Machifu wapewa polisi; watakuwa na mamlaka kama wakati wa Kanu

Taifa Leo
Published: May 09, 2025 07:55:23 EAT   |  News

HATUA ya kuwapa machifu maafisa wa polisi imeibua kumbukumbu ya mamlaka makubwa waliyokuwa nayo enzi ya utawala wa chama kimoja cha KANU, ambapo walitumiwa na serikali kunyanyasa raia. Machifu na wakuu wao wa utawala kote nchini Kenya wamepata tena nguvu moja kwa moja kufuatia kuanzishwa kikamilifu kwa Kitengo cha Polisi wa Utawala wa Serikali ya Kitaifa (NGAPU), kikosi kipya cha polisi kilichobuniwa kuimarisha usalama mashinani. NGAPU inasimamiwa na Bw Charles Mutuma, aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Kamanda wa kwanza wa kikosi hicho.Wakati wa Kanu, machifu walikuwa hawaguswi. Walitawala maeneo yao kama wafalme, wakiwa na vikundi vya vijana wa KANU waliotumia nguvu kwa niaba yao. Kwa wengi, kurejea kwa machifu wenye mamlaka kunafufua kumbukumbu za hofu, na ukatili. Mwanahistoria James Gatama, anakumbuka nafasi muhimu ya machifu katika utawala wa Kenya. “Wakati wa ukoloni, walikuwa wakitumikia utawala wa Waingereza,” anaeleza. “Wengine walisaidia harakati za Mau Mau kwa siri, lakini wengi walikuwa washirika wa watawala. Hata baada ya uhuru, machifu waliendelea kuwa na mamlaka makubwa. Chini ya Jomo Kenyatta, walikuwa na nguvu zaidi hata kuliko maafisa wa wilaya.” Katika utawala wa Moi, machifu walikuwa na polisi wao waliotekeleza maagizo yao. Walitoa ardhi, waliamua nani angefaidika na miradi ya serikali, na waliwalazimisha vijana kujiunga na Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS). Kukataa ilikuwa ni kwenda jela. Hakukuwa na nafasi ya kupinga.Sasa, kurejea kwa mfumo huu kunaleta hisia tofauti. Mzee Barisa Iyesa Thise, 70 kutoka Shirango, Ganze, Kilifi, ana hofu kubwa. “Tuliteswa sana chini ya machifu. Walikuwa na polisi wenye silaha. Walitunyanyasa. Na sasa, tunarudi huko tena?” anauliza. “Tulikataa kitu kibaya, kwa nini tukirudie? Watu wengi wasio na hatia wataumia tena.” Anasema ikiwa machifu ni lazima wawe na polisi, basi wawe ni wa jamii hiyo. “Zamani, machifu walitumwa maeneo wasiyoyafahamu, na ndiyo maana walikuwa wakatili. Hawakuwa na uhusiano na watu waliowatawala.” Kwa upande mwingine, Bw Paul Ndunda wa Kisumu, anasema kuwepo kwa polisi wa kusaidia machifu ni kurejesha nidhamu iliyopotea. Anasema zamani, ikiwa chifu na watu wake walifika nyumbani kwako, ilikuwa ni kusuluhisha tatizo au kupata kichapo. “Waliokamatwa walichapwa viboko vikali mpaka hawakuthubutu kufanya kosa tena,” anasema Bw Ndunda. Kumbukumbu zake zinaonyesha kwamba hata wahalifu wadogo waliteswa, huku wengine wakizuiliwa hadi mwezi mzima katika kambi za machifu. “Zamani, machifu walikuwa wakishughullkia kesi nyingi ndogo. Hii ilipunguza msongamano wa kesi mahakamani.” Lakini pia anakiri kuwa katiba ya sasa ya Kenya inaweka mipaka ya mamlaka ya chifu, na inaweza kuzuia unyanyasaji ilivyokuwa zamani. RIPOTI ZA Daniel Ogetta, Maureen Ongala and Angeline Ochieng’