Yanga itaweka rekodi mpya Caf

Mwanaspoti
Published: Jun 02, 2023 09:59:26 EAT   |  Sports

HAKUNA maswali kuwa Yanga wana kazi moja tu ya kufanya ili kuweka historia nyingine ya soka hapa nchini. Tayari vitabu vinasema kuwa Yanga ndiyo timu pekee ya Tanzania kufika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na kupoteza mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Mkapa. Yanga Jumapili iliyopita ililala kwa mabao 2-1 dhidi ya USM Algier ya Algeria kwenye mchezo ulioweka rekodi ya mashabiki hapa nchini, sasa wanakwenda kujiuliza kwenye mchezo wa pili Jumamosi ijayo katika Uwanja wa Stande du 5 Julliet. Hii ni mechi ambayo Yanga itakwenda kucheza kufa na kupona kuhakikisha kuwa wanapokelewa na umati mkubwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere watakaporejea na kombe hilo kwa mara ya kwanza. Tayari kocha wa timu hiyo, Nasreddine Nabi ameshasema hakuna kinachoshindikana kwa kuwa amewaambia wachezaji wake wanachotakiwa ni kucheza kufa na kupona kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwa kuwa walishafanya huko nyuma. “Hakuna shaka kuwa tunamlima wa kupanda, lakini naamini kuwa uwezo wa kuibuka na ushindi ugenini upo, nimeshaongea na wachezaji wangu na wameniahidi kufanya makubwa kwenye mchezo huu naamini tunaweza kwa kuwa tuna wachezaji imara,” alisema Nabi. Yanga walishapata ushindi ugenini msimu huu dhidi ya TP Mazembe, Rivers United na Club Africain ya Tunisia hivyo ni rahisi kuamini kuwa wanaweza pia kuibuka na ushindi kwenye mchezo huu. Rekodi zinaonyesha kuwa ni nchi saba tu zimefanikiwa kuchukua ubingwa wa Kombe la Shirikisho tangu mwaka 2004, wakati mashindano hayo yalipoanzishwa, lakini timu zote zinakwenda kwenye fainali hii kutafuta kombe la kwanza la Afrika, Yanga hawajawahi kuchukua ubingwa sawa na USM. Nchi kinara wa kutwaa ubingwa huu ni Morocco, ambao wametwaa mara saba, lakini wanafuatwa na Tunisia ambao wametwaa mara tatu, katika nchi hizo, Algeria ambapo wanatoka USM Algier hawapo, sawa na ilivyo Tanzania kuonyesha kuwa lolote linaweza kutokea. Katika viwango vya ubora Afrika, Algier na Yanga wapo karibu, kila mmoja akimuonyesha mwenzake kuwa huniwezi, Waarabu hao wanashika nafasi ya 17, huku Yanga ikiwa nyuma yao kwa nafasi moja katika nafasi ya 18 kwa tofauti ya pointi chache. Rekodi zinaonyesha Yanga imekuwa timu ya pili kupoteza mchezo wa kwanza ikiwa nyumbani kuanzia mwaka 2004, baada ya awali Al-Merrikh ya Sudan kukubali kichapo cha mabao 2–4 dhidi CS Sfaxien ya Tunisia mwaka 2007 na ugenini wakalala 1-0. Timu saba tu ndiyo zimeweza kuwazuia wenyeji kupata ushindi nyumbani wakati wa mfumo wa nyumbani na ugenini kwa kuwalazimisha sare, huku nane zikiwa zimepata ushindi nyumbani. Kwenye mechi za pili wenyeji wameendelea kushikilia rekodi baada ya timu moja tu kukubali kichapo nyumbani kwao, ukiwa ni mchezo kati ya Sfaxen ambao walilala kwa mabao 3-2 dhidi ya Rabat. Hawa wanawaonyesha Yanga kuwa jambo hilo linawezekana kwenye mchezo huu wa Jumamosi ijayo. Katika mchezo wa mechi moja ya fainali ambao ulianza msimu wa 2019/2020 na kumalizika msimu uliopita, timu zote ambazo zilitajwa kama timu za nyumbani zilipata ushindi na kutwaa ubingwa. Msimu wa 2019–20, fainali zilifanikiwa Morocco ambapo ilikuwa mechi kati ya Berkane ambayo ilitajwa kama timu ya nyumbani dhidi ya Pyramids ya Misri, ambapo Berkane walishinda 1-0, msimu uliofuata Raja walitajwa wapo nyumbani wakivaana na JS Kabylie ya Algeria, mechi ilipigwa Benin, Raja wakashinda mabao 2-1. Msimu uliopita, RS Berkane ambao walitajwa kama wenyeji waliingia fainali na Orlando Pirates, fainali ilifanyika Nigeria, Pirates wakalala kwa penalti 5-4, baada ya sare ya bao 1-1. Hivyo dua za Watanzania wote zinawatakia kila la kheri Yanga kwenye mchezo huo wa keshokutwa saa 4:00 usiku. Mabingwa waliopita wa Kombe la Shirikisho Afrika: 2004 Hearts of Oak (Ghana) 2005 FAR Rabat (Morocco) 2006 Etoile du Sahel (Tunisia) 2007 CS Sfaxien (Tunisia) 2008 CS Sfaxien (Tunisia) 2009 Stade Malien (Mali) 2010 FUS Rabat (Morocco) 2011 MAS Fez (Morocco) 2012 AC Leopards (Congo) 2013 CS Sfaxien (Tunisia) 2014 Al Ahly (Misri) 2015 Etoile du Sahel (Tunisia) 2016 TP Mazembe (DR Congo) 2017 TP Mazembe (DR Congo) 2018 Raja (Morocco) 2018-19 Zamalek (Egypt) 2019-20 RS Berkane (Morocco) 2020-21 Raja CA (Morocco) 2021-22 RS Berkane (Morocco) 2022-23 ? Timu zilizochukua kombe mara nyingi CS Sfaxien 3: 2007, 2008, 2013, 2010 Étoile Sahel: 2 2006, 2015 2008 RS Berkane 2 2020, 2022 2019 TP Mazembe 2 2016, 2017 2013 Raja 2 2018, 2021 Nchi zinazoongoza kuchukua kombe la Shirikisho Morocco 7 Tunisia 5 DR Congo 2 Misri 2 Ghana 1 Mali 1 Congo 1