Hongera Tamwa, TCRA, asante Rais Samia

KATIKA moja ya kauli zake Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere amewahi kunukuliwa akisema, “Uandishi wa habari ni nyenzo muhimu katika kujenga taifa lenye umoja na maendeleo, vyombo vya habari vinapaswa kuwa na jukumu la kutoa elimu kwa umma, kuhamasisha maendeleo na kuimarisha uzalendo”. Hakuna ubishi kuhusu kauli hii ya Mwalimu Nyerere, kutokana na ukweli …
KATIKA moja ya kauli zake Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere amewahi kunukuliwa akisema, “Uandishi wa habari ni nyenzo muhimu katika kujenga taifa lenye umoja na maendeleo, vyombo vya habari vinapaswa kuwa na jukumu la kutoa elimu kwa umma, kuhamasisha maendeleo na kuimarisha uzalendo”.
Hakuna ubishi kuhusu kauli hii ya Mwalimu Nyerere, kutokana na ukweli kwamba vyombo vya habari vimekuwa na jukumu kubwa la kuhabarisha umma kuhusu masuala ya maendeleo, kuimarisha uzalendo, lakini pia kuhimiza amani nchini.
Kwa hiyo, mchango wa vyombo vya habari yanapokuja masuala ya maendeleo na uzalendo nchini sio kitu cha hiari, bali jukumu la msingi katika kuchangia kuimarisha ustawi wa nchi, kuimarisha uzalendo na kudumisha amani nchini.
Ndiyo maana sisi tumefurahishwa na utoaji wa tuzo za waandishi wa habari zijulikanazo kama ‘Samia Kalamu Awards’ zilizotolewa juzi Dar es Salaam kwa ushirikiano wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zikibeba ujumbe wa ‘Uzalendo ndio ujanja’.
Kwa mujibu wa waandaaji, tuzo hizo zimetolewa kwa wanahabari Watanzania kwa lengo la kuhamasisha, kuhimiza na kukuza wigo wa uchakataji, utangazaji na uchapishaji wa maudhui ya ndani kupitia vyombo vya habari.
Tumeshuhudia kazi nzuri zilizofanywa na waandishi wa habari walioshiriki tuzo hizo wakiwamo wale walioibuka washindi, ambazo zimeonesha kufanyiwa kazi, zimebeba maudhui ya ndani na kubwa zaidi zimeonesha kazi kubwa za kimaendeleo zilizofanyika chini ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Tunazipongeza Tamwa na TCRA kwa kazi hii nzuri na ya kupigiwa mfano ambayo si tu imeonesha kwamba wanahabari nchini wanao weledi na uwezo mkubwa wa kuandika mema ya nchi yao, lakini pia wana uzalendo kwa taifa.
Tunaungana na Rais Samia kusisitiza umuhimu wa wanahabari kuzingatia uzalendo, lakini pia kuhakikisha kalamu zao zinalinda nchi sawasawa na jeshi linavyolinda mipaka yetu.
Kwamba kalamu zitumike katika kujenga umoja wa kitaifa, kuhimiza amani, kudumisha uzalendo na kuiandikia vizuri nchi ili kuvutia uwekezaji.
Sote tunafahamu mchango mkubwa wa serikali na hasa, Rais Samia mwenyewe katika kukuza taaluma ya habari nchini katika uongozi wake, kiasi cha kuwezesha Tanzania kupanda katika uhuru wa habari duniani hadi kufikia nafasi ya 95 mwaka huu.
Kwa hiyo, utoaji wa Tuzo za Waandishi wa Habari za Kalamu ya Samia ni jambo jingine kubwa katika kukuza taaluma ya uandishi wa habari nchini, na waandishi wanapaswa kuendelea kutumia taaluma yao vizuri katika kujenga taifa.