Gharama kubwa ya maradhi yasiyosambaa

BI Prisca Githuka alianza kupambana na maradhi yasiyosambaa, miaka 23 iliyopita.
Kwanza kabisa, marehemu dadake aligundulika kuugua aplastic anemia, tatizo la damu linalotokea kwa uboho (bone marrow) unaposhindwa kuzalisha seli mpya za damu ili kuwezesha mwili kufanya kazi vilivyo.
“Kabla ya kugundulika kuwa na maradhi haya, dadangu alilazimika kuongezewa damu kila mwezi, na baada ya kuthibitishwa kwamba alikuwa akiugua ugonjwa huu, daktari alipendekeza afanyiwe upasuaji wa kupandikiza uboho (bone marrow transplant), lakini bima yake ya afya ilikataa kulipia utaratibu huu, na hatimaye akaaga dunia,” aeleza Bi Githuka.
Kisha, miaka 11 baada ya dadake kuaga dunia, Bi Githuka naye aligundulika kuugua kansa ya matiti. “Mambo yalikuwa magumu kwani nilipogundulika kuwa na maradhi haya, ilikuwa katikati ya mwaka, na bima yangu ya afya tayari ilikuwa imetumika kwa kiwango kikubwa, na hivyo ililipia upasuaji wangu pekee,” asema.
Na hivyo tokea alipofanyiwa upasuaji huo, ilikuwa tatizo kupata pesa za matibabu, na hivyo alilazimika kuchanga pesa kutoka kwa marafiki, kuchukua mikopo na hata kuuza baadhi ya rasilimali alizokuwa nazo ili kupokea matibabu.
“Mojawapo ya dawa nilizokuwa nikitumia ilikuwa herceptin, na wakati huo ilikuwa inauzwa kwa dola 3,500 sawa na Sh453,075 za sasa, ambapo nilistahili kutumia dozi 16 za dawa hii tokea nilipofanyiwa tibakemia yangu ya tano, hadi nilipokamilisha tibakemia ya nane. Pia, Nilifanyiwa awamu 30 za tibaredio.”
Na baada ya matibabu haya, alikumbwa na matatizo kwani alianza kukumbwa na matatizo ya utumbo ambapo hadi leo anatumia dawa.
“Aidha, kutokana na sababu kuwa kansa iliyonikumba ilikuwa ya kihomoni, nilianza kutumia dawa za homoni ambazo nimekuwa nikizitumia kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita. Mojawapo ya dawa hizi imekuwa ikinigharimu dola 5 (Sh647) kila siku, kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita.”
Wakati huo huo, mamake ambaye Bi Githuka alikuwa akimshughulikia wakati huu, alikuwa na shinikizo la damu ambapo alikuwa akitumia dawa. “Baadaye akakumbwa na matatizo ya ngozi ya cellulitis, kiharusi, dementia na maradhi ya moyo, ambapo baadaye mkono wake ulikatwa, kabla ya kufariki.”
Ni masaibu ambayo mbali na kumuathiri kisaikolojia, katika kipindi hiki yameigharimu familia yake pesa nyingi na kuacha mzigo wa kifedha.Taswira hii ndio inawakumba wengi barani wanaoendelea kuhangaika kutokana na maradhi yasiyosambaa.
Kulingana na Shirika la Afya (WHO), hii leo, maradhi yasiyosambaa kama vile kansa, maradhi ya moyo, magonjwa ya mfumo wa kupumua na magonjwa ya akili, yanasababisha asilimia 74 ya vifo duniani huku bara la Afrika likionekana kuathirika pakubwa.Takwimu zaidi zinaonyesha kwamba hapa barani asilimia 37 ya vifo vinatokana na maradhi haya.
Hapa nchini, takwimu za WHO zinaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 50 ya Wakenya wanakabiliana na aina moja ya maradhi au zaidi yasiyosambaa, huku takriban asilimia 40 ya vifo vinavyotokea hospitalini humu nchini, vikisababishwa na maradhi haya.
Takwimu hizi za kusikitisha ni mojawapo ya sababu kuu zilizowashinikiza washikadau katika mapambano dhidi ya magonjwa haya, kuandaa kongamano la nne la kimataifa kuhusu maradhi haya hapa barani.Katika kongamano hilo lililofanyika jijini Kigali, Rwanda juma lililopita, zaidi ya wajumbe 700 kutoka mataifa 86 walikutana kujadili jinsi ya kukabiliana na janga hili.
“Aidha, maradhi haya yanatabiriwa,” alisema Bi Katie Dain, Afisa mkuu mtendaji wa muungano wa mashirika yanayopambana na maradhi yasiyosambaa NCD Alliance.Kulingana na wataalam, taswira ilivyo barani imechangiwa na mambo mengi ikiwa ni pamoja na kubadilika kwa mitindo ya kimaisha.
