Mambo yanayoipa Hifadhi ya Ngorongoro upekee duniani

“HIFADHI ya Ngorongoro ni eneo la kipekee duniani lenye hadhi tatu zinazotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).” Inasema taarifa ya Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA, Dk Elirehema Doriye kuhusu mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na …
“HIFADHI ya Ngorongoro ni eneo la kipekee duniani lenye hadhi tatu zinazotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).”
Inasema taarifa ya Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA, Dk Elirehema Doriye kuhusu mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCA).
Dk Doriye anatoa taarifa hiyo ya hivi karibuni akisema: “Hadhi hizo ni Hifadhi ya Binadamu na Biolojia ambayo ni hadhi inayothibitisha umuhimu wa uhifadhi endelevu unaojumuisha binadamu na mazingira ya asili pamoja na Urithi wa Dunia Mchanganyiko inayotambua thamani ya kipekee ya maliasili na urithi wa kiutamaduni uliopo ndani ya eneo la hifadhi.”
Hadhi ya tatu kwa mujibu wa taarifa hiyo ni Hifadhi ya Jiolojia ya Dunia inayohusisha mandhari ya kipekee ya kijiolojia, milima, volkano na mabonde yanayoelezea historia ya mabadiliko ya dunia. Machapisho mbalimbali yanabainisha kuwa, Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro lilianzishwa mwaka 1959 likiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 8,292.
Lilianzishwa kama eneo la matumizi mseto ya ardhi ambapo shughuli za uhifadhi, utalii, wanyamapori pamoja na shughuli za kibinadamu zinafanyika kwa pamoja kuhakikisha kuna uwiano kati ya maendeleo ya jamii na uhifadhi endelevu wa mazingira.
“Aidha, mwaka 2023 Hifadhi ya Ngorongoro ilichaguliwa na Mtandao wa World Travel Awards kama Kivutio Bora cha Utalii Barani Afrika,” inasema taarifa hiyo. Inaongeza: “Hii ni heshima kubwa inayothibitisha umuhimu wa hifadhi hii katika utalii wa kimataifa.”
Rais Samia aliingia madarakani Machi 19, 2021 kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli. Kamishna Doriye anasema katika kipindi cha miaka minne (2021-2024) ya uongozi wa Rais Samia, NCAA imepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu yake ya uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii.
Akitoa taarifa hiyo kwa wanahabari mjini Dodoma hivi karibuni, Dk Doriye anasema katika kipindi hicho kumekuwa na ongezeko kubwa la watalii nchini likiambatana na ongezeko la mapato ya serikali.
Anasema: “Hifadhi ya Ngorongoro ni moja ya maeneo yanayotembelewa na watalii wengi nchini Tanzania kutokana na vivutio vyake vya kipekee, vikiwemo mandhari ya kuvutia, wanyamapori wengi na historia ya kipekee ya kiutamaduni na kiakiolojia.
“Hali hii imewezesha hifadhi hii kuwa moja ya vivutio vinavyochangia asimilia kubwa ya watalii wanaokuja nchini.” Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa, kati ya Julai 2021 hadi Februari 2025, watalii 2,916,540 wametembelea vivutio vya utalii ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Miongoni mwa vivutio vingi vya utalii ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali ni pamoja na Bonde la Ngorongoro maarufu, ‘Ngorongoro Crater’, Bonde la Empakai, Mlima Oldoinyolengai na mlima pekee Tanzania ambao volkano yake bado ni hai.
Vinasema wanyama wanaopatikana katika hifadhi hiyo ni pamoja na simba, fisi, nyumbu, viboko, swala, kongoni aina ya cokei na ngiri, pofu, pundamilia, duma, mbogo (nyati) na tembo. Viumbe hai ndege ni pamoja na mbuni, tandawala na kanga. Ngorongoro ndio sehemu pekee zaidi Tanzania kuwaona wanyamapori aina ya faru zaidi katika Bonde la Ngorongoro.
Katika Hifadhi ya Ngorongoro pia, kuna mchanga unaohama kwa meta 17 kwa mwaka bila kubadili umbo lake la mwezi mchanga ukiwa umejikusanya pamoja bila kuacha mabaki nyuma. Doriye anasema: “Katika kipindi hicho cha uongozi wa Rais Samia, mapato ya Shilingi 693,959,894,001 yamekusanywa na kuingia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali…”
Anafafanua kuwa, katika Mwaka wa Fedha wa 2021/2022 watalii 425,386 walizuru hifadhi hiyo huku watalii kutoka nje ya nchi wakiwa ni 228,810 na watalii wa ndani 196,576. Kutokana na idadi hiyo ya watalii, maksanyo yaliyopatikana yalikuwa zaidi ya Sh 91.13.
Katika Mwaka wa Fedha 2022/23 takwimu za NCAA zinaonesha watalii wa nje waliotembelea hifadhi hiyo walikuwa 458,351 na wa ndani walikuwa 293,881 hivyo, kufanya jumla ya watalii 752,232 waliozuru hifadhi hiyo. Taarifa inabainisha kuwa, utalii katika hifadhi hiyo katika mwaka wa fedha wa 2022/ 2023 uliingiza takribani Sh bilioni 171.26.
