Maambukizi ya maralia yapungua asilimia 6.7

RUVUMA: TAFITI za viashiria vya malaria nchini zinaonesha ugonjwa huo umepungua kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 8.1 mwaka 2022. Upungufu huo ni hatua kubwa zilizofanywa na serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama anasema. Mhagama amesema hayo leo Mei 12, 2025 katika uzinduzi wa awamu ya pili …
RUVUMA: TAFITI za viashiria vya malaria nchini zinaonesha ugonjwa huo umepungua kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 8.1 mwaka 2022.
Upungufu huo ni hatua kubwa zilizofanywa na serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama anasema.
Mhagama amesema hayo leo Mei 12, 2025 katika uzinduzi wa awamu ya pili ya ugawaji wa dawa za kuua viuadudu vinavyosababisha uwepo wa mbu wanaozalisha ugonjwa wa malaria katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Peramiho.
Amesema mikoa mengine maambukizi yapo juu ikiwemo Tabora 20%, Kagera 18%, Shinyanga 16%, hata hivyo kuna mikoa ambayo maambukizi ni chini ya asilimia 1 ikiwemo Arusha, Manyara, Dar es Salaam, Songwe, Mwanza, Iringa na Singida
“Vifo vinavyotokana na malaria vimepungua kutoka vifo 6,311 kwa mwaka 2015 hadi kufikia vifo 1,503 kwa mwaka 2024, tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake,” amesema Mhagama.
“Leo tumezindua awamu hii ya pili ya kugawa dawa za viuadudu vinavyosababisha uwepo wa ugonjwa wa Malaria ambazo zitatumiwa na halmashauri zote nchini kwa kuwa ni lazima sasa hivi tujikite katika kudhibiti mbu wanaoeneza ugonjwa wa malaria ambao ni kati ya magonjwa yanayosababisha vifo nchini,” amesema Waziri Mhagama.
Aidha, Mhagama amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametenga Sh bilioni 10 ili kununua lita 833,333 ambazo ni dawa za viuadudu vya malaria zinazozalishwa nchini (Kibaha, Pwani) ambazo zitasambazwa katika halmashauri zote ili kukomesha uwepo wa mbu hao.
“Awamu ya kwanza dawa hizi tulizigawa katika halmashauri 57, Mhe. Rais ameiagiza Wizara ya Afya kuendelea kugawa dawa hizo katika halmashauri 127 zilizobakia ikiwemo Halmashauri yetu ya Wilaya ya Songea, tunamshukuru sana Mhe. Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kujali afya za Watanzania,” amesema Waziri Mhagama.
Pia, Waziri Mhagama amezindua ugawaji wa Portable Digital X-Ray Mashine kwa ajili ya kupima viashiria vya uwepo wa ugonjwa wa kifua kikuu (TB) ili kupunguza maambuzi ya ugonjwa kwani mgonjwa mmoja wa TB ana uwezo wa kuambukiza watu 15-20.
Vifaa vingine vilivyozinduliwa ni mitambo ya Oxgen, mashine ya kumsaidia mtoto kupumua pamoja na mashuka na kitanda kutoka MSD.
“Tunawashukuru sana wadau wetu (Doris Mollel Foundation, Exim Bank, Amref Health Afrika, FREE O2, IFKARA Health Institute, CRDB Bank) kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ili kwa pamoja tuweze kuboresha huduma za afya nchini,” amesema Waziri Mhagama.