“Kuna vichocheo vingi ambavyo vimesababisha hali hii barani ikiwa ni pamoja na mitindo ya kimaisha. Siku hizi hatufanyi mazoezi, hatuli vyakula vizuri, matumizi ya pombe na bidhaa za tumbaku yamekithiri, huku uchafuzi wa mazingira ukiendelea kuchochea maradhi ya mfumo wa kupumua,” aeleza Dkt Kibachio Mwangi, mshauri wa kimatibabu kuhusu maradhi yasiyosambaa na afya ya akili katika WHO nchini Afrika Kusini.Hali hii imekuwa mbaya hasa wakati huu ambapo Amerika imejiondoa kwenye WHO na kukatiza msaada wa USAID.
“Mataifa mengi ya Afrika yamekuwa yakitegemea msaada ili kufadhili mifumo ya kiafya, na uamuzi huu kando na kuathiri jithada dhidi ya maradhi ya kuambukizwa, utakuwa na athari kubwa kwa wagonjwa wanaogua maradhi yasiyosambaa,” asema Bi Dain.
Kulingana na Bi Dain, japo kwa kawaida maradhi yasiyosambaa hayajakuwa yakipokea kiwango kikubwa cha msaada, kuna uwezekano kwamba huduma za afya zitaathirika pakubwa, ambapo wagonjwa wa maradhi yasiyosambaa huenda wakapuuzwa, huku serikali zikipambana na magonjwa yanayoambukiza kama vile HIV na kifua kikuu (TB).
Ili kukabiliana na tatizo hili, Bi Dain anasisitiza umuhimu wa serikali za Afrika kuanza kuwekeza katika mifumo yao ya afya ili kuepuka shida kila wakati wafadhili wanapoamua kuondoa misaada.
“Ni jambo la kushangaza kwamba baadhi ya serikali hapa barani zinawakeza pesa kidogo sana katika sekta ya afya, huku asilimia moja au mbili pekee ya bajeti zao za afya, zikielekezwa katika mapambano dhidi ya maradhi yasiyosambaa, ilhali watu wengi wanafariki kutokana na magonjwa haya,’ aelza Dkt Mwangi.
Kulingana na Dkt Mary Amuyunzu Nyamongo, mwenyekiti wa bodi ya muungano wa mashirika ya kupambana na maradhi yasiyosambaa nchini NCD Alliance Kenya, hapa nchini, uwekezaji duni wa kifedha katika mfumo wa afya, na hasa katika mapambano dhidi ya magonjwa haya ni kizingiti.
“Suala hili limeathiri utambuzi wa mapema wa baadhi ya maradhi haya, na hivyo kusababisha wagonjwa wengi kugundua hali zao wakiwa tayari wamechelewa. Hii haithiri tu huduma bali pia inaongeza gharama ya matibabu,” asema Dkt Nyamongo.
“Pia, itakuwa muhimu kwa mtaifa ya Afrika kuanza kujumuisha matibabu ya maradhi haya kwenye mifumo ya afya kwa wote UHC,” aeleza.
Rwanda ni mfano wa mataifa hapa barani ambayo yameonyesha mfano mwema. Kwa mfano, asilimia 90 ya raia wamesajiliwa kwenye bima ya afya nchini humo.
“Aidha, tumekuwa tukijitahidi kuhakikisha kwamba baadhi ya huduma na matibabu yanayotolewa kwa wagonjwa wanaougua maradhi yasiyosambaa, yanalipiwa kwa kiwango fulani au kikamilifu na bima hii,” asema asema Dkt Yvan Butera, Waziri wa Afya nchini Rwanda.
Kando na hayo, serikali ya Rwanda pia imechukua hatua ya kuongeza ushuru zinazounda bidhaa ambazo zimehusishwa na baadhi ya maradhi yasiyosambaa.“Kwa mfano, hivi majuzi tuliongeza ushuru kwenye sigara na pombe, na pia tukaongeza bei ya viwandani ya bia kwa asilimia 65,” aongeza Dkt Butera.Na tayari kumekuwa na matokeo.
“Kwa mfano, viwango vya uvutaji sigara vimepungua kutoka asilimia 13 mwaka wa 2012 hadi asilimia 7.1 mwaka wa 2022,” aeleza.Kulingana na Bi Dain hali ilivyo sasa, serikali za Afrika hazina budi ila kugutuka na kutumia mbinu mbadala ili kufadhili mifumo yao ya afya, badala ya kutegemea misaada kutoka kwa wafadhili katika upande huu.