IEBC: Kalonzo alivyoachwa kwenye mataa

Taifa Leo
Published: May 11, 2025 05:00:20 EAT   |  News

KIONGOZI wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, anaonekana kuhusisha kiongozi wa ODM katika hatua ya Rais William Ruto ya kuteua mwenyekiti na Makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) bila kushauriana na upinzani.

Bw Odinga ni mshirika wa Rais Ruto katika Serikali Jumuishi na Bw Musyoka asema walipuuza barua aliyowaandikia kuhusu kushauriana na upinzani kabla ya kuteua mwenyekiti na makamishna wa IEBC.

Akizungumza wakati wa mazishi ya aliyekuwa Mwakilishi Wadi wa Kariobangi North, Joel Munuve, huko Mwingi siku ya Ijumaa, Mei 9, 2025, Kalonzo alisema aliandikia wawili hao kutaka mashauriano na makubaliano kabla ya kuteuliwa kwa wasimamizi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka.

“Tumeona jinsi Rais William Ruto amewasilisha majina ya watu waidhinishwe kuwa mwenyekiti na makamishna wa IEBC. Huwezi kuwa mwamuzi wa mechi ambayo wewe binafsi ni mchezaji,” alisema Kalonzo.

Rais Ruto alimpendekeza wakili Erastus Edung Ethekon kuidhinishwa na Bunge la Kitaifa kuwa mwenyekiti mpya wa IEBC.

Pamoja naye, Rais pia alipendekeza aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu, wakili Moses Alutalala, Mary Karen Chesang Kigen, Hassan Noor Hassan, Francis Aduol na Fahima Abdallah kuwa makamishna wa IEBC.

Haya yanajiri huku ikiibuka kuwa wengi wa walioteuliwa na Rais William Ruto kusimamia uchaguzi mkuu ujao wana uhusiano wa moja kwa moja au usio wa moja kwa moja naye pamoja na Bw Odinga.

Hali hii imezua malalamishi kutoka kwa upinzani kwamba walioteuliwa hawatakuwa waamuzi huru.Baadhi yao wamekuwa washirika wao wa kisiasa awali, mmoja akiwa mshauri wa kisheria wa chama cha zamani cha ANC kilichoasisiwa na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi.

Kiongozi wa chama cha Wiper amemkosoa Rais Ruto kwa kupuuza mapendekezo ya ripoti ya Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (NADCO) ambayo iliteuliwa na Rais na Bw Odinga na ambayo yeye (Kalonzo) alikuwa mwenyekiti mwenza.

Kwa wakati huu, Ruto na Raila wanaonekana kumtenga Bw Musyoka pamoja na mapendekezo ya ripoti hiyo. Akiwasilisha majina ya mwenyekiti na makamishna wa IEBC kwa bunge yaidhinishwe, Rais Ruto alisema alifanya hivyo kwa mujibu wa Sheria ya IEBC.

Hakutaja NADCO.“Hatutaruhusu jambo hili lipite kwa urahisi. Hata hivyo, tuko tayari! Hata Ruto mwenyewe akijifanya mwenyekiti wa IEBC, lazima aondoke!” Kalonzo alisema.

Kalonzo aliongeza kuwa nchi lazima ikombolewe kutoka minyororo ya Rais Ruto, kauli ambayo iliungwa mkono na kiongozi wa chama cha DAP-K, Eugene Wamalwa.

“Umevunja kanuni ya makubaliano na ushauriano ambayo ilikuwa msingi wa mchakato wa Bomas, na tunataka kukuambia kwamba tuko tayari kwa lolote,” alisema Wamalwa.

Bw Wamalwa alisema watamuomba Bw Odinga ili awaunge mkono katika juhudi za kumng’oa Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Alisema Kalonzo alisimama na Raila mara tatu.