Maeneo ya mpakani hatari kwa usalama

Kenya inakabiliwa na ongezeko la mashambulizi kutoka kwa vikundi vya wanamgambo na wahalifu wanaotoka mataifa jirani.
Kutoka Todonyang kwenye Ziwa Turkana, Moyale, Mandera kwenye mpaka wa Ethiopia na Somalia hadi Boni, Lamu eneo la pwani, raia na maafisa wa serikali wameuawa, kutekwa, au kujeruhiwa katika kile wakazi wanasema ni mapengo hatari katika usalama wa kitaifa.
Katika kisa cha hivi punde, watu wanne waliuawa Alhamisi katika eneo la Todonyang, kaunti ya Turkana miezi michache baada ya wengine 30 kuripotiwa kuuawa na wavamizi kutoka Ethiopia.
Kamishna wa Kaunti ya Turkana, Julius Kavita, alithibitisha kuwa miili hiyo ilipatikana karibu na eneo la Ilemi Triangle, ambalo limekuwa chanzo cha mivutano ya muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.
“Miili imetolewa kutoka eneo la tukio na imehifadhiwa katika mochari ya Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Lodwar. Tumejulisha wakazi wawe watulivu huku uchunguzi ukiendelea. Tuko katika mawasiliano na maafisa wa Ethiopia kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kuadhibiwa,” alisema Kavita.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Turkana, John Tarus, vikosi vya usalama vimeimarisha doria katika maeneo ya mpaka. Hata hivyo, alikiri kuwa changamoto za miundombinu duni, hasa barabara na mawasiliano, zimeathiri pakubwa shughuli za kudumisha usalama.
"Tunahitaji mitandao bora na barabara zinazofikika haraka ili kuweza kuokoa maisha. Hatuwezi kutoa huduma bora za usalama kama hatuwezi kufika kwenye maeneo ya tukio kwa wakati,” alisema Tarus.
Tukio hilo lilijiri huku watu 20 wakiwa hawajulikani waliko kufuatia shambulizi la awali. Mashambulizi katika mipaka ya Kenya na majirani zake yanaongezeka huku Idara ya Taifa ya Ujasusi ikiripoti kudorora kwa usalama katika mipaka ya Kenya isipokuwa upande wa kusini inapopakana na Tanzania.
Katika tukio lililoshangaza taifa, machifu watano wa Kenya walitekwa nyara na wanamgambo wanaoshukiwa kuwa wa Al-Shabaab walipokuwa wakielekea kwenye mkutano wa usalama karibu na Elwak, Kaunti ya Mandera, Februari mwaka huu.
Walizuiliwa mateka nchini Somalia kwa zaidi ya miezi miwili.'Walirudishwa na watu wasiojulikana baada ya mazungumzo kati ya wazee wa jamii na magaidi. Serikali ilifahamu kuhusu tukio hilo, lakini haikuingilia moja kwa moja,' alisema afisa wa usalama ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa sababu ya usiri wa operesheni.
Katika tukio lililotisha zaidi, watu 20 waliuawa mwanzoni mwa Mei baada ya wavamizi waliokuwa na silaha nzito kushambulia wavuvi kwenye Ziwa Turkana katika eneo la Todonyang, Kaunti ya Turkana.
Inadaiwa kuwa wavamizi walivuka kutoka Ethiopia katika kile kinachodhaniwa kuwa ni shambulizi la kisasi kufuatia mzozo wa wavuvi wa jamii ya Turkana na Dasanach.
Siku chache baada ya shambulizi la Turkana, maafisa wa polisi walivamiwa katika eneo la Sessi, Moyale. Mshambulizi aliyekuwa kwenye pikipiki alifyatua risasi na kurusha vilipuzi kwenye kituo cha ukaguzi cha maafisa wa usalama, na kusababisha kifo cha afisa mmoja wa polisi na kujeruhi wengine wawili pamoja na mwanamke mmoja.
Ripoti ya Mkurugenzi Mkuu wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS), Noordin Haji, iliyowasilishwa kwa Bunge, ilifichua kwa kina jinsi Kenya inavyokosa vifaa vya kisasa vya kuimarisha usalama wa mipakani.
“Ukosefu wa bajeti na vifaa umetufanya tushindwe kulinda mipaka yetu kikamilifu. Kuna wavamizi kutoka Uganda (Karamojong), Sudan Kusini (walio na silaha za kijeshi), na Ethiopia (vikundi kama Oromo Liberation Army) ambao wanavamia maeneo yetu,” alisema Haji.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, KDF haijapata vifaa muhimu kwa zaidi ya miaka 10, huku maafisa wakikosa hata uwezo wa kufanya usajili mpya kwa miaka miwili mfululizo kutokana na uhaba wa bajeti. "Ni lazima kama nchi tuamue kama tunachukulia usalama kwa uzito. Hatuwezi kujitetea kwa maneno peke yake," aliongeza Haji.
Wakazi wa maeneo ya mpakani kama Mandera, Moyale, Boni na Todonyang wanalalamika kutengwa na serikali huku Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen akisema serikali imejitolea kulinda raia wake.
“Ni wazi kuwa Kenya iko katika hali hatari kwa kuzingatia matukio ya hivi majuzi ya uvamizi mipakani ambako raia na maafisa wa usalama wanauawa. Serikali inapaswa kuchukua hatua madhubuti na za haraka kuimarisha usalama mipakani,” asema mtaalamu wa masuala ya usalama, David Kiio.
Anasema wananchi wanaoishi maeneo ya mpakani wanaendelea kuishi kwa hofu ya mashambulizi kutoka kwa vikundi kutoka mataifa jirani.
“Kumbuka kuna suala la mpaka katika Ziwa Victoria ambapo wavuvi wa Kenya huwa wanahangaishwa na wale wa Uganda hasa kuhusu kisiwa cha Migingo,”alisema. Mapema mwezi huu, maafisa watano wa polisi wa kitengo cha operesheni maalumu (SOG) waliuawa katika msitu wa Boni kaunti ya Lamu na magaidi kutoka Somalia.