Yanga ilinasa kwenye mtego wa Waarabu

Mwanaspoti
Published: May 31, 2023 13:41:49 EAT   |  Sports

KABLA ya mchezo wa kwanza wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika juzi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Yanga, USM Alger haikuwa na takwimu za kuvutia katika umiliki wa mpira na kucheza soka la pasi. Lakini pia USM Alger ilikuwa na takwimu bora za ulinzi licha ya kwamba ilikuwa imeruhusu idadi kubwa ya mabao kuliko Yanga kwenye mashindano hayo hasa katika uporaji wa mipira, uzuiaji mashuti na kuziba mianya kwa wapinzani. Inawezekana Yanga walizifahamu takwimu hizo hawakuamua kuzipa uzito mkubwa au hawakuzifahamu hivyo hawakuweza kujiandaa vya kutosha na mechi hiyo kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mchezo wa juzi. Matokeo na namna ambavyo timu hizo zilicheza juzi, yalidhihirisha wazi kuwa Yanga haikuwa na maandalizi bora kimbinu kukabiliana na USM Alger kulingana na takwimu na mwenendo wa timu hizo katika mechi za nyuma za mashindano hayo tofauti na wapinzani wao ambao walioonekana kucheza wakiifahamu vyema Yanga. UPANGAJI WA KIKOSI, MBINU ULIIGHARIMU YANGA Ni mchezo ambao uliihitaji wachezaji wabunifu zaidi katika eneo la kushambulia kwa lengo la kuvuruga muundo wa ulinzi wa USM Alger ambayo ilikuwa lazima imekuwa ikijaza kundi kubwa la wachezaji pindi inaposhambuliwa lakini ikawa tofauti. Kocha Nasreddine Nabi na benchi lake la ufundi waliwaanzisha Kennedy Musonda na Tuisila Kisinda kucheza kama washambuliaji wa pembeni katika kile kinachoonekana ni kutegemea zaidi kasi yao pindi wanaposhambulia, mpango ambao ulionekana kutozaa matunda kutokana na wawili hao kuonekana kukosa mbinu mbadala ya kuupenya ukuta wa USM Alger badala ya ile ya kukimbilia pembeni na kupiga krosi tu. Lakini pia viungo wake hasa Mudathir Yahya na Stephane Aziz Ki walichelewa kupiga pasi kwa haraka ambazo zingewafanya wawili hao kutumia kasi yao kwenda kushambulia, jambo lililowapa nafasi wapinzani wao kujipanga kwa haraka na kuziba mianya ambayo Yanga wangeitumia kufunga mabao. Hata uhai wa Yanga ulionekana katika kipindi cha pili baada ya kuingia Salum Abubakar 'Sure Boy' na Bernard Morrison ambao huwa hawakai sana na mpira mguuni lakini pia wamekuwa ni wabunifu wa kupiga pasi zinazovunja mistari ya ulinzi ya wapinzani ingawa uamuzi wa kuwaingiza ulifanyika kwa kuchelewa. MAYELE HANA LAWAMA Katika siku ambayo kundi kubwa la wachezaji wa Yanga walionekana kutochangamka, Fiston Mayele aliendelea kujitofautisha na wengine kutokana na kiwango bora alichoonyesha licha ya timu yake kupoteza. Alirudi nyuma kusaidia ulinzi pindi walipokuwa wakishambuliwa na wakati wanashambulia, alikimbia katikia maeneo tofauti ya uwanja ili kuwatanua mabeki wa USM Alger ambao walionekana kujiandaa vilivyo kumdhibiti lakini kwa bahati mbaya wenzake walishindwa kutumia vyema nafasi ambazo ziliachwa na mabeki wa timu pinzani waliovutika kumkaba Mayele. Kubwa zaidi alifunga bao pekee la Yanga kwa kufanya maamuzi ya haraka kugeka na mpira na kumtazama kwa haraka lango la wapinzani na kupiga shuti lililomshinda kipa Oussama Benbot wa USM Alger. USM ALGER WALIISHIKA PABAYA YANGA Muda mwingi wa kipindi cha kwanza, USM Alger walitumia mbinu ya kupiga mipira mirefu kwenda mbele jambo huku ikiwaacha yanga wamiliki zaidi mpira ingawa ilihakikisha lango lao halifikiwi kirahisi. Pengine benchi la ufundi la Yanga liliamini wapinzani wao wataendelea kucheza kwa namna hiyo kwenye kipindi cha pili lakini mambo yakwa tofauti kidogo. USM Alger walibadilika na kupiga pasi nyingi fupifupi za haraka hasa katika upande wa mpinzani wao jambo lililowaweka Yanga matatizoni mara kwa mara wakionekana kukosa mbinu mbadala ya kudhibiti mpango huo wa wapinzani wao. MWAMUZI ALIVYOTOA FUNDISHO Dakika 10 ziliongezwa na mwamuzi wa mechi hiyo, Jean Jacques-Ndala Ngambo kutoka DR Congo mara baada ya kukamilika kwa dakika 90 za mchezo ikiwa ni muda wa kufidiwa kutokana na dakika zilizopotezwa wakati wa muda wa kawaida ama kwa makusudi au kwa matukio kama kutibiwa kwa wachezaji au timu kufanya mabadiliko ya wachezaji. Ni fundisho kwa waamuzi wetu wa hapa nchini ambao wamekuwa wazito kuzifidia dakika nyingi ambazo zimekuwa zikipotea mchezoni. NABI MATUMAINI BADO YAPO. Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema kuwa bado wa namtuamini ya kupindua meza ugenini na kutwaa ubingwa wa mashindano hayo. "Ingawa ni ukweli kwamba USM alger ni timu iliyo ngumu kiulinzi, tulitengeneza nafasi nyingi. Tulikuwa na umiliki wa mpira asilimia 62 dhidi ya timu ambayo ina ukuta mgumu na wachezaji wapambanaji. Hii ndio maana nasema bado haijaisha, tuna utamaduni wa kufunmga mabao ugenini," alisema Nabi.