Argwing-Kodhek alikuwa wakili shupavu wa MauMau

C. M. G Argwing-Kodhek alikuwa wakili wa haki za binadamu na mbunge wa kwanza wa Gem aliyehudumu kuanzia 1963 hadi 1969.
Ufupisho CMG uliotangulia jina lake ulimaanisha; Chiedo Moa Gem (yaani aliyekaangwa kutoka Gem).
Alipewa jina hilo na wazazi wake kama kumbukumbu ya mababu zao. Alitumia jina hilo katika ulingo wa siasa kuvutia ufuasi.Mbali na hayo, marehemu Argwings-Kodhek ni miongoni mwa mawakili wa kwanza wa asili ya Kenya ambaye alisomea uanasheria nchini Uingereza.
Alikuwa katika tapo alilokuwa Mwanasheria Mkuu Charles Njonjo na aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge na Mbunge wa Tinderet (kati ya 1963 na 1975) Jean Marie Seroney.
Alifanya kazi ya uwakili jijini Nairobi mapema miaka ya sitini, akiegemea nyanja ya haki za kibinadamu.Hii ndio maana utawala wa ukoloni ulimchukulia kama’ kichwa moto’ kutokana na uanaharakati wake huku akiwatetea wapiganiaji wa kundi la Mau Mau kama vile Waruru Kanja, miongoni mwa mibabe wengine.
Ni alipokuwa akiendesha kazi yake ya uwakili na uanaharakati, jijini Nairobi ambapo alijiunga na siasa na hatimaye akabuni chama cha kisiasa cha Nairobi Congress Party.
Chama hicho kilishindana na kile cha Nairobi People’s Convention Party, kilichoasisiwa na marehemu Tom Mboya.Kenya ilipopata uhuru mnamo 1963, Waziri Mkuu Jomo Kenyatta alimteua Argwings-Kodhek kuwa Waziri Msaidizi wa Ulinzi.
Na mnamo 1966, alipandishwa cheo kuwa Waziri wa Mali Asili na hatimaye mnamo 1967 aliteuliwa kuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni.Argwing- Kodhek alizaliwa mnamo 1923 katika kata ya Malanga, eneobunge la Gem, wilaya ya Siaya, (sasa kaunti ya Siaya).
Alisomea katika shule ya upili ya St Mary’s Yala na kisha akajiunga na Chuo cha King’s College Budo, Uganda. Alitoka ukoo wa Kagola Ojuodhi ambao pia ndio anatoka aliyekuwa mbunge wa Gem Isaac Omolo Okero (kuanzia 1969 hadi 1979).
Huo pia ndio ukoo wa msomi mashuhuri Profesa Bethwel Allan Ogot, mumewe Grace Ogot ambaye alihudumu kama mbunge wa Gem kati ya 1985 hadi 1992.
Baada ya kuhitimu kutoka chuo cha Budo, Argwing-Kodhek alifunza katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Kapsabet, ambako alikutana na Rais mstaafu Daniel Moi.
Ni baada ya hapo ambapo alipata udhamini kuenda kwa masomo ya juu nchini Uingereza, ambako alitakiwa kusomea taaluma ya ualimu. Hata hivyo, alivutiwa na kozi ya uanasheria ambayo serikali ya ukoloni haikutaka asomee.
Kwa hivyo, baada ya mwaka mmoja, udhamini wa masomo aliopewa ulikatizwa.Hii ilimlazimu babake kuuza mifugo wake ili kugharimia karo yake aweze kusomea shahada ya kwanza katika uanasheria.
Baada ya kuhitimu kama wakili alianza kuhudumu kama wakili katika kituo cha Lincoln Inn ambapo alikuwa akipokea mashahara mzuri.Lakini siku moja aliwashangaza wenzake, alipowajulisha kwamba angetaka kurejea nyumbani, Kenya.
Baada ya kurejea nyumbani Argwings- Kodhek aliajiriwa na serikali ya mkoloni kama mshauri wa masuala ya sheria katika afisi ya Msajili Mkuu ambako alifanya kazi pamoja na Njonjo, Seroney na Mareka Gecaga.
Baada ya mwaka mmoja, CMG alijiuzulu kazi hiyo na akaamua kuhudumu kama wakili wa kundi la Mau Mau, kazi aliyofanya kwa malipo duni au nyakati nyingine bila malipo.
Wakati wa mapambano ya uhuru, Bw Argwing-Kodhek pamoja na Achieng Oneko na Paul Ngei ndio walikuwa watu wasio wa kabila la Agikuyu ambao walishirikiana moja kwa moja na kundi la Mau Mau.
Hii ndiyo maana Rais Kenyatta aliwateua watatu hao katika baraza lake la kwanza la mawaziri mnamo 1963.Mnamo 1966, Jaramogi Oginga Odinga alipogura Kanu na kuunda chama cha Kenya People’s Union (KPU), tofauti na wanasiasa wengine kutoka Luo Nyanza, Kodhek aliamua kusalia katika chama hicho tawala.
Hii ndiyo maana Rais Kenyatta alimdumisha katika baraza lake la mawaziri ambapo kati ya 1967 na 1969 alihudumu kama Waziri wa Masuala ya Kigeni. Alifariki mnano 1969 gari lake lilipohusika katika ajali ya barabarani katika eneo la Kilimani, Nairobi.