Doriye anasema: “Katika Mwaka wa Fedha 2023/24 idadi ya watalii ilikuwa 908,627. Watalii wa nje walikuwa 553,875 na watalii wa ndani walikuwa 354,752. Mapato yaliyokusanywa yalikuwa Shilingi 219,547,542,813.”
Kuhusu mwaka huu wa fedha, takwimu za NCAA zinabainisha kuwa tangu Julai 2024 hadi Februari 2025, watalii waliotembelea vivutio mbalimbali katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro walikuwa 830,295. Kati yao, watalii kutoka nje ya nchi walikuwa 509,610 na wa ndani ya nchi walikuwa 320,685.
Jumla ya mapato yaliyokusanywa katika kipindi hicho cha Julai 2024 hadi Februari 2025 yalikuwa Sh 212,023,179,255.68. “Katika mwaka 2024/25, mwenendo unaonesha NCAA itapata watalii zaidi ya milioni moja na mapato zaidi ya lengo ambalo iliweka ambalo ni kukusanya Shilingi bilioni 230. “Hadi sasa katika mapato hayo, imeshakusanya asilimia 92…” anasema Kamishina Doriye.
Anaongeza: “Takwimu hizi zinaonesha kuwa juhudi za Mheshimiwa Rais Samia kupitia filamu za ‘Royal Tour’
na ‘Amazing Tanzania’ zilizochangia kuitangaza Tanzania na kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea vivutio vya utalii.
Aidha, mikakati mbalimbali ya shirika pamoja na ushirikiano kati ya sekta binafsi na mamlaka za utalii umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko hili.”
Kuhusu uhifadhi bora na ulinzi wa rasilimali za hifadhi, NCAA imefanikiwa kutekeleza hatua mbalimbali, zikiwamo kuendelea kutunza hadhi zake za kimataifa kutoka Unesco kama eneo lenye urithi mchanganyiko pamoja na eneo hilo kuendelea kuwa moja ya maajabu saba ya asili barani Afrika likiwa na miamba na sura za nchi zinazoelezea historia ya dunia na uumbaji wake.
Akizungumzia ufuatiliaji na ulinzi wa wanyamapori, Dk Doriye anasema: “Mfumo wa ufuatiliaji wa wanyamapori umeimarishwa na faru 29 wamewekewa alama za masikio na vinasa mawimbi ili kufuatilia mwenendo wao na
kuimarisha ulinzi.”
Kuhusu udhibiti wa ujangili, anasema NCAA kwa kushirikiana na vikosi maalumu na vyombo vya usalama
imedhibiti ujangili dhidi ya wanyamapori ndani na nje ya Hifadhi ya Ngorongoro na Pori la Akiba la Pololeti.
“Matukio ya ujangili dhidi ya tembo yamepungua kutoka 25 mwaka 2020/2021 hadi tukio moja pekee mwaka
2022/2023 na hakuna tukio lolote mwaka 2024,” anasema.
Anaongeza: “Mamlaka imekamata watuhumiwa 207 wa ujangili na 175 kati yao wamefikishwa mahakamani.
“Aidha, mitandao ya ujangili inayotumia sumu na silaha za jadi imevunjwa katika maeneo mbalimbali.”
Kamishina wa Uhifadhi huyo wa NCAA anasema matukio ya uhalifu dhidi ya wageni ndani ya hifadhi yamepungua kutoka 7 mwaka 2020/2021 hadi sifuri mwaka 2024 jambo linaloimarisha usalama wa watalii…”
Akizungumzia ongezeko la Idadi ya wanyamapori, anasema idadi ya faru weusi imeongezeka kwa asilimia 40 kutoka mwaka 2020 hadi 2024 kutokana na juhudi madhubuti za uhifadhi. “Idadi ya simba ndani ya hifadhi imefikia takribani 188 na idadi ya tembo imeongezeka kutoka 800 mwaka 2020 hadi makadirio ya 1,300 mwaka 2024,” anafahamisha.
Anaongeza: “Kuhusu kuimarika kwa hali ya uhifadhi katika Pori la Akiba Pololeti na Ngorongoro Mamlaka imeimarisha ulinzi wa rasilimali, hali iliyosaidia kudhibiti ujangili na kurejesha mfumo wa kiikolojia wa
Serengeti – Masai Mara. Hatua hizi zimechochea urejeo wa uoto wa asili na malisho ya wanyamapori.”
Kamishina Doriye anafahamisha kuwa, Machi 2025 NCAA ilipandikiza faru weupe ndani ya Kreta ya Ngorongoro kusaidia kuhifadhi wanyama hao adimu walio hatarini kutoweka duniani pamoja na faru weusi ambao Kreta ya Ngorongoro inasifika kwa kuwa mahali salama kwao.
Anasema: “Baada ya kufanya tafiti kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), mamlaka
ilijiridhisha kuwa eneo la kreta ni salama na bora kwa ustawi wa wanyama hawa. Kwa sasa, faru hawa wanaendelea vizuri bila changamoto yoyote.”