Elimu kwa wakulima yaongeza tija katika kilimo cha pamba

Habari Leo
Published: Feb 18, 2025 08:48:25 EAT   |  Educational

SERIKALI imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha inalipaisha zao pamba kwenye uzalishaji pamoja na kuliwezesha kupenya kwenye soko…

The post Elimu kwa wakulima yaongeza tija katika kilimo cha pamba appeared first on HabariLeo.

SERIKALI imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha inalipaisha zao pamba kwenye uzalishaji pamoja na kuliwezesha kupenya kwenye soko la dunia.

Kwa kuona umuhimu wa zao hilo, na nia ya kuongeza uzalishaji wake serikali imeamua kutoa pembejeo za zao hilo bure kupitia Bodi ya Pamba Tanzania.

Akizungumza mkoani Simiyu hivi karibuni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anasema ili kuongeza tija katika zao hilo, serikali imeongeza maofisa ugani kupitia mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) ili waweze kuwafikia wakulima kwa
urahisi na kuongeza tija ya uzalishaji wa zao hilo.

Ndege ndogo isiyo na rubani maarufu ‘drone’ ikitumika kunyunyuzia dawa ya kuua wadudu katikashamba la pamba lililopo kijijini Mwamashimba,Kata ya Mwamalasa, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu.

Maofisa hao wamekuwa wakiwafikia wakulima mashambani na kuwaelekeza mbinu za kitaalamu za kilimo cha pamba, jambo ambalo limeonekana kuwasaidia wakulima hao katika maeneo mbalimbali kuweza kuzalisha kwa tija.

Hilo linathibitishwa na wakulima katika kijiji cha Kinampanda kata ya Mwamalasa mkoani Shinyanga ambao wanaonesha wazi kuridhishwa na elimu waliyopata kutoka kwa wataalamu kuhusu kilimo bora cha zao hilo.

Wanakijiji hao walizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Annamringi Macha aliyetembelea mashamba yao hivi karibuni. Mkazi wa kijiji hicho, amelima Ekari kumi kwa kusimamiwa na wataalamu wa kilimo na kufuata kanuni bora za kilimo cha zao hilo peke yake bila kuchanganya na mazao mengine.

Mayunga anasema kupitia wataalamu wa kilimo, wemeweza kujua muda gani ni sahihi kupiga dawa kama ambavyo sasa hivi wakulima wako kwenye kipindi cha kupuliza dawa kwenye mimea ingawa bado wanakabiliwa na changamoto ya vifaa vya kufanyia kazi hiyo.

Anasema kwa sasa wanatumia pampu ya kubeba mgongoni ambayo imekuwa ikiwachosha sana na kuwafanya watumie muda wa takribani siku mbili au tatu kumaliza kupuliza dawa katika shamba la ekari moja. Mkulima mwingine wa Kijiji hicho,

Konga Jinadali anasema amekuwa akifuatilia kilimo cha kisasa cha pamba kwa kipindi chote cha msimu uliopita na kuvutiwa kiasi cha kuamua kujiunga na kilimo cha hicho mwaka huu akiwa na matarajio ya kupata mavuno mengi.

“Mwaka jana nilivuna pamba kidogo kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, kuwa na mvua nyingi na kuiharibu pamba lakini mwaka huu hali ni nzuri matarajio ni kuvuna ekari moja zaidi ya kilo 1,000,” anasema Jinadali.

Naye Diwani wa Kata ya Mwamalasa, Bushi Mpina anasema wakulima wana matarajio ya kupata mavuno mengi baada ya kufuata kanuni za kilimo cha kisasa cha pamba.

Ofisa kilimo kutoka kata ya Mwamalasa, Joseph Msusa anasema kwenye kata hiyo wapo wataalamu watano kutoka Bodi ya Pamba Tanzania kupitia mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) wamekuwa wakifanya kazi kwa ushirikiano.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Annamringi Macha akizungumza na wataalamu wa kilimo pamoja na wananchi walipotembelea Kijiji cha Kinampanda, Kata ya Mwamalasa wilayani Kishapu hivi karibuni. (Picha zote na Kareny Masasy)

Msusa anasema walipatiwa viuatilifu 500 ambavyo vilitosha kuhudumia ekari 14,082 zilizolimwa. Anaongeza kuwa Novemba mwaka jana walipatiwa tani 204 za mbegu za pamba na wana matarajio ya kuvuna kilo 204,000 katika msimu huu.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Annamringi Macha anasema awali wakulima hao walikuwa wakiletewa mbegu zisizo na ubora lakini kwa sasa wamepata mbegu bora jambo ambalo limeleta tija kwa wakulima na amelifurahia.
“Kilichonifurahisha wakulima wamefuata kilimo cha kisasa, sisi tunataka kwa wastani wakulima wavune ekari moja kilo 1,200. Nimewapongeza BBT kufanya kazi kwa bidii katika kila eneo hili,” anasema Macha.

