Elimu ya malezi yatakiwa Mtwara

BAADHI ya watendaji katika halmashauri mbalimbali mkoani Mtwara wametakiwa kuhakikisha elimu ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali…
The post Elimu ya malezi yatakiwa Mtwara appeared first on HabariLeo.
BAADHI ya watendaji katika halmashauri mbalimbali mkoani Mtwara wametakiwa kuhakikisha elimu ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto inafikia kikamilifu kwa jamii pamoja na wadau kwa ujumla.
Hayo yamejiri wakati wa mkutano wa mapitio ya utekelezaji wa shughuli za Programu Jumuishi ya Taifa ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (PJT-MMMAM) Mkoa wa Mtwara kwa kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2024, uliyofanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani na kukutanisha watendaji hao pamoja na wadau.
Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Theresia Ngonyani amesema elimu hiyo iende kwa kila mtu, mdau ili kwa pamoja waweze kulea watoto wao katika ukuaji uliyotimilika ili mwisho wa siku wawe na wananchi au raia waliyokuwa wema wanaofanya matendo mema pasipo kuwepo mmomonyoko wa maadili.
‘’Halmashauri kupitia kwa waratibu na waratibu wengine katika maeneo matano ya mpango huu wa MMMAM kuweza kuifikia jamii wanayotoka wao wenyewe katika halmashauri zao kuanzia ngazi ya kijiji, mtaa, kata pamoja na halmashauri elimu hii iweze kwenda kwa kila mtu na wadau kwa ujumla’’amesisitiza Ngonyani
Aidha katika malengo ya mpango huo waliyojiwekea watendaji hao ya kuhakikisha wanazifikia shule za awali pamoja na vituo vya kulelea watoto wadogo mchana (Baby Cares), wahakikishe wanafikia malengo husika ya mpango kwa kuwafikia walengwa ambao ni mtoto kuanzia mwaka 0 hadi miaka 8.
Meneja Uchechemuzi wa Mtandao wa Malezi na Makuzi ya Watoto Nchini (TECDEN), Bruno Ghumpi amesema watoto chini ya miaka mitano nchini asilimia 47 wako kwenye ukuaji wao sahihi na asilimia 53 hawako kwenye ukuaji sahihi hali inayowafanya wawekeze zaidi kwenye eneo hilo.
‘’Kwa hali hii inatufanya kuwekeza zaidi kama taifa ili tuwapate hawa watoto wawe na tija kwa taifa, wawe ni watu wenye afya njema, uelewa na wanaoweza kukafanya kazi za uzalishaji’’ amesema Bruno
Mkurugenzi wa Mtandao wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali (MTWANGONET) mkoani humo, Fidea Luanda ametoa ushauri kwa watendaji hao kuwa kwenye mikutano hiyo kuwe na utaratibu unaoruhusu kuwataja watoto wenye mahitaji maalumu kama iliyokuwa watoto wengine ili kuzingatia usawa katika elimu hiyo.
Mwenyekiti wa Baby Cares Mkoa wa Mtwara, Selemani Mkonga amewaomba watendaji hao kuwa pale wanapofanya mikutano yao na wazazi katika shule hizo ni vema wakashirikisha vituo hivyo vya baby cares ili kuboresha zaidi utaoji wa elimu hiyo na mkoa una jumla ya baby cares 180.
The post Elimu ya malezi yatakiwa Mtwara appeared first on HabariLeo.