani Foundation, Frank Johnson, amesema kuwa kupitia sekta ya michezo, kampeni hiyo inalenga kuibua vipaji, kukuza kujiamini kwa watoto wa kike, na kuchangisha fedha kwa ajili ya miundombinu bora mashuleni.

Kampeni hiyo pia imeungwa mkono na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, pamoja na kampuni ya Premium Security.

“Hii ni zaidi ya soka; ni harakati ya kumwinua mtoto wa kike,” amesema Anifa kutoka AKM Foundation.