Maelfu wamuaga Msuya Mwanga

Habari Leo
Published: May 13, 2025 05:46:56 EAT   |  Educational

MAELFU ya wananchi wake kwa waume wa Wilaya ya Mwanga na maeneo ya jirani wamejitokeza kwa wingi kuuaga mwili wa Mbunge wa Kwanza wa Jimbo la Mwanga, Cleopa Msuya kwenye Uwanja wa Cleopa Msuya mjini Mwanga mkoani Kilimanjaro. Kwa heshima ya alama aliyoiweka katika sekta ya elimu, shule za msingi na sekondari za maeneo ya …

MAELFU ya wananchi wake kwa waume wa Wilaya ya Mwanga na maeneo ya jirani wamejitokeza kwa wingi kuuaga mwili wa Mbunge wa Kwanza wa Jimbo la Mwanga, Cleopa Msuya kwenye Uwanja wa Cleopa Msuya mjini Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Kwa heshima ya alama aliyoiweka katika sekta ya elimu, shule za msingi na sekondari za maeneo ya karibu, zilifungwa kwa muda ili kutoa nafasi kwa wanafunzi na walimu kumuaga Msuya ambaye ndio mwasisi wa maendeleo ya elimu wilayani humo.

Kuwasili uwanjani

Msafara uliobeba mwili wa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu Msuya, uliwasili kwenye Uwanja wa Cleopa Msuya saa 10:40 asubuhi ukiwa katika gari la Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na jeneza lililobeba mwili wake likiwa limefunikwa kwa bendera ya taifa.

Usalama uliimarishwa kwa kiwango kikubwa katika barabara zote ndani ya wilaya ikiwamo Barabara Kuu ya Dar es Salaam – Arusha ambayo ilifungwa kwa muda.

Wananchi wamlilia Msuya

Wananchi mbalimbali wamemwelezea Msuya kuwa kiongozi bora na mwasisi wa Wilaya ya Mwanga aliyeiletea maendeo lukuki.

Izadini Hemedi kutoka Kijiji cha Lwami alisema kama binadamu ambaye hakosi upungufu, Msuya alifanya jambo la maana kufanikisha kuundwa kwa wilaya hiyo.

Abdallah Kichikiro kutoka Kijiji cha Kisangiro alisema Msuya alifanikiwa kuimarisha Wilaya ya Mwanga katika sekta ya elimu, afya na barabara.

Msami Mkwizu ambaye ni mfugaji alisema mbali na mambo mengi mazuri aliyowafanyia wana Mwanga, Msuya kama mbunge alishindwa kuwatetea wananchi wa Lwami kupata fidia ya mashamba yao yaliyochukuliwa na jeshi miaka ya 1980.

Mama Fatuma ambaye ni mamalishe Kata ya Mwanga alisema wananchi wa Mwanga wanastahili kufurahia maisha yake kutokana na maendeleo aliyowaletea.

Shughuli ya kuaga mwili wa Msuya ilianza saa 6:40 mchana na kuongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi na kukamilika saa 7:30 mchana, ambako msafara uliobeba mwili wa Msuya uliondoka na kwenda nyumbani kwake Usangi ambako atazikwa leo.

Mabasi kusafirisha waombolezaji leo

Kutokana na jiografia ya eneo la Usangi kuwa katika milima, Kamati ya Maandalizi ya Wilaya imeandaa utaratibu wa kusafirisha wananchi kwenda Usangi kwenye maziko kwa kutumia usafiri wa mabasi.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mwanga ilisema magari yote binafsi yameandaliwa maegesho maalumu Mwanga Mjini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, lengo ni kuepusha usumbufu kutokana na uhaba wa maeneo ya kuweka magari pamoja na usalama wa watu.

Maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kuegeshwa magari ni pamoja na Uwanja wa Mpira wa Cleopa Msuya na Uwanja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria misa ya kuaga mwili wa Msuya ni Lukuvi, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Dk Jim Yonazi, Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, wabunge wa Mkoa wa Kilimanjaro na mikoa ya jirani pamoja na wakuu wa wilaya za mkoa huo.