DC Longido aisifu wizara msaada wa kisheria bure

Habari Leo
Published: Mar 03, 2025 09:19:25 EAT   |  News

ARUSHA: MKUU wa Wilaya ya Longido, Salum Kalli amesifu juhudi za wizara ya Katiba na Sheria kwa kuwaletea…

The post DC Longido aisifu wizara msaada wa kisheria bure appeared first on HabariLeo.

ARUSHA: MKUU wa Wilaya ya Longido, Salum Kalli amesifu juhudi za wizara ya Katiba na Sheria kwa kuwaletea wananchi huduma ya msaada wa kisheria bure na kusisitiza kuwa wananchi wa Arusha wanapaswa kuitumia ipasavyo kwa manufaa yao na jamii kwa ujumla.

Pia amewataka wakazi wa mkoa wa Arusha kuchangamkia fursa ya kipekee ya kupata msaada wa kisheria kupitia Mama Samia Legal Aid Campaign inayoendelea jijini Arusha.

Akizungumza Machi 2, 2025, alipotembelea mabanda ya huduma za kisheria katika viwanja vya TBA jijini Arusha, Kalli amesema kuwa kampeni hiyo itadumu kuanzia Machi 1 hadi Machi 8, 2025 na ni nafasi muhimu kwa kila mwananchi mwenye changamoto za kisheria kufika na kupata msaada bure.

“Hii ni fursa adhimu kwa kila mwenye changamoto za kisheria. Kuanzia masuala ya mirathi, migogoro ya ardhi, ndoa, na mengineyo. Napenda kuwaalika wananchi wote, hususan wanawake wanaokabiliwa na changamoto hizi, kufika na kupata msaada wa kisheria bila malipo,” amesema Kalli.

Aidha, ametoa mfano wa mama mjane ambaye amenyang’anywa mali alizochuma na mume wake baada ya kufariki. Kupitia kampeni hii, mama huyo na wengine wenye changamoto kama hizo wanaweza kupata haki zao kwa msaada wa wataalam wa sheria waliopo kwenye mabanda hayo.

“Hii ni kampeni muhimu inayohakikisha haki inapatikana kwa wote, hususan wale waliokosa sauti ya kutetea haki zao,” ameongeza.

Mama Samia Legal Aid Campaign inaendelea jijini Arusha hadi Machi 8, 2025, ikiwa na lengo la kuwasaidia wananchi kupata haki zao bila gharama yoyote.

The post DC Longido aisifu wizara msaada wa kisheria bure appeared first on HabariLeo.