SPOTIDOKTA: Mashabiki wanakata moto uwanjani kwa sababu hizi

Mwanaspoti
Published: Jun 02, 2023 15:27:55 EAT   |  Sports

KATIKA mchezo kwanza ya fainali ya kombe la shirikisho CAF uliochezwa Jumapili jijini DSM katika dimba la Mkapa klabu ya Yanga ilipoteza mchezo huo kwa kufungwa mabao 2-1 dhidi ya US Alger ya nchini Algeria. Chakusikitisha ni pale ilipotokea tukio la mashabiki kulazimisha kuingia ndani kiasi cha kutokea vurumai iliyolazimisha polisi wakutuliza ghasia kutumia maji yenye kasi kuwatawanyisha. Katika taarifa ya baadaye iliyotolewa na wizara ya Afya kupitia waziri wa Afya Ummy Mwalimu ilieleza kuwa majeruhi 30 walipokelewa katika hospitali ya rufaa ya Temeke kupata huduma za matibabu. Bahati mbaya kati ya hao 1 alifariki ambaye alikuwa ni mwanaume mwenye takribani miaka 40. Pale zinapokutana timu katika hatua kama hii ya fainali ni kawaida kujitokeza matukio kadhaa ikiwamo tatizo la kukata moto yaani kuzimia hasa pale inapotokea huzuni kali au furaha iliyopitiliza. Mchezo huo uliobeba hisia kali kwa mashabiki wa Yanga, ilishuhudia furaha yao ya kukomboa goli ikidumu kwa dakika moja na kukutana na huzuni kali mara baada ya kufungwa goli la pili. Goli hili lilileta simanzi sana kwa mashabiki kiasi kwamba wapo baadhi walikata moto kutokana na mstuko wa kufungwa. Sababu za kukata moto Kukata moto kama ivyojulikana mtaani, kitabibu ni Syncrope au kwa Kiingereza fainting. Ni hali ya kupoteza fahamu kwa muda mfupi inayoweza kumpata mtu yoyote ikiwamo wenye afya njema. Mara nyingi sababu kuu huwa ni uchache wa hewa ya oksijeni katika ubongo. Na pia ni kawaida mara chache sababu isijulikane. Ukikata moto mwili huruhusu kufanyika kwa shughuli za ndani ya mwili huku shughuli za nje ya mwili ikiwamo kutembea, kusikia, kuongea na kuona zikisitishwa. Ni tatizo la muda endapo tu hakuna tatizo lolote la kiafya lililochangia, mwili utatua hatilafu hiyo na baadaye fahamu hurudi katika hali ya kawaida. Vilevile tatizo hili linaweza kuwa ni ishara ya uwepo wa tatizo kubwa la kiafya mwilini na ndiyo maana inashauriwa anayezimia apewe huduma ya kwanza na uangalizi kama mgonjwa wa dharura. Mliona waliokata moto walibebwa kwa machela na kwenda kupata huduma ya kwanza eneo salama. Kawaida mwili ukiwa katika hali hiyo maeneo nyeti ikiwamo ubongo na moyo ndiyo yanayopewa kipaumbele kupata damu nyingi yenye oksjeni. Mwili hubana matumizi ya damu kwa kuinyima misuli ambayo kipindi cha kuzimia huwa imetulia. Kipindi hiki mishipa ya pembezoni hujibana ili kuongeza msukumo wa damu na moyo hudunda kwa kasi ili kuhakikisha maeneo nyeti yanapata damu yenye oksijeni. Unaweza kujiuliza kwanini wasisizimie wachezaji waliopo uwanjani? lakini kumbe washabiki ndiyo huwa katika shinikizo kubwa wakifuatilia kwa umakini kila kinachoendelea wakiwa katika hisia ya hali ya juu. Kuwepo katika msongamano mkubwa katika michezo ya mashindano makubwa kama haya ambayo huwa na idadi ya watu kati ya 50,000+ ambacho ni kihatarishi cha kukata moto. Tofauti na wachezaji ambao wapo dimbani wakiwa wanapata hewa ya kutosha, mashabiki wao wamesongamana jukwaani au katika foleni ya kuingia ndani wakipokonyana hewa kidogo. Hali ya hewa ya joto na kutokwa na jasho sana kunaweza kusababisha mtu kupoteza maji mengi mwili hivyo kuweza pia kusababisha mtu kukata moto kutokana na upungufu wa maji na chumvi mwilini. Upenzi wa timu uliokithiri huchangia kupatwa na mshtuko mkali pale wanapofungwa hivyo kupata mabadiliko ya ghafla ya hisia. Hali hii kuzalisha hasira inayoambatana na kutiririshwa kwa wingi kwa homoni ya Adrenalini ambayo nayo inaweza kuchangia kukata moto. Baadhi ya watu miili yao hukosa ustahimilivu wa kukabiliana na hali ngumu ya uchache wa hewa hivyo kukata moto kirahisi Maelfu ya Mashabiki hupokonyana hewa kidogo na huku miili yao huwa katika shinikizo kubwa kutokana na hali ya hewa ya mvua, makelele na hisia kali za ushabiki huweza kuchangia kuzimia. Kutumia muda mwingi kusafiri na foleni barabarani mpaka kufika viwanjani, mihangaiko ya kuweza kuingia ndani ni mambo yanayouchosha mwili hivyo hatarini kuzimia huwa ni kubwa. Ikumbukwe wapo mashabiki wamesafiri kutoka sehemu mbalimbali ikiwamo toka mikoani kama vile Mwanza, Mbeya kigoma, Lindi na Mtwara. Dalili za kukata moto ni hizi Dalili zinaweza zisiwe za moja kwa moja kwani inawezekana mtu aliyekata moto akakumbuka tu kuona giza au kizunguzungu na kisha asikumbuke kitu. Pia mtu anawezakata moto na akakumbuka kila kitu ikiwamo dalili zilizompata mpaka alipoanguka na kugonga chini. Wengi wanaozimia wanakumbuka tu dalili ya kuona mawimbi mawimbi au giza giza na kizunguzungu hatimaye kuishiwa nguvu na kukata moto. Mara nyingi dalili za jumla ni pamoja kuishiwa nguvu, kupumua kwa shida, kuona nyota na giza, kizunguzungu, mapigo ya moyo ya kasi, kuchanganyikiwa au kuweweseka, Vile vile kuhisi miguu kukosa nguvu na kuwa mizito, joto kupanda au kutokwa jasho, kupata kichefuchefu au kutapika na kupiga miayo mingi. Walio katika hatari ni pamoja na wenye magonjwa ya moyo, ubongo, upungufu wa damu, lishe duni, shinikizo la damu la kushuka, magonjwa mfumo wa hewa, upungufu wa maji, msongo wa mawazo na wasiofanya mazoezi. Huduma ya kwanza iko hivi Kwanza kumtoa katika eneo hatarishi na kumweka eneo salama lililo na hewa ya kutosha, fungua au legeza nguo zote alizovaa. Kama huna ujuzi toa mwito haraka kwa watoa huduma ya kwanza wafike kutoa msaada huku Hakikisha njia ya hewa haina mikwamo , msaidie upumuaji kwa kumpepea au kumweka katika eneo lenye hewa. Mgonjwa hulazwa katika mtindo wa kunyanyuliwa kidogo eneo la miguu kuwa juu kuliko kiwiliwili ili damu nyingi ifike katika ubongo kirahisi. Akipata nafuu huwekwa katika ulalo mzuri unaosaidia mwili kupata nafuu haraka. Ili kukabiliana na tatizo la kukata moto katika viwanja vya michezo inashauriwa kudhibiti msongamano, viwanja viwe katika maeneo ya wazi yenye hewa ya kutosha na kujidhibiti hisia kali za ushabiki. Vile vile kunywa maji mengi na mlo kabla ya kwenda katika mechi kama ya jumapili na vizuri kuongeza watoa huduma ya kwanza viwanjani na kutoa elimu ya huduma ya kwanza kwa jamii. Chukua hii Faida ya kukata moto ni mwili kusahihisha dosari iliyojitokeza kwani kipindi hiki mwili hulipa deni la upungufu wa hewa ya oksijeni kwa kuruhusu damu kwenda maeneo nyeti zaidi ili kulinda uhai. Hasara yake ni pamoja na majeraha ya kichwa, kuchubuka na kujeruhi tishu laini. Kifo huweza kutokea kama mwili utashindwa kurekebisha dosari iliyojitokeza na pia kama oksijeni ni chache sana na ubongo ukaendelea kukosa oksijeni muda mrefu.