Maambukizi matende, mabusha yapungua 96%
SERIKALI imesema kati ya halmashauri 119 nchini zilizokuwa na ugonjwa wa matende na mabusha halmashauri 114 ambazo sawa…
The post Maambukizi matende, mabusha yapungua 96% appeared first on HabariLeo.
SERIKALI imesema kati ya halmashauri 119 nchini zilizokuwa na ugonjwa wa matende na mabusha halmashauri 114 ambazo sawa na asilimia 96 zimefanikiwa kupunguza maambukizi na kuendesha zoezi la ugawaji wa kingatiba ngazi ya jamii.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri wa Afya Jenista Mhagama amesema kwa ugonjwa wa trakoma au vikope, kati ya halmashauri 69 zilizokuwa na maambukizi, halmashauri 61 sawa na asilimia 88 zimefanikiwa kupunguza na hivyo kusitisha zoezi la umezeshaji wa kingatiba katika ngazi ya jamii.
Waziri Mhagama amesema kuwa kwa upande wa ugonjwa wa usubi, maambukizi yamepungua wastani wa asilimia 20 hadi 70 kabla ya udhibiti hadi viwango vya kati ya asilimia 0.1 na 10 baada ya udhibiti katika halmashauri 30 nchini.
–
Amesema upande wa magonjwa ya minyoo ya tumbo na kichocho ambayo ni tatizo kwenye jamii katika halmashauri zote 184 bado mpango wa serikali kudhibiti magongwa yasiyopewa kipaumbele unaendelea kumezesha kingatiba.
“Hata hivyo umezeshaji wa kingatiba ngazi ya jamii bado unaendelea katika halmashauri zote thelathini. Kwa upande wa magonjwa ya minyoo ya tumbo na kichocho ambayo ni tatizo kwenye jamii katika halmashauri zote 184 bado mpango unaendelea kumezesha kingatiba,” amesema Mhagama.
Mhagama ametoa takwimu hizo ikiwa ni Siku ya Kilele Maadhimisho ya Siku ya Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele yenye kauli mbiu ‘Tuungane Tuchukue Hatua, Kutokomeza Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele’ ambapo pia amesisitiza usafi wa uso na usafi wa mwili, matumizi ya vyoo bora na usafi wa mazingira ili kudhibiti magonjwa hayo.
Amesema kati ya aina 21 za magonjwa yasiyopewa kipaumbele duniani, serikali imeamua kujikita na aina tano za magonjwa ambazo ni matende na mabusha (ngirimaji), trakoma (vikope), usubi, kichocho, na minyoo ya tumbo.
Amesema kuanzia Novemba hadi Desemba 2024 halmashauri 130 zilifanya zoezi la kumezesha kingatiba za ugonjwa wa kichocho na minyoo ya tumbo kwa kutumia fedha za ndani ambapo mchango wa serikali ulikuwa ni Sh bilioni 38.765 sawa na asilimia 16.7 ya gharama zilizotumika katika ununuzi, ugomboaji, utunzaji na usambazaji wa shehena za dawa, vifaa tiba na vitendanishi nchini.
Waziri Mhangama ametaja makundi ya walengwa wa magonjwa hayo kuwa ni watoto wa miaka mitano hadi 14 na makundi maalumu yaliyo katika mazingira hatarishi dhidi ya magonjwa hayo. Amesema licha ya kusababisha usumbufu mkubwa kwa waathirika, pia yanaongeza matumizi ya rasilimali chache katika kuyakabili.
Amesema serikali kwa kushirikiana na wadau imepata fedha pamoja na madawa ya kutibu na kukinga magonjwa hayo ambapo kwa kushirikiana na wadau mwaka 2024 wametoa dawa za kingatiba za kudhibiti na kutokomeza magonjwa hayo.
Amesema watu 257,358 kati ya 265,217 walipatiwa kingatiba za kutokomeza ugonjwa wa matende na mabusha kutoka kwenye Halmashauri za Mtama na Mtwara Mikindani sawa na asilimia 97, watu milioni 5,462,851 kati ya 6,447,157 kutoka katika halmashauri 24 walipatiwa kingatiba ya ugonjwa wa usubi sawa na asilimia 85, watu milioni 1,603,425 kati ya 1,967,143 kutoka halmashauri 7 za Ngorongoro DC, Monduli DC, Longido DC, Kiteto DC, Simanjiro DC, Mpwapwa DC na Kalambo DC, walipatiwa kingatiba za ugonjwa wa trakoma sawa na asilimia 82, watoto wenye umri wa kwenda shule (yaani umri wa miaka 5-14) 9,896,694 walilengwa kupatiwa huduma ya kingatiba kwa ugonjwa wa minyoo ya tumbo.
Amesema hadi kufikia Disemba 2024 watoto 8,676,234 sawa na asilimia 88 walimeza kingatiba. Aidha, kwa ugonjwa wa kichocho walengwa wa kumeza kingatiba walikuwa 8,145,947 kati ya hao watoto 6,289,884 sawa na asilimia 77 walimeza Kingatiba tajwa. Walengwa hao walifikiwa katika halmashauri 171 sawa na asilimia 93 ya halamashauri zote.
The post Maambukizi matende, mabusha yapungua 96% appeared first on HabariLeo.