Benki ya Akiba yawazawadia washindi Kampeni ya Twende Kidigitali
Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital Benki ya Akiba (ACB) imewashukuru wateja wake kwa kushiriki katika kampeni ya ‘Twende Kidigitali Tukuvushe Januari’ na kuwahimiza kuendelea kutumia huduma zake za kidijitali. Shukrani hizo zimetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Biashara, Dk. Danford Muyango, wakati wa kuwazawadia washindi wa kampeni hiyo ambapo wateja mbalimbali kutoka Dar es Salaam […]
Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Benki ya Akiba (ACB) imewashukuru wateja wake kwa kushiriki katika kampeni ya ‘Twende Kidigitali Tukuvushe Januari’ na kuwahimiza kuendelea kutumia huduma zake za kidijitali.
Shukrani hizo zimetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Biashara, Dk. Danford Muyango, wakati wa kuwazawadia washindi wa kampeni hiyo ambapo wateja mbalimbali kutoka Dar es Salaam na mikoa mingine walikabidhiwa zawadi pamoja na fedha zilizowekwa moja kwa moja kwenye akaunti zao.
“Kampeni ya ‘Twende Kidijitali, Tukuvushe Januari’ ilizinduliwa katikati ya Desemba 2024 kwa lengo la kuboresha mazingira ya kibenki kwa wateja wakati wa msimu wa sikukuu na kuwasaidia kushinda changamoto za kifedha mwezi huu kupitia zawadi mbalimbali hivyo, droo hii haitaishia hapa ni endelevu,” amesema Muyango.
Baadhi ya wateja wameishukuru benki hiyo kwa jitihada zake za kuimarisha huduma za kidijitali ambazo zimeboresha uzoefu wao wa kibenki kwa kuwapatia urahisi wa kupata huduma za kifedha wakiwa mahali popote na wakati wowote.
Mmoja wa wateja hao Alfayo Zephania, alieleza jinsi alivyopokea habari njema za kuibuka mshindi wa kampeni hiyo.
“Nilifurahishwa na taarifa ya ushindi na ninaishukuru Benki ya Akiba kwa kujali wateja wake na kutoa huduma bora, natoa rai kwa watu wengine kujiunga na benki hii ili wanufaike na mengi ikiwemo mikopo ambayo imenivusha pakubwa katika biashara zangu,” amesema.
Mteja mwingine Ezekiel Willium, amesema ushindi aliopata umempa hamasa zaidi ya kushiriki kwa bidii ili kupata zawadi kubwa katika droo kuu ya mwisho wa kampeni.
Benki hiyo imewashukuru wateja wake kwa kushiriki katika kampeni hiyo na kuwasihi waendelee kutumia huduma za kidijitali za benki.