Macha anasema wakulima wenye mashamba makubwa zaidi ya ekari kumi wapewe kipaumbele cha kutumia ndege nyuki kunyunyuzia dawa za kuua wadudu kwenye pamba. Macha anasema baadhi ya wakulima wameendelea
kutumia pampu za mikono hivyo amewataka wataalamu kuelekeza ndege nyuki kwa ajili ya kunyunyuzia kwenye
mashamba yao ili wasipate hasara.

Macha anasema kitaalamu Teknolojia hii ya kutumia ndege nyuki ikisetiwa vizuri ina uwezo wa kunyunyuzia ekari moja kwa dakika sita hivyo jitihada zinatakiwa kufanyika kwa kila mkulima kunyunyuziwa dawa kwenye shamba lake.

“Serikali imeweka kipaumbele katika sekta ya kilimo na maofisa ugani wamewekwa kuanzia ngazi ya vijiji ambao wamepewa vitendea kazi, hizi zote ni jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu katika mikakati ya kuwakomboa wakulima kuinuka kiuchumi,” anasema Macha.

Macha anasema awali wakulima walianza kukikimbia kilimo cha Pamba lakini sasa imani yao imerejea baada ya kuona usimamizi ni mzuri. Aliwataka wakulima kuacha kuchanganya pamba na mazao mengine kwenye shamba moja ili kupata mavuno mengi yenye ubora ili kujiingizia kipato kikubwa kupitia zao hilo.

Msimamizi wa zao la pamba kutoka bodi ya pamba wilayani Kishapu, Thadeo Mihayo anasema kwa mkoa wa Shinyanga zipo ndege nyuki saba lakini mipango iliyopo ni kupata zingine ili kufikia 14.

Mihayo anasema matarajio ya kulima zao la pamba kwa wilaya ya Kishapu mwaka 2024/2025 ni ekari 220,000 hivyo bodi ya pamba ipo tayari na imeendelea kusimamia zao hilo kwa umakini ili kufikia lengo.

Ofisa Kilimo kupitia mradi wa jenga kesho iliyo bora (BBT) Yombi Chedi anasema changamoto iliyokuwepo kwa wakulima wa kata ya Mwamalasa ni kukosa elimu ya kilimo bora kwani walio wengi walikuwa wakichanganya zao la pamba na mazao mengine.

Ofisa kilimo kutoka Halmashauri ya Kishapu Denis Mayomba anaeleza kuwa imepima sampuli 1,405 za udongo katika msimu wa kilimo kwa mwaka 2024/2025 na kubaini mashamba mengi hayana rutuba. “Licha ya wilaya hii kuwa na mifugo mingi hawatumii mbolea ya samadi kuboresha rutuba kwenye mashamba yao na ndiyo sababu ya wakulima kutovuna mazao mengi,” anasema Mayomba.

“Ukosefu wa rutuba kwenye mashamba yao ndiyo yanawafanya washindwe kupata mazao mengi wakati mwingine kuwa na mimea ambayo haina lishe au ulemavu,” anasema Mayomba.

Anasema mashamba kutoka kata 28 za halmashauri hiyo yalipimwa na kila mmiliki wa shamba alisajiliwa kupitia mfumo na udongo wa shamba lake na majibu yalitolewa kwa wahusika sambamba na kupewa ushauri wa kitaalamu.

Mkuu wa Wilaya hiyo Peter Masindi aliwaeleza wananchi wa kata hiyo kuwa hata kama wameelezwa ardhi yao haina
rutuba wasikate tamaa bali wanatakiwa watumie mbolea kwenye mashamba yao kipindi cha kupanda na pia ya kukuzia mimea yao.

The post Elimu kwa wakulima yaongeza tija katika kilimo cha pamba appeared first on HabariLeo.