Simba yafuata beki Muivory Coast

Mwanaspoti
Published: Jun 01, 2023 08:28:30 EAT   |  Sports

SIMBA imeamua kuboresha kila idara kwenye kikosi chake, achana na winga Kramo Aubin inayoweza kumalizana naye muda wowote, sasa imetua kwa beki wa kati Coulibaly Wanlo raia wa Ivory Coast kutoka ASEC Mimoses. Taarifa zilizoandikwa juzi Jumatatu na Mwanaspoti, zilieleza jinsi Simba ilipofikia mazungumzo na winga Aubin, lakini baada ya kuona kuna beki mahiri, ikaamua kupiga ndege wawili kwa jiwe moja kwa kuanza kufanya naye mazungumzo. Chanzo cha taarifa hizo kinasema: "Lengo lilikuwa ni winga, lakini mtathimini wetu wa viwango akashauri beki huyo anaweza akatufaa, tukaona tuna nafasi ya kufanya naye mazungumzo ambayo yameanza ili kujua mkataba upoje. "Kuna ulazima wa kusajili beki wa kati kwani ni eneo linalohitaji marekebisho tangu awali, hivyo dili hili likikamilika tutakuwa tumeua ndege wawili kwa jiwe moja." Nje na hao wachezaji aliowataja wapo wengine ambao Mwanaspoti linawafuatilia kwa ukaribu ambao Simba wanawahitaji kwenye kikosi chao, akiwemo kipa na mwanzo alihusishwa wa Coastal Unon, Justin Ndikumana, washambuliaji wawili na winga. "Kwenye winga anahitajika mgeni na mzawa bado tunalifanyia kazi kuona nani anaweza akaja akaongeza nguvu kwenye kikosi, hatutaki ili mradi wachezaji tu, bali wenye uwezo wa kuifanya thamani ya Simba kuendelea kuwa juu," alisema. Akizungumza kuhusu usajili wa msimu huu, Mkuu wa Kitengo cha Habari Simba, Ahmed Ally alisema timu hiyo imejipanga vizuri sana kuboresha sehemu ambazo kocha wao anataka na wale watakaosajiliwa ni wale walioshiriki Ligi ya Mabingwa msimu huu au Shirikisho Afrika. "Tumejipanga vizuri na hadi sasa tumeshafahamu nani anasajiliwa kwa ajili ya msimu ujao, wachezaji wanaoingia ni moto haswa, ni wale ambao walikuwa kwenye Ligi ya Mabingwa msimu huu na Kombe la Shirikisho," alisema Ahmed. Kauli hiyo inakubaliana na data ambazo Mwanaspoti inazo, kwani Asec msimu huu ilishiriki Kombe la Shirikisho na kutolewa nusu fainali na USM Algier.