Elimu yahitajika vihatarishi mahala pa kazi

Habari Leo
Published: May 29, 2025 14:37:02 EAT   |  Educational

DAR ES SALAAM: WAFANYAKAZI kutoka taasisi mbalimbali wametakiwa kupata elimu namna ya kudhibiti vihatarishi katika maeneo ya kazi ili kutimiza majukumu yao katika mazingira yenye usalama. Mkurugenzi wa Usalama na Afya wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Dk Jerome Materu amekiri kuwa maeneo mengi ya kazi kuna vihatarishi ila wanaweza wasione athari …

DAR ES SALAAM: WAFANYAKAZI kutoka taasisi mbalimbali wametakiwa kupata elimu namna ya kudhibiti vihatarishi katika maeneo ya kazi ili kutimiza majukumu yao katika mazingira yenye usalama.

Mkurugenzi wa Usalama na Afya wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Dk Jerome Materu amekiri kuwa maeneo mengi ya kazi kuna vihatarishi ila wanaweza wasione athari kutokana wahusika kutokuwa na elimu sahihi.

Akizungumza leo Mei 29 katika Kongamano la Kimataifa la Afya Mahala Pa Kazi lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Dk Materu ameeleza kuwa wafanyakazi wahakikishe taasisi zao zimesajiliwa na Osha ili kurahisisha ukaguzi na kupewa elimu ya kudhibiti vihatarishi hivyo.

“Lengo letu mfanyakazi afanye kazi akiwa na afya njema kuwa na tija kwa kampuni yake na taifa na kupunguza fedha za kigeni kununua vifaa tiba na tiba yenyewe,” amesema Dk Materu.

Ameeleza kuwa tafiti nyingi zinaonesha bila kuzingatia usalama mahali pa kazi athari ni kupoteza muda wa kufanya kazi, taasisi husika kuwajibishwa, kupoteza taswira ya taasisi husika.

SOMA ZAIDI

MUHAS waja na mpango wa mazoezi usimamizi kitabibu

 

Dk Nyarubeli amesema pia kongamano hilo linalenga kujadili tafiti zilizofanyika ili kuunganisha jitihada zao kuona namna ya kutatua changamoto mahala pa kazi, hivyo kutakuwa na mawasilisho ya kisayansi na mijadala ya kisera.

“Moja katika kujenga taalamu yenyewe tuna vyuo ambavyo vimeshiriki kwa mchanga mkubwa kuna Norway na Ethiopia kwa pamoja tumekuwa tukishirikiana katika ufundishaji wa wanataalamu na kufanya tafiti mbalimbali,” amesema Dk Nyarubeli.

“Chuo chetu pamoja na wadau tumefanya taifiti nyingi, ila kikubwa namna gani tunavyoweza kuzuia wafanyakazi wasipate madhara wanapofanya kazi kwa maana ya kinga,” ameongeza Dk Nyarubeli.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Afya ya Mazingira Mahala Pa Kazi kutoka Wizara ya Afya, Joseph Birago kuna ulazima wa kuwekeza kwenye usalama wa afya ili kupunguza magonjwa yatakayoweza kuathiri wafanyakazi kwenye maeneo yao ya kazi.

SOMA ZAIDI

Muhas waandaa kambi uchunguzi magonjwa ya moyo

Amesema magonjwa mengi yamekuwa yakijitokeza taratibu na kuleta ugumu katika tiba hasa kwa kuchukuwa muda mrefu wa matibabu.

“Vizuri wananchi wanaofanyakazi kuchukuwa tahadhari kutokana na kazi na aina ya viashiria ambavyo vinaweza kuleta madhara. Inatofautiana pia na aina yak kazi,” amesema Birago.

Aidha, Profesa Simon Mamuya kutoka MUHAS amesema changamoto nyingi alizofanya kwenye tafiti zake ni baadhi ya watu kutokuwa na uelewa wa madhara ya vitendea kazi na madhara yatokanayo na sehemu zao za kazi.

Prof Mamuya ametolea mfano wa wakulima wanaotumia viuatilifu kuwa wakati mwingine vinaweza kuwa na madhara kwa afya zao, lakini pia sehemu za migodi.

“Uelewa wa madhara ni muhimu sana, ndio maana hapa tunafundisha wataalamu waende kwenye ngazi za wilaya, vijiji waende wakaelimishe, tunakutana mpaka na watunga sera wetu tunazungumza nao waende wakaelimishe,” amesema Prof Mamuya.

Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kinafanya kongamano hilo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Addis Ababa Ethiopia na Chuo cha Bergen kutoka Norway.