Hii hapa nembo ya asali Tanzania

Habari Leo
Published: Oct 04, 2024 13:09:23 EAT   |  Business

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk Pindi Chana amezindua nembo ya asali ya Tanzania itakayotumika kuitambulisha bidhaa hiyo katika soko la dunia. Uzinduzi huo umefanyika leo Oktoba 4, katika Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki Tabora (BTI) mkoani Tabora. ”Kupitia mradi wa BEVAC imeandaa nembo ya asali ya Tanzania (Tanzania Trade Mark). Uwepo wa …

The post Hii hapa nembo ya asali Tanzania first appeared on HabariLeo.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk Pindi Chana amezindua nembo ya asali ya Tanzania itakayotumika kuitambulisha bidhaa hiyo katika soko la dunia.

Uzinduzi huo umefanyika leo Oktoba 4, katika Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki Tabora (BTI) mkoani Tabora.

”Kupitia mradi wa BEVAC imeandaa nembo ya asali ya Tanzania (Tanzania Trade Mark). Uwepo wa nembo hii utawahakikishia walaji kuwa bidhaa watakayoitumia iko salama na inakidhi viwango vya ubora,”Dk Chana amesema.

Dk Chana ametoa rai kwa wafanyabiashara wa asali ndani na nje ya nchi kuanza kuitumia nembo hiyo ya ubora huku akiielekeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania – Tan Trade yenye jukumu la kusimamia matumizi ya nembo kutoa elimu kwa wafanyabiashara kufahamu faida za matumizi ya nembo hiyo.

SOMA: Ni hatari kuzidisha vijiko 5 vya asali, sukari

Amefafanua kuwa serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wafugaji nyuki kwa kutenga maeneo maalum ya kufugia nyuki (Hifadhi za Nyuki) na kujenga viwanda vinane vya kuchakata na kufungasha mazao ya nyuki katika mikoa ya Tabora, Iringa, Katavi, Singida, Geita na Kigoma.

Amesema serikali imeendelea kutafuta masoko mapya ya asali nje ya nchi ambapo Julai 15, 2024 Tanzania imesaini Itifaki na nchi ya Jamhuri ya Watu wa China inayoruhusu asali ya Tanzania kuuzwa katika masoko ya China.

”Nitumie nafasi hii kuwataka wafanyabiashara wote wenye nia ya kuuza asali China kuwasiliana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ili kupewa utaratibu wa kuuza asali nchini China.” amesema Chana.

SOMA: Wapatiwa mizinga kuongeza uzalisha asali

Waziri Chana ameweka Jiwe la Msingi katika jengo la bweni la wanafunzi wasichana la Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki Tabora ambalo litagharimu Sh bilioni 2.65 na ujenzi wake utatumia muda ya miezi 12.

Amesema hatua hiyo inachochea ushiriki wa wasichana katika maendeleo ya sekta ya nyuki na kutumia fursa hiyo kutoa rai kwa wasichana kuchangamkia fursa hiyo na kujiunga na masomo katika Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki Tabora ili waweze kupata ujuzi utakaowawezesha kuajiriwa au kujiajiri.

Tanzania inazalisha wastani wa tani 33,276 za asali na tani 1,913 za nta kwa mwaka. Kiwango hiki bado ni kidogo ikilinganishwa na uwezo wa uzalishaji wa asali ambao unakadiliwa kuwa tani 138,000 kwa mwaka.

Hata hivyo, kiwango cha asali kinachozalishwa kwa sasa kinaiweka Tanzania katika nafasi ya 14 duniani, nafasi ya Pili Afrika na nafasi ya Kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki na SADC.

The post Hii hapa nembo ya asali Tanzania first appeared on HabariLeo.