CCM Iringa yaahidi kura za kipekee kwa Samia 2025

Habari Leo
Published: Jan 25, 2025 10:46:09 EAT   |  News

Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa kimeweka dhamira ya kuongoza kitaifa kwa idadi ya kura atakazopata mgombea…

The post CCM Iringa yaahidi kura za kipekee kwa Samia 2025 appeared first on HabariLeo.

Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa kimeweka dhamira ya kuongoza kitaifa kwa idadi ya kura atakazopata mgombea urais wa chama hicho, Dk Samia Suluhu Hassan, katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, 2025.

Ahadi hiyo imejengwa juu ya rekodi ya ushindi mkubwa wa CCM mkoani humo, ambapo chama hicho kilijipatia asilimia 99.99 ya ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa, Daud Yasin, alitoa tamko hilo wakati wa matembezi maalumu yaliyolenga kuunga mkono uamuzi wa Mkutano Mkuu wa CCM kumpitisha Dk Samia kuwa mgombea urais kwa mwaka huu.

Akihutubia umati mkubwa baada ya matembezi hayo, Yasin alieleza kuwa maendeleo makubwa yaliyoletwa na Dk Samia mkoani Iringa ni kigezo kinachowapa sababu ya kujivunia na kujitahidi kuleta ushindi mkubwa zaidi katika uchaguzi huo.

“Nataka niwaambie, Mkutano Mkuu wa CCM umezingatia kanuni na katiba kumpitisha Dk Samia, tofauti na madai ya upotoshaji kutoka kwa baadhi ya watu wasiojua mamlaka ya mkutano huo,” alisema Yasin.

Yasin alibainisha baadhi ya miradi inayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita, ikiwemo upanuzi wa uwanja wa Ndege wa Iringa, ujenzi wa barabara za kimkakati kama Iringa-Msembe na Mafinga-Mgololo.

Mingine ni miradi wa umwagiliaji na miundombinu ya umeme, huduma bora za afya, elimu, maji, na mikopo kwa vijana na wanawake.

Mwanasiasa na mchungaji maarufu mkoani Iringa, Peter Msigwa, aliutumia mkutano huo kufuta uvumi kuhusu kurejea kwake CHADEMA.

Alisisitiza kuwa maendeleo yaliyofanikishwa na CCM yanathibitisha kuwa ni chama pekee chenye uwezo wa kuliongoza taifa.

“Nikijaribu kufanya ulinganisho wa nilikotoka na nilipo, hakuna chama kingine kinachoweza kuongoza nchi zaidi ya CCM. Sina mpango wa kurudi nyuma,” alisema Msigwa.

Mbunge wa Iringa Mjini na Mwenyekiti wa Wabunge wa Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu, aliwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika matembezi hayo.

Pia aliwataka wananchi wote kujitokeza kwa wingi zaidi katika uchaguzi mkuu, akisema hilo litahakikisha ushindi wa kishindo kwa Dk Samia.

Matembezi hayo, yaliyoanzia Uwanja wa Michezo wa Samora hadi Ofisi za CCM Mkoa wa Iringa, yalivutia umati mkubwa wa wananchi wa Iringa na viunga vyake waliojitokeza kuunga mkono uamuzi wa chama hicho.

Mwisho.

The post CCM Iringa yaahidi kura za kipekee kwa Samia 2025 appeared first on HabariLeo.