Ndolela” Ufinyu wa maslahi, chanzo cha bendi nyingi kuvunjika”

Mtanzania
Published: Mar 24, 2023 10:24:53 EAT   |  Entertainment

Na Oliver Oswald, Mtanzania Digital Mwimbaji mashuhuri nchini, Malima Kabondo maarufu kama ‘ndolela’, ameweka bayana kuwa maslahi madogo wanayolipwa wasanii ni moja ya sababu kubwa inayochangia Bendi nyingi nchini kusambaratika kabla hazijafikia malengo. Malima aliyasema hayo jijini Dodoma Jana, wakati akielezea sababu za bendi nyingi za muziki nchini kuvunjika na kutodumu kwa muda mrefu. Alisema […]

Na Oliver Oswald, Mtanzania Digital

Mwimbaji mashuhuri nchini, Malima Kabondo maarufu kama ‘ndolela’, ameweka bayana kuwa maslahi madogo wanayolipwa wasanii ni moja ya sababu kubwa inayochangia Bendi nyingi nchini kusambaratika kabla hazijafikia malengo.

Malima aliyasema hayo jijini Dodoma Jana, wakati akielezea sababu za bendi nyingi za muziki nchini kuvunjika na kutodumu kwa muda mrefu.

Muimbaji wa nyimbo za asili nchini , Malima Kabondo ‘Ndolela’ ambaye pia ni Stafu Sajenti wa Jeshi la Polisi , Makao Makuu ya Polisi Dodom , akiwa katika sare zake za kazi.

Alisema kwa kipindi kirefu kumekuwa na mlolongo mrefu wa uanzilishi wa Bendi lakini baada ya muda baadhi ya Bendi hizo husambaratika kimya kimya na kupotea moja kwa moja.

“Kumekuwa na Bendi nyingi zikianzishwa na kupotea ghafla bila taarifa, lakini ukifuatilia kwa undani utagundua sababu kubwa inayosababisha kufa kwa bendi nyingi ni ufinyu wa maslahi kwa wasanii.

“Wasanii wengi wanaotokea kwenye Bendi hulalamikia suala la malipo kuwa hafifu na muda mwingine kucheleweshewa malipo yao na viongozi wao.

Alisema, wasanii wengi wamekuwa wakilipwa mishahara midogo ikilinganishwa na kazi kubwa wanayo ifanya ya kutoa burudani kwenye shughuli mbalimbali.

“Awal, mimi nilikuwa namiliki Maringo Bendi, iliyokuwa na wasanii wengi, ila baada ya muda bendi ikasambaratika baada ya kiongozi wa wasanii hao ambao walikuwa wazaire kutoka nchini Congo , kutofautiana na wenzie kutokana na madai ya kuwa maslahi ni madogo.

“Baada ya bendi kufa ikabidi nitafute wasanii wangu wachache, ambao ndo wanaunda ‘ Maringo Group’ kwa ajili ya kuwatumia kwenye kazi zangu za sanaa pindi ninapopata mialiko mbalimbali ya kwenda kutumbuiza.

Sambamba na hilo, pia alisema kazi ya kuongoza bendi ni ngumu zaidi ukilinganisha na kuongoza kikundi cha wasanii.

“Kiuhalisia umiliki wa bendi ni mgumu zaidi kuliko umiliki wa kikundi ambacho mara nyingi kazi zake hufanyika kwa makubaliano ya muda mfupi ukilinganisha na bendi ambayo hufanyika kwa mikataba ya muda kulingana na makubaliano ya mmiliki na wasanii wake.

“Kwahiyo hata gharama zinazotumika kwenye maandalizi ya bendi ni kubwa zaidi ya kundi ambalo mara nyingi kazi zao huwa za muda mfupi na siyo mara kwa mara, kwani bendi hadi ikamilike Jukwaani vitu vingi vya kupiga muziki vinahitajika viwepo kama maiki, ngoma ‘drums’ na vingine vingi.

Muimbaji wa nyimbo za asili nchini, Malima Kabondo ‘Ndolela’ wa Kwanza Kulia , akiwa pamoja na wasanii wake wa Maringo Grou , wakifurahi kwa pamoja.

“Lakini pia malipo ya wasanii wa bendi wengi wao hulipwa mwisho wa mwezi, tofauti na kikundi ambao mara nyingi malipo hufanyika baada ya kazi kukamilika.

“Mfano, mimi wasanii wangu mbali ya kuwalipa, lakini pia huwa nina wagharamia nauli za kwenda na kurudi , maradhi na chakula hadi shughuli itakapo kamilika,” alisema Malima.

Alisema, wamiliki wa bendi za muziki nchini, wanapaswa kuboresha maslahi ya wasanii wao ili kuzinusuru bendi zao zisisambaratike.