Twiga Stars ilikuwa ni lazima ishinde

TIMU ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars imesonga hatua inayofuata kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) mwakani zitakazofanyika Morocco baada ya kuitoa Ivory Coast kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya sare ya 2-2. Kila timu ilipata ushindi nyumbani kwake kwani baada ya Ivory Coast kushinda 2-0, juzi Tanzania ikacharuka na kushinda mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex na kulazimisha mchezo kuingia katika hatua ya kupigiana matuta. Mabao yote ya Tanzania yalifungwa kipindi cha pili na kiungo Donisia Minja katika dakika ya 49 aliyepiga mpira wa kutengwa (frii-kiki) uliozama kambani moja kwa moja huku dakika ya 51 Oppah Clement akiiongezea bao la pili. Hata hivyo, Twiga bado haijamaliza kazi kwani ili kufuzu WAFCON ni lazima iitoe Togo ambayo imetinga hatua ya pili baada ya kuing’oa Djibouti kwa jumla ya mabao 13-0, ikishinda mchezo wake wa kwanza kwa mabao 7-0 na wa marudiano juzi kwa 6-0. Mwanaspoti linakuletea mambo yaliyoifanya Stars kushinda mchezo huu BENCHI LA UFUNDI Wengi hupenda kumwita mchawi mweusi, kocha mkuu wa kikosi hicho, Bakar Shime ambaye ndiye nahodha wa kuliendesha gurudumu la soka la wanawake nchini akisaidia na Kocha wa JKT Queens, Ester Chabruma. Pengine uwepo wake katika kikosi hicho unaisadia timu hiyo kupata matokeo ambayo watu waliikatia tamaa Stars baada ya kipindi cha kwanza kuisha kwa 0-0. Uzoefu wake katika timu za taifa umeipa nguvu timu hiyo kushinda mchezo huo muhimu. UZOEFU WA WACHEZAJI Licha ya kipindi cha kwanza Tanzania kumiliki mpira kwa asilimia 53 dhidi ya 47 za Ivory Coast lakini bado iliwekwa katika wakati mgumu kutokana na wageni kupanga mashambulizi yao kwa hesabu kali. Hata hivyo, uzoefu wa wasichana hao kwenye ligi na wale wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi uliipa uhai Twiga Stars. Wachezaji kama Donisia Minja, Amina Ally ambao wako Ligi Kuu na Oppah Clement alifunga bao la pili na lile la penalti lililoivusha timu hiyo hatua inayofuata waliifanya kazi kubwa kuhakikisha ubao unasomeka vizuri. Mwingine ni kipa Naijat Abbas ambaye anakipiga kwa wanajeshi wa JKT Queens na mabingwa wa Ligi Kuu Bara (WPL) ameifanya Tanzania ibaki salama kwa kuokoa mipira mitatu ya hatari langoni kwake. Hii sio mara ya kwanza kwa Naijat kufanya hivyo kwani aliwahi kuliweka lango la JKT salama na kuokoa penalti moja kwenye fainali za CECAFA zilizofanyika Uganda ambako JKT ilishinda 5-4 na akashinda tuzo ya kipa bora. SAPOTI YA MASHABIKI Timu za taifa za wanawake zimekuwa zikifanya vizuri na hii inachagizwa na uwepo wa mchezaji wa 12 uwanjani, ambao ni mashabiki. Mashabiki wamekuwa kipaumbele kwasasa kufuatilia na kuwapa sapoti kubwa wachezaji kufanya vizuri uwanjani na hilo limeonekana juzi Azam Complex. MSIKIE SHIME Kocha mkuu wa kikosi hicho, Bakari Shime alisema mpango wake wa kipindi cha pili umeisaidia timu kushinda kwani walikuwa wametoka kwenye reli. Alisema kipindi cha kwanza timu yake ilikosa utulivu na walivyorudi kipindi cha pili aliwaambia wacheze kwa tahadhari na kupata matokeo. “Timu imekua sasa, kuitoa kwenye mashindano timu kama Ivory Coast sio rahisi kwasababu na wao walikuwa wanacheza na kutushambulia, nashukuru Mungu mpango niliowapa wachezaji wangu umeisadia timu kipindi cha pili kupata matokeo,” alisema Shime. Mfungaji wa bao la pili, Oppah Clement alisema mechi hiyo imewafunza mambo mengi kwani hawakuwahi kucheza dhidi ya wapinzani hao. “Nashukuru kwa kufunga bao na maelekezo ya kocha yametusaidia kuipa ushindi timu yetu, najua hatujamaliza ila naamini tutafuzu mwakani,” alisema Oppah ambaye kwasasa anakipiga Besiktas ya Uturuki. MECHI IJAYO Ushindi wa Twiga umeivusha kwenda raundi ya pili na sasa inatarajiwa kuvaana na Togo iliyoing’oa Djibouti kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini.