4R zaimarisha Muungano

DAR ES SALAAM; SERIKALI imesema falsafa ya 4R ya Rais Samia Suluhu Hassan ya Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na…
The post 4R zaimarisha Muungano appeared first on HabariLeo.
DAR ES SALAAM; SERIKALI imesema falsafa ya 4R ya Rais Samia Suluhu Hassan ya Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga upya, ni daraja la kuimarisha Muungano.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni alisema hayo akifungua Kongamano la Miaka 61 ya Muungano lililofanyika Dar es Salaam jana.
Masauni alisema falsafa hiyo inajenga na kuimarisha dhamira ya kuundwa kwa Muungano ambayo ni kujenga umoja wa kitaifa, ushirikiano wa kijamii, upendo na undugu miongoni mwa wananchi bila kujali tofauti za kiitikadi.
Alisema kupitia falsafa hiyo, mambo mengi yamefanyika yakiwamo mapitio ya mfumo wa haki jinai, uhuru wa kujieleza umeimarika, vyama vya siasa kufanya shughuli zao kwa uhuru, kufanyika kwa mazungumzo ya kuleta umoja wa kitaifa, ushirikishwaji, mabadiliko kwenye Sheria ya Uchaguzi, Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Alionya dhidi ya watu wanaochokonoa Muungano na kuwakumbusha kuwa wasiuchukulie poa.
Masauni alisema serikali haitacheka na yeyote mwenye nia ovu na Muungano na kukumbusha kuwa ‘asiyesikia la mkuu huvunjika guu’.
Alisema serikali imejidhatiti kuulinda Muungano kwa gharama yeyote na kwamba itaendelea kukemea na kusimamia Muungano ili vizazi vijavyo warithi Muungano mzuri zaidi na wenye maslahi mapana kwa pande zote.
Aidha, alisema kutokana na uthubutu na ujasiri wa kukubali na kuruhusu kufanyika mageuzi nchini, Rais Samia anastahili kupewa jina lingine hasa la ‘Mama Mageuzi’ kwa sababu amekuwa chachu ya mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini.
Alisema katika kipindi cha miaka minne ya Rais Samia madarakani, amepunguza kwa kasi hoja za Muungano kutoka hoja 18 alizozikuta kati ya hoja kuu 25 hadi kubaki hoja tatu tu akimaanisha ametoa majibu ya hoja 15.
“Hizo hoja tatu zilizobaki zipo katika hatua mbalimbali za utatuzi… na nina hakika kunako majaliwa ya Mwenyezi Mungu katika kipindi chake cha miaka mitano iliyobakia hizi hoja tatu atazipatia majibu kutokana na hatua zilipofikia,” alieleza Masauni.
Alisema Muungano ni wakfu ambao Watanzania waliachiwa na waasisi wa taifa hivyo hawana budi kuuenzi na kuulinda kwa wivu mkubwa huku wakielimisha umma kuhusu Muungano ambao Watanzania wengi wa leo wamezaliwa ndani ya Muungano.
Alisema Muungano umeifanya Tanzania kuwa salama katika eneo la ulinzi na usalama na kufanya kusiwe na tabiriko lolote la kuvunjika kwa amani na utulivu wa nchi.
“Muungano umeleta matunda mengi yakiwemo kumaliza ukabila, ubaguzi wa rangi, udini na ukanda ambao unasababisha katika nchi zingine kuvunja amani ya nchi yao,” alisema Masauni.
Aliwataka viongozi kuhakikisha wanapata ufahamu wa kutosha kuhusu Muungano na hilo limeoneshwa katika taarifa ya Sensa ya Watu na Makazi ambayo imebainisha kuwa baadhi ya viongozi hawana ufahamu wa kutosha.
Alisema kutokana na jamii kubwa hasa vijana kuwa na uelewa hafifu wa Muungano, serikali imeandaa makakati wa kuimarisha utoaji wa elimu ya Muungano ambao hautasubiri matukio ya Muungano na badala yake kila maadhimisho ya Muungano yanapoisha utoaji wa elimu utaendelea kwa rika tofauti.
Aisha, alisema serikali itaendelea kuienzi misingi iliyowekwa na waasisi kwa sababu imeonesha kuwa ndio nguzo ya kuimarika kwa Muungano.
Alisema msingi wa kuundwa kwa Muungano haukuwa kwa sababu ya vitu, kwamba nani kapata na nani kakosa, bali ilikuwa ni kwa sababu za undugu wa dhati wa damu uliopo baina yao, ushirikiano wa wananchi katika mapambano ya ukombozi, jiografia ya nchi na usalama.
Alisema tangu kuasisiwa Muungano, umeendelea kuwa na mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kijamii hivyo ni Muungano unaoishi na kutimiza matakwa na malengo ya wananchi wake.
The post 4R zaimarisha Muungano appeared first on HabariLeo.