CCM kujenga makao makuu mapya Dodoma

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinajenga jengo jipya la makao makuu mapya ya chama hicho. Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya (NEC) ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla alisema tukio la uwekaji wa jiwe la msingi la jengo hilo litafanyija Mei 28, mwaka huu. “Tunakwenda kujenga jengo la makao makuu pembeni mwa jengo …
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinajenga jengo jipya la makao makuu mapya ya chama hicho.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya (NEC) ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla alisema tukio la uwekaji wa jiwe la msingi la jengo hilo litafanyija Mei 28, mwaka huu.
“Tunakwenda kujenga jengo la makao makuu pembeni mwa jengo la mkutano (la Jakaya Kikwete). Chama chetu ni kikubwa na kinaendelea kukua siku hadi siku na kwa sasa kina wanachama milioni 11,” alisema Makalla.
Aliongeza: “Kwa hiyo ili tuwe na uwezo wa kuhudumia vizuri shughuli za chama chetu tumeona pale pamekuwa padogo sasa tuwe na makao makuu eneo kubwa lenye hadhi na huduma zote muhimu, ikiwemo kumbi za mikutano”.
Makalla alisema Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM huo utatanguliwa na vikao vya awali ambavyo ni kikao cha Kamati Kuu ya CCM kitakachofanyika kesho na kufuatia na Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kitakachofanyika Mei 28, mwaka huu.
Alisema mkutano huo utapokea taarifa ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.
Makalla alisema pia, mkutano huo utakuwa jukwaa la CCM kuzindua Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2025-2030.
“Ilani tunayokwenda kuizindua ni mkataba wa chama na wananchi kutelekeza, itakayotuongoza katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu na ndiyo kitendea kazi chetu…” alisema.
Makalla alisema CCM inajivunia mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2020 hadi 2025 na serikali ya chama hicho imefanya kazi kubwa kuitekeleza.
“Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi za maendeleo, wabunge, madiwani na Watanzania ni mashahidi kwani katika kila kijiji, mitaa kuna alama imewekwa ikiwa ni darasa, zahanati, umeme; huduma zote,” alisema.
Makalla alisema katika kuandaa ilani hiyo CCM imefanya tathmini ya utekelezaji wa ilani iliyopita na kufanya utafiti kwa kukusanya maoni ya asasi za kiraia na wananchi kwa kuona vipaumbele na mahitaji ya wananchi.
“Ni ilani ya Watanzania, tumekwenda kujibu kiu ya Watanzania, inaenda kukonga mioyo ya Watanzania, kwa lugha rahisi niseme yajayo yanafurahisha,” alisema.
Aliongeza: “Nawaalika wajumbe wote wa mkutano mkuu maalumu wa Chama Cha Mapinduzi, karibuni Dodoma, mambo yote yamekamilika na pia tunawaalika wageni, wanachama na Watanzania wote. Pia, tutaweka maeneo maalumu kwa ajili ya wananchi kufuatilia mkutano huu ambao utakuwa ni wa kipekee”.