ATCL mguu sawa kuiunganisha Afrika

Habari Leo
Published: May 23, 2025 06:41:27 EAT   |  Travel

MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Peter Ulanga amesema katika miaka mitano ijayo anaiona ATCL ikiwa sehemu ya ukuaji wa uchumi na mnyororo wa thamani katika sekta ya utalii. Pia, Ulanga amesema katika muda huo anaiona ATCL itakuwa na uwezo wa kuunganisha bara la Afrika na Ulaya. Amesema hayo alipozungumza katika kipindi cha …

MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Peter Ulanga amesema katika miaka mitano ijayo anaiona ATCL ikiwa sehemu ya ukuaji wa uchumi na mnyororo wa thamani katika sekta ya utalii.

Pia, Ulanga amesema katika muda huo anaiona ATCL itakuwa na uwezo wa kuunganisha bara la Afrika na Ulaya.

Amesema hayo alipozungumza katika kipindi cha Tunatekeleza kilichorushwa na kituo cha televisheni cha TBC1 cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Ulanga alisema katika miaka mitano ijayo anaiona ATCL itakuwa na uwezo wa kuunganisha bara la Afrika kupitia usafirishaji wa abiria na mizigo.

Alisema ATCL imekuwa sehemu ya mnyororo wa thamani kwa sekta ya utalii na kwamba litakuwa miongoni mwa taasisi zinazoingizia taifa fedha za kigeni.

“ATCL itakuwa sehemu ya ukuaji wa uchumi na tuna matumaini itachangia maendeleo kutokana na juhudi tunazozifanya usiku na mchana,’’ alisema Ulanga.

Alisema alipoteuliwa kuiongoza ATCL alipewa maagizo manne likiwemo la kuhakikisha safari za Watanzania zinakuwa salama, kunakuwa na usafiri wa uhakika, kwa gharama nafuu na kurudisha imani ya Watanzania kwa shirika lao.

Ulanga alisema mikakati aliyonayo katika kushughulia maeneo hayo ni pamoja na kupima ucheleweshaji wa safari za ndege zao kila siku na kwamba wanapobaini tatizo hushughulikia kwa lengo la kuimarisha huduma.

Alisema wanaendelea kuangalia namna ya kupunguza gharama za usafiri ili kila Mtanzania atumie usafiri wa anga.

“Kwa gharama zilizopo ni nafuu na ndio maana ndege zetu zinajaa lakini tutaendelea kupunguza gharama za uendeshaji kupunguza nauli,’’ alisema Ulanga.

Alisema gharama za uendeshaji huchangiwa na mafuta kati ya asilimia 30 hadi 40 ya uendeshaji ghafi, matengenezo na mishahara.

Ulanga alisema ATCL inaendelea kutanua mabawa yake kwa kwenda nchi mbalimbali za Afrika na nje ya bara hilo.

Alisema baada ya kuzindua safari za Afrika Kusini na Congo, Juni mwaka huu wanatarajia kwenda Lagos nchini Nigeria na wameomba kibali cha kutua Accra Ghana, Abidjan Cote d’Ivoire na Senegal.

Pia, Ulanga alisema wameomba kibali cha kurusha ndege za ATCL kwenye anga la Ulaya ili kufika Uingereza, Amerika Kusini, Ulaya na Urusi.

“Msumbiji wameomba tuanzishe safari kwenda Maputo, Beira, Nampula na Pemba lakini hata hapa nchini bado tuna uhitaji wa kutua katika Kisiwa cha Pemba, Mafia na Serengeti wakati wa msimu wa utalii ambao itawapa wateja fursa ya kutalii,’’ alisema.

Ulanga alisema ATCL inahitaji ndege ndogo ya mizigo itakayotua katika kila kiwanja cha ndege na kubeba mizigo ambayo itachukuliwa na ndege kubwa inayosafirisha kwenda nje ya nchi.

Alisema ndege ya mizigo waliyonayo inaweza kutua katika viwanja vitano nchini, hivyo ndege hiyo ndogo
itasaidia Tanzania kuwa kituo cha usafirishaji wa mizigo na kuipeleka maeneo mbalimbali.