Asilimia 91 ya Saccoss Geita hali mbaya

Habari Leo
Published: Mar 03, 2025 09:06:41 EAT   |  News

MKOA wa Geita umebainisha kuwa jumla ya Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOS) 195 sawa na…

The post Asilimia 91 ya Saccoss Geita hali mbaya appeared first on HabariLeo.

MKOA wa Geita umebainisha kuwa jumla ya Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOS) 195 sawa na asilimia 91 ya Saccos zote 212 zilizosajiliwa zina hali mbaya (hali sinzia) na zimeshindwa kujiendesha kwa tija.

Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji mkoani humo, Alfred Msenya ametoa taarifa hiyo wakati akifunga mafunzo kwa wanachama, viongozi na watendaji wa Saccos Mkoa wa Geita.

Msenya amesema taarifa ya ukaguzi inaonyesha ni Saccos 17 pekee zilizo hai ambapo kati ya yake Saccos 10 zipo daraja A, Saccos moja ipo daraja B na Saccos zisizo na daraja lolote ni sita.

Amesema uchunguzi unaonyesha Saccos nyingi zimekuwa zikijiendesha kwa mazoea pasipo kuwa na wataalamu wa uchumi na fedha kiasi cha kushindwa kuratibu na kuhasibu kwa ufasaha shughuli zao.

Amesema serikali imejizatiti kuboresha sekta ya fedha ikiwemo Saccos hivo ni lazima viongozi, watendaji na wanachama wa Saccos kufuata miongozo waliyojiwekea na kupunguza migogoro katika vyama.

Aidha amewataka viongozi wa Saccos wajifunze kuelewa dhana ya ushirika katika mifumo ya uzalishaji na huduma za kifedha zenye tija na manufaa kwa wanachama na wananchi wote ili kujiimarisha kiuchumi.

Ofisa Ushirika Mkuu mkoani Geita, Martine Kimisha amesema katika kurejesha uhai wa Saccos waliandaa mafunzo ya siku tano kwa viongozi, watendaji na wanachama wa Saccos ili kuimarisha misingi ya ushirika.

“Walioitikia kwenye mafunzo haya zilikuwa Saccos 13, kati ya Saccos 17 za mkoa wa Geita zinazofanya vizuri, na mkoa wa Geita tuna jumla ya Saccos 212, kwa hiyo utaona Saccos nyingi bado zimesinzia.

“Lengo la mafunzo haya ni kuimarisha na kuamusha Saccos za mkoa wa Geita, lakini pia kuhakikisha hizi Saccos zinafuata matakwa ya sheria ya huduma za kifedha ya mwaka 2018 na kanuni zake za mwaka 2019”, amesema.

Kaimu Ofisa Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Geita, Kivuruge Athuman amekiri kiini cha anguko la Saccos nyingi ni kukosa vitabu sahihi vya taarifa za kifedha, migogoro baina ya wanachama na viongozi kutokuwa waadirifu.

Mwanachama wa Songambele-Katoro Saccos, Simon Mallando amesema wao ni moja ya Saccos ya mfano wakiwa na miaka 24 tangu kuanzishwa na ambapo aliviomba vyama vingine kutanguliza mshikamano ili kufikia malengo.

The post Asilimia 91 ya Saccoss Geita hali mbaya appeared first on HabariLeo.