Katambi: Sheria inawalinda watumishi wajawazito

NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amewataka watumishi wa sekta binafsi na sekta isiyo rasmi ambao wamefukuzwa kazi na kuna viashiria kuwa kumetokana na kupata ujauzito, kwenda kutoa taarifa kwa ofisa kazi wa mkoa ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mwajiri. Katambi alisema hayo jana bungeni wakati wa …
NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amewataka watumishi wa sekta binafsi na sekta isiyo rasmi ambao wamefukuzwa kazi na kuna viashiria kuwa kumetokana na kupata ujauzito, kwenda kutoa taarifa kwa ofisa kazi wa mkoa ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mwajiri.
Katambi alisema hayo jana bungeni wakati wa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Alice Kaijage (CCM).
Katika swali lake, Alice alitaka kujua mkakati wa serikali wa kuwatetea watumishi wanawake katika sekta binafsi na isiyo rasmi ambayo wamekuwa hawahuishiwi mikataba yao ya ajira kutokana na kupata ujauzito.
Alice alitaka pia kujua mpango wa serikali wa kuziwezesha kifedha na kwa rasilimaliwatu vyombo vya ukaguzi ili kuhakikisha zinatekeleza sheria.
Akijibu maswali hayo, Katambi alisema wanawake wanaopata ujauzito wakiwa kazini au kunyonyesha wanalindwa na sheria ambayo inatoa haki ya kupewa likizo ya uzazi, kunyonyesha na hata kama amejifungua watoto njiti.
“Ikitokea mwajiri anamfukuza kazi mwanamke kwa kuwa amepata ujauzito hatua za kisheria zitachukuliwa, hivyo ikitokea mwanamke anaona kufukuzwa kwake kazi kuna viashiria vya yeye kupata ujauzito basi akamuone ofisa kazi mkoa husika ili mwajiriwa wake huyo achukuliwe hatua stahiki,” alisema.
Katika swali la msingi, Alice alitaka kujua ni kwa namna gani serikali inalinda haki ya kufanya kazi kwa watumishi wanawake wa sekta binafsi na zisizo rasmi wanaoachishwa baada ya kuwa na ujauzito.
Akijibu swali hilo, Katambi alisema serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kulinda haki za wafanyakazi wote nchini wakiwemo wanawake.
Alizitaja hatua hizo ni pamoja na kuzifanyia marekebisho sheria za kazi ikiwemo yaliyopitishwa na bunge Februari, 2025 ambayo pamoja na mambo mengine, yameboresha haki ya likizo ya uzazi kwa wafanyakazi wanawake wanaojifungua watoto njiti.
Alisema pia kutoa mwongozo wa waajiri wa kuandaa sera za kuondoa ubaguzi katika maeneo yao ya kazi.
Pia, kuendelea kufanya kaguzi katika maeneo ya kazi na kuchukua hatua stahiki pindi inapobainika kuwepo kwa ukiukwaji na kutoa elimu kwa wafanyakazi ili kuwawezesha kufahamu haki zao, ikiwemo haki ya kufungua mashauri CMA endapo wameachishwa kazi isivyo halali.