Majaliwa: Sanaa ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi

Habari Leo
Published: May 17, 2025 12:08:32 EAT   |  Jobs and Career

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema sekta ya utamaduni na Sanaa ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa wasanii na Taifa, kuongeza fursa za ajira, kurasimisha kazi za sekta sambamba na kuimarisha maadili ya jamii. Majaliwa ametoa wito kwa wasanii nchini kuweka kipaumbele kuwekeza mapato yatokanayo na kazi zao katika shughuli za mnyororo wa thamani wa …

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema sekta ya utamaduni na Sanaa ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa wasanii na Taifa, kuongeza fursa za ajira, kurasimisha kazi za sekta sambamba na kuimarisha maadili ya jamii.

Majaliwa ametoa wito kwa wasanii nchini kuweka kipaumbele kuwekeza mapato yatokanayo na kazi zao katika shughuli za mnyororo wa thamani wa sanaa ili kuongeza wigo wa kuajiri vijana katika sekta hiyo na kuongeza pato la Taifa.

Ameyasema hayo leo Mei 17 alipomuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Pili wa Wadau wa Utamaduni na Sanaa uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema sekta hizo zimeajiri makundi yote jumuishi yakiwemo ya watu wenye ulemavu, vijana, wazee na watoto kwa jinsia na hali tofauti na watu wote.

Waziri Mkuu amesema zaidi ya hayo, sekta hiyo inakuza ujasiriamali na biashara ndogondogo na za kati.

”Sote tumewashuhudia wasanii wakianzisha biashara, kuzirasimisha na kuziweka katika mfumo unaotambuliwa na mabenki ili  kuzitumia kama dhamana kwenye taasisi za kifedha ili kupata mitaji kwa shughuli mbalimbali,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wasanii wote nchini kujitahidi kutengeneza kazi bora zaidi na kurasimisha shughuli zao za sanaa katika mamlaka husika za binafsi na Serikali ili kila msanii awe rasmi na aweze kunufaika na fursa zilizopo.

Amesema Sekta za Utamaduni na Sanaa inatoa mchango mkubwa katika uchumi kote ulimwenguni, ambapo Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) ya mwaka 2022, imebainisha kuwa sekta hizo zilichangia asilimia 3.1 ya Pato la Dunia (GDP), huku ikitoa asilimia 6.2 ya ajira sawa na ajira milioni 50 duniani kote.

Waziri Mkuu amesema kwa kutambua umuhimu wa sekta za utamaduni na sanaa, Serikali imefanya jitihada mahsusi za kuendeleza sekta hizo. Jitihada hizo ni pamoja na kuimarisha mifumo kisera na rasilimalifedha kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kisekta.