Dar Leopards kupimana na Les Gaulois Jumamosi

Habari Leo
Published: May 29, 2025 09:36:21 EAT   |  Educational

DAR ES SALAAM– TIMU ya mchezo wa Rugby au Raga ya DAR Leopards inatarajia kuumana na Les Gaulois de Nairobi kutoka Kenya katika mchezo wa kirafiki wa kujenga mahusiano. Pambano hilo litafanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Jumamosi ya Mei 31, 2025. Akizungumza na Dailynews Digital, Katibu Mkuu wa Chama …

DAR ES SALAAM– TIMU ya mchezo wa Rugby au Raga ya DAR Leopards inatarajia kuumana na Les Gaulois de Nairobi kutoka Kenya katika mchezo wa kirafiki wa kujenga mahusiano.

Pambano hilo litafanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Jumamosi ya Mei 31, 2025.

Akizungumza na Dailynews Digital, Katibu Mkuu wa Chama cha Rugby Tanzania (TRU), Antony Edward, amesema mechi hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuinua viwango vya mchezo huo Afrika Mashariki.

“Tunatarajia tukio la aina yake. Hii si mechi ya kawaida ni vita ya vigogo wa Rugby wa ukanda huu. Tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kushuhudia kipute hiki cha kihistoria,” amesema Antony.

Mbali na mechi kuu ya wanaume, kutakuwa pia na onesho la kuvutia la wanawake kupitia timu ya Cheetahs Women’s 7s, watakaoingia uwanjani saa 9:00 alasiri, kabla ya pambano la wanaume kuanza saa 9:30.

Antony pia amethibitisha kwamba Tendai Mtawarira “The Beast” mchezaji wa zamani wa Afrika Kusini waliochukua ubingwa wa Dunia 2019, alipaswa kuhudhuria, hatoweza kufika kufuatia kufutwa kwa hafla hiyo aliyoalikwa awali.

Hata hivyo, ameongeza kuwa hamasa na nguvu za mchezo zitabaki kuwa juu mno.“Ni kweli, The Beast hatoweza kuungana nasi, lakini hiyo haipunguzi chochote kwenye ubora wa tukio. Tunahakikisha mashabiki wanapata burudani ya kiwango cha juu kabisa,” ameongeza.

Kwa mujibu wa Antony, tukio hili ni fursa ya kipekee kwa Rugby ya Afrika Mashariki kuonesha maendeleo na ushindani wa hali ya juu.