TFS yatoa fursa ya ajira kwa watu 400 Ileje

Mtanzania
Published: Feb 11, 2023 18:12:00 EAT   |  Jobs and Career

Na Denis Sinkonde, Songwe Wakala wa Uhifadhi wa Misitu Tanzania(TFS) Wilaya ya Ileje mkoani Songwe imefanikiwa kutoa ajira kwa watu 400 kwenye shamba linalomilikiwa na Serikali chini ya Wakala huyo linalofahamika kama Iyondo Mswima pamoja na kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa wananchi 600 wanaouzunguka shamba hilo. Hayo yamebainishwa Februari 10, 2023 na Kaimu […]

Na Denis Sinkonde, Songwe

Wakala wa Uhifadhi wa Misitu Tanzania(TFS) Wilaya ya Ileje mkoani Songwe imefanikiwa kutoa ajira kwa watu 400 kwenye shamba linalomilikiwa na Serikali chini ya Wakala huyo linalofahamika kama Iyondo Mswima pamoja na kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa wananchi 600 wanaouzunguka shamba hilo.

Hayo yamebainishwa Februari 10, 2023 na Kaimu Mhifadhi wa shamba hilo, Jovan Emmanuel kwenye ofisi za TFS zilizopo Katengele wakati wa ugawaji wa miche ya miti kwa wananchi wanaozunguka shamba hilo zoezi lililofanywa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Farida Mgomi.

Jovan amesema TFS imekuwa na utaratibu wa kugawa miche ya miti kwa wananchi wa vijiji vinavyolizunguka shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 5,418 ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi hao umuhimu wa uhifadhi mazingira.

Amesema ili kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa mazingira kwenye msitu wa shamba la Iyondo Mswima tayari wananchi takribani 600 wamepewa elimu ya utunzaji wa mazingira kutoka vijijiji vinavyolizunguka shamba hilo.

“Kwa mwaka wa fedha 2022/23 ofisi ya shamba la miti Iyondo Mswima linatarajia kugawa miche ya miti 30,000 ikiwa ni kutimiza lengo la kushirikiana na jamii inayowazunguka kutunza mazingira,” amesema Jovan.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Farida Mgomi akizungumza wakati wa kugawa miche kwa wananchi hao amesewataka wananchi kujiepusha na uharibifu wa mazingira ikiwepo kufanya shughuli za kibinadamu kama kulima, kuchungia mifugo kuchoma mkaa na kuchoma misitu hovyo kwani shughuli hizo zinaharibu uoto wa asili uliopo.

Mgomi amesema kila mwananchi wa Ileje anaowajibu wa kulinda mazingira kwa kushirikiana na wakala wa uhifadhi wa misitu TFS lengo likiwa ni kuendeleza takwa la kisheria la kila kaya kupanda miti ikiwepo ya kivuli majumbani, matunda na ya zao la mbao kwa ajili ya kujiingizia kipato.

“Kila mwananchi na taasisi zitakazonufaika kupata miche hiyo izingatie upandaji kitaalamu ili isiharibike kwani tusipozingatia hayo tutaharibu miche hiyo na kupoteza lengo la TFS,”amesema Mgomi.

Aidha, amewataka wananchi wote waliopata fursa ya ajira na elimu ya kuhifadhi mazingira watumie nafasi hiyo kuhakikisha msitu wa Iyondo Mswima unakuwa wa mfano kwa Tanzania.

Akizungumza kwaniaba ya wananchi waliopokea miche hiyo Diwani wa kata ya Kalembo, Reward Songa amewahakikishia TFS kuwa wataendelea kushirikiana kutunza miti ya asili na ya kupandwa ndani ya shamba hilo ili mazingira ya Ileje iwe kivutio kwa watalii.

Shamba la miti Iyondo Mswima lina ukubwa wa hekta 5,418 na  ni miongoni mwa mashamba yanayomilikiwa na Serikali chini ya TFS ambapo kwa mwaka 2022/23 takribani miche 200,000 iliandaliwa ambapo mingine inaendelea kupandwa na mingine itagawiwa kwa wananchi.