Sixstus Sabilo, apewe maua yake

Mwanaspoti
Published: Jun 02, 2023 15:25:01 EAT   |  Sports

EBWANA Eeh! Huko mtaani nguvu kubwa imekuwa kuzizungumzia klabu za kariakoo , Simba na Yanga sambamba na wachezaji wake, ni jambo zuri lakini kwa namna flani ni kama wanaofanya vizuri nje ya timu hizo wamesahaulika. Naam. Kila kina sasa ukipita utasikia stori za Yanga na Simba, utasikia majina ya kina Fiston Mayele, Stephane Aziz Ki, Clatous Chama na Jean Baleke, ni mara chache sana utawasikia Jumanne Elfadhili au Collins Opare. Achana na hayo, ni kawaida yetu wabongo. Pale Mbeya City kuna mshambuliaji mmoja anaitwa Sixtus Sabilo, jamaa ni mzaliwa wa kijiji cha Kasahunga, Bunda, mkoani Mara. Ni moja ya wachezaji walio kwenye viwango bora zaidi msimu huu katika Ligi Kuu licha ya kwamba timu yake ya Mbeya City inapumulia mashine ikihaha kushuka daraja ikiwa imebakiza mechi mbili dhidi ya Yanga na KMC. ANGA ZA SAIDO, MAYEL Licha ya kuwa yupo timu unayoshika nafasi ya 12, kwenye msimano na alama 30 baada ya michezo 28, lakini amekaa meza moja na Mayele wa Yanga mwenye ubingwa wa ligi msimu huu na Saidi Ntibanzokiza ‘Saido’ na Chama wa Simba iliyopo nafasi ya pili kwenye msimamo. Ndio. Sabilo ni miongoni mwa wachezaji wanne waliohusika kwenye mabao mengi katika Ligi Kuu msimu huu. Kinara wa orodha hiyo ni Saido, aliyehusika katika mabao 22, akiwa amefunga 10, na kutoa pasi za mwisho ‘Asisti’ 12, akifuatiwa na Mayele aliyehusika katika mabao 19, akifunga 16 na kuasisti mara tatu, kisha Chama alihusika kwenye mabao 18 akifunga manne na kuasisiti mara nne na baada ya hao ni Sabilo aluyehusika kwenye mabao 16 akifunga tisa na kuasisti mara saba. Ukiachana na kuwa kwenye anga za mastaa hao, pia sabilo ni mchezaji pekee mzawa wa Tanzania aliingia kwenye tano bora ya mastaa waliohusika kwenye mabao mengi akishika nafasi ya nne nyuma ya Saido, Mayele na Chama huku nafasi ya tano akiwepo Moses Phiri wa Simba aliyehusika kwenye mabao 13 akifunga 10 na kuasisti tatu. KAMA HAAMUONI HIVI Licha ya kuwa na kiwango bora na namba zinazombeba Sabilo, lakini ni kama wadau wa soka nchini wamemfumbia macho na kumnyima kile anachostahili katika msimu huu. Pamoja na moto wote aliouwasha msimu huu, Sabilo alichokiambulia hadi sasa ni tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Oktoba mwaka jana pekee, mwezi ambao alitia asisti mbili na kufunga mabao matatu. Hakuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’ kilichotangazwa mwezi Machi mwaka huu chini ya kocha Adel Amrouche kilichocheza mechi mbili za kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (AFCON 2023), dhidi ya Uganda licha ya kuwa alistahili kuliko baadhi ya wachezaji walioitwa. Haikuishia hapo, Sabilo hakutajwa tena katika orodha ya wachezaji wanaowania tuzo za msimu huu, sio katika kipengele cha mchezaji bora, wala kiungo bora alikotajwa. Kiufupi anetoka kapa. ALIKOTOKA Kama ulikuwa haujui, Sabilo aliwahi kuwa mvuvi katika Ziwa Victoria lakini pia aliwahi kuwa mpiga debe pale kwenye stendi ya Bunda Mjini katika nyakati tofauti huku akiendelea mdogo mdogo kuifukuzia ndoto yake ya kuwa mwanasoka. Jamaa amecheza sana Ndondo za Kanda ya ziwa kabla ya Stand United kumuona, kupitia kwa nahodha wa timu hiyo kwa wakati ule mwaka 2016, Jacob Masawe aliyemuomba akafanye majaribio na kufuzu kisha safari yake ikaanzia hapo. Masawe huyu ni yule kiungo wa sasa wa Namungo na misimu miwili nyuma alikua Gwambina FC. Msimu wa 2016/2017, Sabilo alicheza Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza akiwa ndani ya Stand United ‘Chama la Wana’ alipodumu kwa muda wa miaka miwili na nusu kisha kujiunga na KMC mwaka 2018 katika dirisha dogo la msimu huo. Hata hivyo hakuwa na wakati mzuri ndani ya kikosi cha KMC, kwani alicheza kwa miezi sita tu kabla ya kutolewa kwa mkopo kwenda Polisi Tanzania alikokiwasha na baada ya msimu kumakizika akapewa mkataba wa kuendelea kusalia kwa wafunga buti hao. Baada ya hapo alijiunga na Namungo, kisha Mbeya City anapocheza hadi sasa ikiwa ni timu ya Ligi Kuu aliyoifungia mabao mengi zaidi kwenye maisha yake ya soka hadi sasa. ANAITAKA TIMU YA TAIFA Pamoja na ndoto nyingine alizonazo Sabilo ukizingatia kwa sasa ni kipindi cha vuguvugu la usajili lakini Sabilo ameliambia Mwanaspoti ndoto yake kubwa kwa sasa ni kuitumikia timu ya taifa. “Natamani kuichezea timu ya taifa, ni ndoto yangu tangu zamani na sasa nasikilizia kama ikitimia nitafurahi na kuhakikisha nafanya vizuri zaidi,” alisema Sabilo anayehusishwa kuhitajika na klabu za Azam, Singida Big Stars na Geita Gold.