Robertinho aiwekea mikakati robo fainali CAF, Yanga

Mwanaspoti
Published: Mar 23, 2023 12:00:14 EAT   |  Sports

SIMBA inarudi kazini leo baada ya mapumziko ya siku tatu wakitoka kufanya mauaji makubwa katika mchezo wao wa Kimataifa dhidi ya Horoya wakishinda kwa mabao 7-0 lakini kocha wao akatuma salamu wanaoubeza mziki wao. Kocha Robert Oliveira ‘Robertinho’ amezungumza na Mwanaspoti na kueleza sababu za wao kujitabiria makubwa na wanarudi kuanza maandalizi kujipanga na mechi zao zijazo za Kimataifa. Kocha huyo raia wa Brazil alisema Simba kushinda kwao mabao 7-0 sio kitu cha kubahatisha; “Nina furaha ya aina mbili, kwanza wachezaji wangu wamebadilika na kuelewa kucheza kulingana na falsafa yangu tunavyocheza sasa ndivyo Simba ninayoitaka icheze, pia hakuna ambaye hataogopa kukutana na Simba ikiwa nyumbani tukiwa na mashabiki wetu bora kabisa. “Hizi mechi za hatua ya robo tutabadilika kidogo, unajua kama tutaanzia nyumbani kisha kwenda ugenini basi tunatakiwa kumaliza kazi hapa halafu utajua ucheze vipi kule ugenini, kwa hiyo kifupi tutakuja na sapraizi nyingine.” “Nilisema awali Simba haina sababu ya kuhofia mpinzani yoyote, mimi ni kocha ambaye napenda presha ya mechi kubwa kama hizi ije tu. Hatukushinda dhidi ya Horoya kwa kubahatisha tulikaa na kuwasoma wapinzani wetu na kuwabadilishia mbinu zetu tofauti na tulivyocheza kwao,” alisema Robertinho ambaye ni Kocha wa zamani wa Vipers ya Uganda. “Hata hizo mechi zinazokuja Simba itakuja na mkakati sahihi kulingana na timu tutakayopangiwa lakini kwa sasa tutawaangalia kwanza Raja ambao tunakwenda kukutana nao kumalizia mechi za makundi.” MKAKATI WA YANGA Robertinho ambaye ni winga wa zamani wa Brazil alisema Simba yake haitajikita kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa pekee, itaendelea kuwafukuza Yanga wanaongoza ligi kuhakikisha wanaitia presha kuweka uwezekano wa kupunguza tofauti ya pointi. “Hatuwezi kuangalia mashindano ya CAF pekee, tunarudi uwanjani, hizi mechi za ndani zina maana yake, kwanza tunatakiwa kuendelea kuwawekea presha wanaongoza ligi (Yanga) kuangalia kama watafanya makosa, hili ni kubwa sana, pia kuna mechi za Kombe la FA,” aliongeza kocha huyo ambaye hushangilia na mashabiki kila Simba inaposhinda.