Kampuni ya Utalii yatoa msaada wa baiskeli kwa wanafunzi

Mtanzania
Published: Mar 22, 2025 13:44:34 EAT   |  Travel

Na Malima Lubasha, Serengeti Kampuni ya Kitalii Nomad Tanzania inayofanya shughuli katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara, imetoa msaada wa Baiskeli 10 zenye thamani ya Sh 2 .0 milioni kwa wanafunzi wa kike wa kidato cha kwanza wanaotoka kijiji cha Mbirikiri na kusoma Shule ya Sekondari Sedeco kutokana na umbali ulipo ili kuepuka […]

Na Malima Lubasha, Serengeti

Kampuni ya Kitalii Nomad Tanzania inayofanya shughuli katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara, imetoa msaada wa Baiskeli 10 zenye thamani ya Sh 2 .0 milioni kwa wanafunzi wa kike wa kidato cha kwanza wanaotoka kijiji cha Mbirikiri na kusoma Shule ya Sekondari Sedeco kutokana na umbali ulipo ili kuepuka vishawishi na utoro.

Makabidhiano ya baiskeli hizo yalifanyika mbele ya Ofisa Mtendaji Kijiji cha Mbirikiri, Yohana Senteu, Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi, Hamisi Mega na wawakilishi wa kampuni ya Nomad Tanzania kupitia Meneja wao wa kanda ya Serengeti, Lawrence Ghadwe yaliyofanyika katika viwanja vya shule hiyo.

Ghadwe amesema kampuni hiyo imetoa msaada wa baiskeli kwa wanafunzi wa kike 10 na kubakia wengine watano ambao watasaidiwa baadaye baada ya kutembea umbali wa kilometa 10 kwenda na kurudi kutoka shule.

Akizungumza na wazazi, wananchi, walimu na wanafunzi hao amesema msaada huo umetokana na faida wanayopata katika shughuli zao za utalii kuirejesha kwa jamii ya vijiji vinavyopakana na hifadhi ya Serengeti ambapo walitaka baiskeili hizo kutunzwa vizuri huku wakisisitiza wanafunzi hao kusoma kwa bidii.

Meneja wa Kampuni ya Nomad Tanzania Lawrence Ghadwe akizungumza na wazazi,wanafunzi waliopata msaada wa Baiskeli hafla ya makabidhiano yaliyofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Mbirikiri

Aidha Ofisa Mtendaji wa Kijiji Yohana Senteu amewaonya na kuwataka wazazi kuwapunguzia kazi za nyumbani ili watoto wapate muda mzuri wa kujisomea na kufanya mazoezi ya nyumbani wanayopewa na walimu ambapo alisisitiza baiskeli hizo zitumike vizuri na watafuatilia matumizi sahihi yaliyokusudiwa ya baiskeli hizo.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mbirikiri, amesema kwa kushirikiana na uongozi wa kampuni hiyo, walikubaliana nini kifanyike ili kuwasaidia watoto wa kike wa kijiji hicho wanaosoma sekondari ili wafikie ndoto zao wasipate adha ya kutopenda shule na hasa kuchelewa kwenda na kurudi kutoka nyumbani na shuleni kutokana na umbali hali iliyosababisha utoro na vishawishi njiani.

“Wazazi wenzangu napenda kuwajulisha kuwa baada ya kuona watoto wetu wa kike waliokuwa wanasoma shule hii na wamefaulu kwenda sekondari kukabiliwa na changamoto mbalimbali njiani pamoja na kushindwa kuhudhuria shuleni vizuri ikichangia utoro nikaona nitafute wadau wa elimu Kampuni ya Kitalii ya Nomad Tanzania kuwaomba kufanikisha zoezi hili na sasa mnaona watoto wanakwenda shule kila siku na kusoma vizuri,” amesema Mega

Mwalimu Mega amesema suala hilo limeongeza chachu ya kusoma na kupenda shule kwa watoto wa kike waliopo shule ya msingi kama motisha na wao waweze kusoma kwa bidii na kutokatisha masomo ili watimize ndoto zao kwa kuwaonba wadau wa elimu kufanikisha zoezi la kutoa msaada wa baiskeli kwa wanafunzi kidato cha kwanza wanaotembea umbali mrefu zaidi ya kilometa 5 kwenda Sedeco Sekondari kutoka kijijini hapo.

Aidha wazazi, wanafunzi na wananchi wameipongeza kampuni hiyo kutoa msaada kwa watoto wao, kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu na kusema wameupokea kwa mikono miwili baiskeli hizo na kuahidi kuzisimamia kwa uadilifu mkubwa kwa kuzitunza, kuzitengeneza zinapopata hitirafu ili wamalizapo kidato cha nne waweze kuwaachia wengine na kuonya zisitumiwe na wazazi kwa shughuli zisizo za elimu.

“ Tunaipongeza kampuni yenu kwa kuona changamoto waliyonayo watoto wa kijiji hiki kwani kila siku wanatembea kwenda kijiji cha Bonchugu ilipo sekondari ambako ni mbali hali ambayo inasababisha baadhi ya wasichana kuwa watoro hivyo msaada huu wa baiskeli ni mkombozi tunaomba muendelee kuwasaidia wengine pia tunaahidi kuwapa nafasi ya muda wa kujisomea usiku,” wamesema wazazi hao.