Janabi ataja vipaumbele vyake saba WHO

Habari Leo
Published: Apr 04, 2025 10:24:03 EAT   |  News

MGOMBEA nafasi ya Ukurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi ametaja vipaumbele…

The post Janabi ataja vipaumbele vyake saba WHO appeared first on HabariLeo.

MGOMBEA nafasi ya Ukurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi ametaja vipaumbele vyake saba akichaguliwa kushika wadhifa huo Afrika.

Profesa Janabi alitaja vipaumbele hivyo wakati akiomba kura za wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa WHO, Kanda ya Afrika.

Alisema kipaumbele chake cha kwanza ni kuhakikisha malengo ya milenia yanatimia Afrika kwa kushirikiana na nchi za Afrika ili kupunguza magonjwa kwa asilimia 68 ya lengo la dunia kutoka asilimia 46 ya sasa.

Alitaja kipaumbele cha pili ni kuwa na vyanzo imara vya mapato ikiwa ni pamoja na kuongeza michango ya ndani ya Afrika kufikia asilimia 50 badala ya hali ya sasa ya asilimia 80 kutegemea wafadhili.

Alisema kipaumbele chake cha tatu ni kuimarisha utayari wakati wa dharura.

Profesa Janabi alisema ni muhimu kwa Bara la Afrika kuwa tayari kukabiliana na dharura za kiafya wakati wote, huku akisisitiza utekelezaji wa udhibiti wa masuala ya afya ya binadamu.

Pia, alisema afya ya mtoto na lishe ni kipaumbele chake kingine akipata madaraka hayo WHO.

Alisema kuenea kwa udumavu kunahusiana na changamoto za lishe hivyo ameahidi kusimamia suala hilo na kuhakikisha tatizo hilo linapungua.

Profesa Janabi alisema Kanda ya Afrika inaongoza kwa vifo vya uzazi na watoto duniani ikichangia asilimia 70 ya vifo vya uzazi na asilimia 56 ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano duniani kote.

Kipaumbele cha tano ni kupambana na magonjwa ya kuambukiza, yasiyoambukiza na yale yaliyopuuzwa kwa kuongeza mikakati ya kudhibiti magonjwa hayo hususani ya kitropiki na kuwahamasisha watu kubadili mtindo wa maisha ili kupunguza maambukizi.

Alisema jambo la sita atakalofanyia kazi ni kukabili usugu wa dawa za antibayotiki ambao kwa sasa ni tatizo linaloongezeka kwa kasi. Tatizo hilo linatajwa kusababisha vifo vya watu milioni 1.27 Afrika.

Alitaja kipaumbele cha saba ni kujenga uwezo wa uzalishaji wa dawa ndani ya Afrika na akatoa mfano janga la Covid-19 kama somo lililoonesha namna Afrika haikuwa tayari kulikabili.

The post Janabi ataja vipaumbele vyake saba WHO appeared first on HabariLeo.