Yanga yapewa mwamuzi mwenye njano 43

YANGA ina dakika 90 za kuchukua au kuutema ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika wakati itakapokuwa na shughuli pevu katika mchezo wa marudiano wa fainali dhidi ya USM Alger utakaopigwa Jumamosi hii nchini Algeria. Katika mchezo huo utakaopigwa Stade du 5 Juillet, Yanga inahitaji ushindi kuanzia mabao 2-0 ili kuchukua taji hilo baada ya mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Dar es Salaam kukubali kichapo cha cha mabao 2-1. Wakati mchezo huo ukisubiriwa kwa hamu, tayari Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limemteua mwamuzi, Dahane Beida kutoka nchini Mauritania kusimama kati pambano hilo la kusisimua huku akiwa na rekodi mbalimbali. Rekodi zinaonyesha mwamuzi huyo amechezesha michezo 11 ya kimataifa na kati ya hiyo, timu za nyumbani zimeshinda sita, sare tatu na za ugenini zikishinda mbili huku akitoa kadi za njano 43 na nyekundu moja. Timu zilizoshinda ugenini ni MC Alger ya Algeria iliyoifunga Teungueth ya Senegal bao 1-0 kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na San Pedro iliyoshinda pia 1-0 na Jaraaf ya Senegal katika Kombe la Shirikisho Afrika. Licha ya Yanga kukutana na USM Alger kwenye fainali ila zina kumbukumbu ya kukutana kwenye hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika na mchezo wa kwanza uliopigwa nchini Algeria Mei 6 mwaka 2018, Yanga ilikubali kichapo ugenini cha mabao 4-0. Mchezo wa marudiano uliopigwa jijini Dar es Salaam Agosti 19, mwaka huo Yanga ililipa kisasi na kushinda kwa mabao 2-1, yaliyofungwa na nyota wake wa zamani, Deus Kaseke na Heritier Makambo. Msimu huo Alger ilimaliza ikiwa kinara wa kundi 'D' baada ya michezo sita na pointi 11 nyuma ya Rayon Sports kutoka Rwanda ambayo ilimaliza ya pili baada ya kujikusanyia jumla ya pointi tisa. Gor Mahia ya Kenya ilimaliza ya tatu na pointi nane huku Yanga ikiburuza mkia baada ya kukusanya pointi nne.