Gachagua anavyorudia makosa yaliyofanya aondolewe serikalini

Taifa Leo
Published: May 15, 2025 02:55:49 EAT   |  News

ALIYEKUWA naibu rais Rigathi Gachagua anaonekana kurudia makosa yaliyomfanya akosane na wenzake serikalini kwa kutoa vitisho vya kisiasa vinavyoweza kuvuruga juhudi za kuunda muungano madhubuti wa upinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Kauli zake dhidi ya viongozi wenzake wa upinzani, Fred Matiang’i na Kalonzo Musyoka, zimeibua maswali kuhusu iwapo dhamira yake ni kuunganisha nchi au kujijenga binafsi kisiasa katika eneo la Mlima Kenya pekee.

Wachambuzi wanasema kauli zake kuhusu vinara wa upinzani na masharti anayowapa zinakinzana na wito wake wa kuunganisha Wakenya ili kumuondoa Rais Ruto mamlakani.

Katika mahojiano na hotuba zake kwenye hafla za umma, Bw Gachagua amekuwa akitoa masharti makali kwa wawili hao, akisisitiza kuwa hawezi kuunga mkono mtu yeyote asiye na uungwaji mkono wa jamii yake.

Hii inaonekana kama kurudia yale ambayo viongozi wa UDA walimlaumu kwa kuendeleza siasa za kikabila na kimaeneo.

Mnamo Jumatatu, Bw Gachagua alisema kuwa licha ya kuwa na sifa za uongozi, Dkt Matiang’i hana maana yoyote bila baraka kutoka kwa jamii ya Kisii.

“Ikiwa hana watu wake nyuma yake, ataenda wapi? Siwezi kumuunga mtu ambaye nyumbani kwao hawamkubali,” alisema katika kauli iliyotafsiriwa kama tishio na dharau kwa waziri huyo wa zamani wa usalama wa ndani na elimu.

“Matiang’i anaonekana kuwa na sifa, ni mchapakazi, lakini ikiwa Kisii hawamuungi mkono kwa sauti moja, azma yake itaenda wapi?” aliuliza Bw Gachagua. Alifichua kuwa ametuma kundi la wafuasi 20,000 katika eneo la Kisii kuchunguza kama kweli Bw Matiang’i anaungwa mkono. Aliongeza kuwa hatamuunga mkono mtu ambaye hajakubalika nyumbani, akisema wazi kuwa, “Siwezi kuwa mjinga kumuunga mtu ambaye watu wake hawamtaki.”

Bw Gachagua amemtaka Dkt Matiang’i kuunda chama chake mwenyewe kukitumia kwa mazungumzo ndani ya muungano wa upinzani, hatua ambayo imekera chama cha Jubilee ambacho kimemteua waziri huyo wa zamani mwenye nguvu kama mgombea wao wa urais.

Wachambuzi wa kisiasa wanachukulia pendekezo hilo la Bw Gachagua kama mbinu ya kulinda ushawishi wake katika eneo la Mlima Kenya, ambapo anatarajia kuzindua chama chake kipya leo.

Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni, amemshutumu Bw Gachagua kwa kuendeleza siasa za “wenyehisa” ndani ya upinzani.

Aliambia Taifa Leo kuwa watakataa jaribio lolote la kuwafanya viongozi wa kitaifa kuwa viongozi wa kieneo.

“Hatuko katika harakati za kutafuta mgombea aliyeteuliwa na viongozi wachache, bali tunataka mtu anayekumbatiwa na wananchi. Kwa kweli, tunapendekeza tafiti za kisayansi zitumike kuchagua mgombeaji ili kuepuka uteuzi kwa misingi ya idadi ya kura kutoka kwa jamii zao,” alisema Bw Kioni.

“Alichosema Gachagua ni sehemu ya fikra zake za wenyehisa ambapo anaangalia mgombea na kura kutoka kwa eneo lake. Anataka kumkumbusha Matiang’i kwamba anatoka kwa jamii ndogo,” alisema.

Mpango wa Gachagua wa kulinda ushawishi katika Mlima Kenya ndio chanzo cha mzozo wake na mshirika wake wa karibu, Bw Ngunjiri Wambugu.

“Siwezi kuunga mkono chama kimoja (cha mlimani) kwa sababu hata kama inanisaidia, si haki kwa wote. Kama mtu anayemcha Mungu, ninasimamia haki na usawa. Siwezi kupoteza misimamo yangu kwa ajili ya manufaa ya muda,” alisema Wambugu.

Mwaka jana, Gachagua alitoa tisho sawa kwa kwa Kalonzo Musyoka.

“Ukambani wana kura milioni mbili – haitoshi. Wakifikisha milioni 4, watutafute. Na Kalonzo lazima aachane na Raila Odinga,” alisema, akimlazimisha Kalonzo kujiondoa kwa mshirika wake wa muda mrefu.

Aliitaka jamii ya Ukambani kuongeza idadi ya wapiga kura kutoka milioni mbili hadi takribani milioni nne kabla ya kudai nafasi ya kuungwa mkono na Mlima Kenya. “Uongozi ni idadi. Mkifikisha kura milioni 3.5 hadi 4, njoo unitafute,” alisema Gachagua.

Wachambuzi wa siasa na utawala wanasema kuwa badala ya kujenga daraja kati ya jamii na vyama mbalimbali, Gachagua anaonekana kuendeleza siasa za masharti na ubinafsi, hali inayohatarisha umoja wa upinzani dhidi ya Rais William Ruto.

“Gachagua anarudia makosa kwa kutoa vitisho vya kisiasa ambavyo vinaashiria hajaacha siasa za masharti, ubinafsi, na ubaguzi wa kisiasa. Kauli zake dhidi ya viongozi wa upinzani Fred Matiang’i na Kalonzo Musyoka zimeibua maswali kumhusu kuelekea 2027,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.

Wachambuzi wengi wa siasa wanatafsiri matamshi yake ya hivi majuzi kama mwendelezo wa tabia hiyo ya kutoa masharti na kujichukulia kama kiranja wa muungano wa upinzani unaosukwa.

“Si ajabu anahepwa na washirika wake hata eneo la Mlima Kenya. Asipobadilisha tabia kuna uwezekano wake kutengwa hata na vinara wa upinzani," asema mchanganuzi wa siasa Beatrice Goreti.

Wakati wa utawala wa Uhuru, Gachagua alikuwa mmoja wa waliokuwa mstari wa mbele kumpinga ndani ya serikali baada yake kuungana na William Ruto wakati huo akiwa naibu rais, hali iliyomfanya kuonekana kama msaliti.

Baadaye, hata baada ya kupewa nafasi kubwa na Rais Ruto, alitengwa na kutimuliwa mamlakani Oktoba 2024.

“Badala ya kuunganisha upinzani dhidi ya serikali ya Ruto, Gachagua anaonekana kurudia makosa ya awali: kutoa masharti, kugawa jamii, na kuweka maslahi ya binafsi mbele ya mustakabali wa taifa huku akitumia wingi wa kura katika eneo la Mlima Kenya,” asema Bi Goreti.