JIFUNZE LUGHA: Matumizi yasiyofaa ya kitenzi kisaidizi ‘weza’

DHANA ‘weza’ hutumiwa kama kitenzi kisaidizi katika mawasiliano. Katika miktadha michache ambapo kitenzi hiki hutumiwa kikiwa peke yake, hudhamiriwa kuibua maana mahususi.
Kwa mfano, kauli ‘kumweza mtu’ hurejelea kitendo cha kumdhibiti au kumzuga mtu kiasi cha kumfanya kutenda unalolitaka.
Kutokana na kitenzi ‘weza’, huundwa vitenzi vingine kama vile ‘wezekana’ na ‘wezesha’ ambavyo tutavijadili katika makala tofauti.
Katika makala haya, nitaangazia miktadha ambapo kitenzi ‘weza’ hutumiwa visivyo katika mawasiliano kama kitenzi kisaidizi.
Dhana kitenzi kisaidizi hutumiwa kwa maana ya kitenzi kinachotokea sambamba na kitenzi au vitenzi vingine katika tungo ambapo hiki cha kwanza hukisaidia cha pili katika kulikamilisha wazo fulani.
Aghalabu kitenzi ambacho ni kitovu cha mjadala wetu hutumiwa visivyo katika tungo zinazorejelea matukio ambayo tayari yametendeka.
Hata katika tungo zilizo katika nyakati na hali nyingine, kitenzi hicho hutumiwa kwa wingi kama ‘kishikizi’ tu pasi na kutekeleza dhima maalumu.
Suala hili mara nyingi huanzia katika mazungumzo kabla ya kuhawilishiwa lugha andishi.
Kamusi ya Kiswahili Sanifu inaeleza kuwa dhana ‘weza’ ina maana ya kuwa na nguvu za ujuzi wa kufanya jambo.
Ijapokuwa hiyo ndiyo maana ya msingi ya kitenzi chenyewe, zipo maana nyingine ambazo hueleweka na kujitokeza vyema katika miktadha ya matumizi.
Katika muktadha mmojawapo kitenzi hiki huibua dhana ya kukisiwa kutendeka kwa jambo au kutokea kwa hali fulani kutokana na jambo au hali nyingine.
Tazama mfano huu: Ukinywa maji machafu, unaweza kuugua.
Nitaonyesha jinsi ‘weza’ hutumiwa vibaya kurejelea hali au mambo yaliyokwisha kutendeka.
Hali hiyo hudhihirika wakati vitenzi vyenye viambishi {li} na {me} vya wakati na hali, katika mtawalia huo, hutangulia kitenzi hicho.
Tazama mifano hii: (1) Tuliweza kuwasaidia wenzetu. (2) Tumeweza kufanya kazi hiyo na kutimiza makataa yaliyowekwa.
Katika sentensi tulizozitaja, kitenzi ‘weza’ hakina mchango muhimu katika kutimilika kwa ujumbe.
Hata katika lugha za kwanza za watu, hapana kitenzi kisaidizi ambacho ni kufu ya ‘weza’ inavyotumiwa kimakosa katika lugha ya Kiswahili.
Kwa njia nyingine, kuchopekwa kwacho katika muktadha tulioutaja ni mazoea mabaya ya kuitumia lugha ya Kiswahili. Kauli ‘Watu wanne waliweza kuangamia katika ajali’ ina mantiki gani?
Hata hivyo, kitenzi ‘weza’ kinapotumiwa kwa tukizi kuonyesha mapendekezo au maoni, hali hiyo huenda isichukuliwe kuwa kosa la sarufi.
Mfano: Vijana wanaweza kuanzisha biashara ndogondogo za kujikimu badala ya kuitegemea serikali kuwaajiri.
Ikumbukwe hata hivyo kuwa hii ni tafsiri ya sisisi ya Kiingereza ya ‘they can’ ambayo yamkini ndicho kiini cha kosa tunalolizungumzia.