Kreta ya Ngorongoro na ujio wa faru weupe

Habari Leo
Published: Mar 14, 2025 08:57:27 EAT   |  Travel

KRETA ya Ngorongoro ipo katika Eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ambalo ni la kipekee duniani…

The post Kreta ya Ngorongoro na ujio wa faru weupe appeared first on HabariLeo.

KRETA ya Ngorongoro ipo katika Eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ambalo ni la kipekee duniani likiwa na hadhi tatu zinazotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Moja ya hadhi hizo ni kuwa Hifadhi ya Binadamu na Biolojia. Hii ni hadhi inayothibitisha umuhimu wa uhifadhi endelevu unaojumuisha binadamu na mazingira ya asili.

Akizungumza na vyombo vya habari hivi karibuni kuelezea mafanikio ya NCAA kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Kamishina wa Uhifadhi wa NCAA, Dk Elirehema Doriye anasema nyingine ni hadhi ya Urithi wa Dunia Mchanganyiko inayotambua thamani ya kipekee ya maliasili na urithi wa kiutamaduni katika hifadhi hiyo.

“Nyingine,” anasema; “Ni Ngorongoro Lengai UNESCO Global Geopark yaani Hifadhi ya Jiolojia ya Dunia inayohusisha mandhari ya kipekee ya kijiolojia, milima, volkano na mabonde yanayoelezea historia ya mabadiliko ya dunia.”

Mwaka 2023, Hifadhi ya Ngorongoro ilichaguliwa na Mtandao wa World Travel Awards kama Kivutio Bora cha Utalii Barani Afrika.

Anasema, “Hii ni heshima kubwa inayothibitisha umuhimu wa hifadhi hii katika utalii wa  imataifa.” Upandikizaji wa faru weupe Machi 4, 2025, serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ilipokea faru weupe 17 kutoka Kampuni ya AndBeyond ya Afrika Kusini na faru hao wakapandikizwa ndani ya Kreta ya Ngorongoro.

 

Katika hafla ya kupokea faru hao katika eneo la Kreta ya Ngorongoro, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana anasema faru hao kutoka Afrika Kusini ni wa awamu ya kwanza na kwamba, awamu ya pili itahusisha faru wengine 19 watakaopelekwa maeneo mengine ya uhifadhi nchini.

Anasema mradi wa kupeleka faru weupe Tanzania unalenga kuimarisha shughuli za uhifadhi na kupanua wigo wa watafiti ambao kupitia faru hao watasaidia kutoa elimu kwa wananchi na hata wageni wenye lengo la kujifunza kuhusu maisha ya wanyama hao.

Chana anasema kutokana na uwezo na uzoefu wa Ngorongoro na Tanzania kwa ujumla, yapo matarajio makubwa ya faru hao kuongezeka na kustawi kwani uwezo na uzoefu wa Tanzania katika sekta ya uhifadhi ni mkubwa.

“Ushirikiano wetu ulianzishwa na waasisi wetu Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Nelson Mandela na sasa hatua hii ya kutukabidhi faru hawa, inadhihirisha mwendelezo wa uhusiano wetu mzuri. “Ombi langu ni kwamba, tuendeleze ushirikiano huu kusukuma maendeleo yetu mbele,” anasema Dk Chana.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA Jenerali Venance Mabeyo, anasema kuwasili kwa wanyamapori hao katika Kreta ya Ngorongoro kumeandika historia mpya kwa Tanzania kwani nchi itaongeza uhifadhi wa wanyama hao kwa ajili ya kizazi kijacho.

Anasema NCAA itaweka kipaumbele katika usalama wa faru na kushirikiana na wadau wa uhifadhi kuendeleza mikakati madhubuti ya kupambana na kudhibiti ujangili hasa kwa kutumia teknolojia za kisasa. Hizi ni pamoja na teknolojia ya ufuatiliaji kwa kutumia ndegenyuki, vikosi maalumu vya doria na mifumo mingine ya ufuatiliaji ukiwa wa GPS.

Kamishina wa Uhifadhi wa NCAA, Dk Elirehema Doriye anasema, “Ngorongoro tunajivunia kuwa moja ya maeneo machache Afrika ambapo faru weusi wanaendelea kustawi. “Kwa kushirikiana na taasisi nyingine za utafiti za kitaifa na kimataifa, tumefanya tathmini ya kina na kuhakikisha Ngorongoro inakidhi mahitaji ya faru weupe ili kuendelea kuimarisha uhifadhi.”

Katika mazungumzo na waandishi wa habari Dodoma Machi 10, mwaka huu, Dk Doriye anasema, “Mamlaka, baada ya kufanya tafiti kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), ilijiridhisha kuwa eneo la Kreta ni salama na bora kwa ustawi wa wanyama hawa.”

Anasema kwa sasa faru hao 17 walioplekwa Ngorongoro kuimarisha shughuli za uhifadhi wanaendelea vizuri ndani ya Kreta ya Ngorongoro na wanafurahia kuwepo Tanzania kwani hawana changamoto yoyote na wanafurahia hali ya hewa ya Tanzania.

