Chatu aleta sintofahamu wananchi waomba msaada

KATAVI: WAKAZI wa Mtaa wa Kasimba, Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, wanalalamikia kusimama kwa shughuli zao za kiuchumi kufuatia kuonekana kwa nyoka mkubwa aina ya chatu katika bonde linalotumika kwa kilimo na ufyatuaji wa tofali. Wakizungumza wakazi hao wamesema wameacha kwenda mashambani kwa hofu ya kushambuliwa, jambo ambalo linahatarisha mazao yao pamoja na maisha yao …
KATAVI: WAKAZI wa Mtaa wa Kasimba, Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, wanalalamikia kusimama kwa shughuli zao za kiuchumi kufuatia kuonekana kwa nyoka mkubwa aina ya chatu katika bonde linalotumika kwa kilimo na ufyatuaji wa tofali.
Wakizungumza wakazi hao wamesema wameacha kwenda mashambani kwa hofu ya kushambuliwa, jambo ambalo linahatarisha mazao yao pamoja na maisha yao ya kila siku.
“Kwa sasa hatuwezi kuendelea na kilimo wala kufyatua tofali, hii ni shughuli ambayo ndiyo tegemeo letu kuu la kipato,tukiacha hata kwa wiki moja, familia haziwezi kupata chakula,” amesema Amina Maziku mkazi wa eneo hilo.
Wakazi hao wamesema kuwa nyoka huyo amekuwa akiwinda na kula mifugo yao kama vile kuku, bata na mbuzi, hali inayowatia hofu kubwa kuhusu usalama wa familia na mali zao.
“Tuna hofu kubwa hata kwenda shambani, tunaweza kupoteza kila kitu tulichopanda, maana nilimuona nyoka mkubwa ana mabaka kama Chui,nimuona akiwa anatembea kuelekea upande wa pili, sikumuona kichwa kwa kuwa alikuwa akimalizikia” amesema Mwajuma Athuman.
Mtaa wa Kasimba ni miongoni mwa maeneo yanayochipukia kwa shughuli za kilimo cha mazao ya chakula na biashara, pamoja na ufyatuaji wa tofali unaochangia pato la kaya na ujenzi wa miundombinu ya jamii.
Mwenyekiti wa mtaa huo, Benard Nswima, amesema kuwa tayari ameshawasiliana na vyombo vya usalama na idara ya wanyamapori ili kusaidia kuliondoa tishio hilo.
Aidha, amewataka wananchi kufanya usafi wa mazingira ili kuondoa vichaka vinavyoweza kuwa makazi ya nyoka hao. “Huu ni wakati wa kushirikiana, tukifanya usafi, tunapunguza uwezekano wa nyoka kujificha na kushambulia,lakini tunahitaji msaada wa kitaalamu kutoka serikalini,” amesema Nswima.
Katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, chatu wawili waliuawa katika eneo hilo kwa ushirikiano wa serikali na wananchi, ishara kuwa changamoto hiyo ni ya muda mrefu na inahitaji suluhisho la kudumu.
Wananchi hao wameiomba serikali kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto hiyo, ikiwemo kuleta wataalamu wa wanyamapori, kuweka elimu ya tahadhari na kusaidia kutafuta njia mbadala za kiuchumi hadi hali itakapodhibitiwa.