Kafulila atoa somo deni la taifa

Habari Leo
Published: May 28, 2025 06:41:30 EAT   |  Educational

MKURUGENZI wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), David Kafulila amesema ingawa deni la taifa linaongezeka, uchumi wa nchi ni himilivu. Kafulila amesema wastani wa deni la serikali kwenye uchumi ni takribani asilimia 47. Kafulila ameyasema hayo katika Ukumbi wa Maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam …

MKURUGENZI wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), David Kafulila amesema ingawa deni la taifa linaongezeka, uchumi wa nchi ni himilivu.

Kafulila amesema wastani wa deni la serikali kwenye uchumi ni takribani asilimia 47.

Kafulila ameyasema hayo katika Ukumbi wa Maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika kongamano kuhusu nafasi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Amesema ingawa deni linaongezeka uchumi ni himilivu ukilinganishwa na mwenendo wa uchumi wa nchi nyingi Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Alisema taarifa ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) ya Oktoba mwaka jana inaonesha uchumi wote wa dunia unaendeshwa kwa mikopo na mwaka jana deni la dunia lilikuwa zaidi ya Dola za Marekani trilioni 10.

“Huu ni mwenendo wa dunia deni kuongezeka na sababu kubwa ya duniani kote ukiacha mazingira ambayo yamejitokeza hapo katikati ni Covid-19 na madhara yake yaliyotengeneza mahitaji zaidi ya kukopa ili kuokoa uchumi,” alisema Kafulila.

Alisema ipo tofauti kubwa ya wastani wa deni la serikali katika nchi nyingine za Afrika na Tanzania, na akatoa mfano baadhi ya nchi za Afrika kwamba wastani wa deni la serikali kwenye uchumi kwa Kenya ni asilimia 70, Rwanda ni asilimia 71, Malawi asilimia 84 na Ghana asilimia 90.

“Katika muktadha huo ndiyo msingi wa kusema kwamba pamoja na deni kuongezeka bado uchumi ni himilivu ukilinganisha na mwenendo wa uchumi wa nchi nyingi Kusini na Mashariki mwa Afrika,” alifafanua Kafulila.

Alisema kumekuwa na urahisi wa Tanzania kupata mikopo nafuu kutokana na makadirio ya mikopo yaliyafanyika wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne na matokeo yake yalionesha hali nzuri kuliko nchi zote za Afrika Mashariki na nchi nyingi Kusini mwa Afrika.

Akizungumzia malengo ya kufikia uchumi wa Dola za Marekani trilioni moja kufikia mwaka 2050, Kafulila alisema malengo hayo yanaweza kuonekana makubwa ya kuzidi uwezo lakini yanaweza kufikiwa kama yatafanyika mabadiliko ya namna mambo yanavyofanyika.

Aidha, Kafulila alisema ufanisi katika taasisi ni msingi wa kuimarisha ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma utakaosaidia kukuza uchumi.

Alisema tafiti zinaonesha katika mataifa 13 makubwa kiuchumi duniani, asilimia 65 ya ukwasi wao umetokana na ufanisi wa taasisi na asilimia 62 imechangiwa na rasilimaliwatu na asilimia tano ni maliasili.

“Hizi nchi zimeendelea sana katika teknolojia na ufanisi wa taasisi kiasi ambacho maliasili siyo mjadala mkubwa kwao kwa sababu teknolojia na uwezo wa taasisi zinaamua sehemu kubwa ya ushindani katika dunia ya ushindani,” alisema Kafulila.

Aliongeza: “Ukifanya tathmini ya miundombinu ya umeme, barabara, bandari, reli na kadhalika, hali tuliyonayo unaweza kuona ni kiasi gani tunahitai uwekezaji na uwekezaji huo hauwezi kutimizwa kwa tozo, kodi na mikopo kwa sababu ni uwekezaji mkubwa ambao unahitaji vyanzo mbadala vya kifedha”.