Kwa mujibu wa Dk Doriye, hao wamepelekwa na kupandikizwa katika Kreta ya Ngorongoro kutokana na wanyamapori hao ambao ni kivutio kikubwa cha utalii kuwa katika hatari ya kutoweka. Hii ina maana kuwa, ni hatua ya kuimarisha uhifadhi wa wanyama hao walio katika hatari ya kutoweka duniani pamoja na faru weusi ambao Kreta ya Ngorongoro inasifika kwa kuwa mahali salama kwao.

“Lengo letu ni kuhakikisha hawa faru wanahifadhiwa kwa usalama, kwani wako hatarini kutoweka. Ikiwa idadi yao  itapungua kule walikotoka, wataweza kurejeshwa kutoka hapa na kupandikizwa tena Afrika Kusini,” anasema. Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kulinda wanyamapori adimu ili kudumisha urithi wa taifa na kukuza utalii endelevu.

Ilibainika kuwa, upandikizwaji huo wa faru weupe umezingatia usalama na uhakika wa malisho ya majani mafupi. Mwakilishi wa viongozi wa mila kutoka Afrika Kusini, iNkosi Zwelinzima Gumede anasema lengo la kutoa faru hao kwa Tanzania ni kuendeleza juhudi za uhifadhi na uzalishaji wa faru weupe nchini Tanzania.

Aidha, alisema lengo lingine ni kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Afrika Kusini ulioasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere na Rais Nelson Mandela. “Kabla ya kuleta faru hawa hapa Ngorongoro watalaamu wetu walikuja kujiridhisha na uhifadhi wa eneo hili na pia tumeona tafiti mbalimbali zinaonesha hifadhi hii ni nyumbani kwa faru tena wakiwa katika maeneo yao ya asili…” anasema.

Gumede ambaye ni kiongozi wa mila wa jamii ya Makhasa iliyopo Afrika Kusini anasema wataendelea kushirikiana na Tanzania kulinda wanyama hao ili wazidi kuongezeka. Anafahamisha namna Afrika Kusini ilivyopitia wakati mgumu wa majangiri tangu mwaka 2008 na kwamba, hadi mwaka 2023 takribani faru 10,000 walikuwa wameuawa.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, Hifadhi ya Munywana imekuwa ikisambaza faru wake katika nchi za Botswana, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na sasa Tanzania ili kuhakikisha faru weupe wanaongezeka katika ukanda wa Afrika.

“Sisi, Hifadhi ya Munywana tunaahidi ushiriikiano wakati wowote mtakapotuhitaji ili kuendeleza mapambano dhidi ya ujangiri wa faru weupe,” anasema Gumede. “Kimsingi wanakula nyasi na kreta, uwepo wa nyasi ni mkubwa. Hii itafanya watalii waweze kuwaona faru kwa urahisi tofauti na ilivyo kwa faru weusi ambao wanakula majani ya juu na muda mwingi hujificha.”

Mdau anena Mmoja aliyejitambulisha mtandaoni kwa jina la Hilary Swai ameandika: ‘Mpaka wenzetu wanakubali faru wapelekwe Kreta ni kwamba ‘research’ (utafiti) imefanyika na kuridhia kwenye kila ‘angle’ (namna). Kikubwa wenzetu wenye dhamana ya kuwalinda na kuwatunza wafanye kazi yao kwa ufasaha.”

Anaongeza: “Tunajua wenzetu (majirani) hawakupenda hili litokee hapa kwetu kwa kuwa ndilo ‘product’ (zao) inayouza sana (kwao).” Walivyo faru weupe Kamishina wa Uhifadhi wa NCAA anasema kuna tofauti kidogo kati ya faru weupe na weusi. Kwamba, faru weupe hula nyasi na wale weusi na wanapendelea kukaa maeneo tambarare.

“Ndiyo maana tumeona hapa panafaa zaidi kwa ustawi wao tofauti na wale weusi wanaopenda kukaa maeneo yenye vichaka na kula majani ya juu juu, hivyo ulinzi wa hawa viumbe unamtegemea kila Mtanzania,” anasema Dk Doriye. Kwa mujibu wa vyanzo mtandaoni, faru ni wanyamapori wakubwa wa familia ya ‘Rhinocerotidae.’ Hufahamika kwa umbo lao kubwa na ni miongoni mwa wanyama wala nyasi wakubwa.

Wana uwezo mkubwa wa kusikia na kunusa, lakini uoni wao ni hafifu. Weusi huishi kwa miaka 60 na zaidi. Tofauti kubwa kati ya faru mweupe na faru mweusi ni muundo wa midomo yao. Faru mweupe ana mdomo mpana kwa ajili  ya kula nyasi huku mdomo wa faru mweusi ikiwa imechongoka kiasi.

Faru weupe kwa mwonekano ni wa kijivu. Neno ‘mweupe’ ni tafsiri ya neno la Kiingereza ‘white’. Nadharia maarufu ni kwamba, neno hilo linatokana na neno la Kiholanzi ‘wijd’ au la Kiafrikaans ‘wyd’ linalomaanisha ‘pana’ kwa kuwa midomo yao ni mipana na yenye umbo la mraba.

The post Kreta ya Ngorongoro na ujio wa faru weupe appeared first on HabariLeo.