Rais RT ang'aka, mikoa iliyojitoa riadha Taifa kuchukuliwa hatua

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Silas Isangi amesema, mikoa iliyojitoa kushiriki mashindano ya taifa mwaka huu itachukuliwa hatua. Akionyesha kuchukizwa na mshindi wa pili wa mashindano yaliyopita, mkoa wa Arusha kujitoa kushiriki, amesema wachezaji hawajatendewa haki. "Kama leo ingekuwa ni uchaguzi mkuu au mkutano mkuu, viongozi hao wa mikoa wangekuwa hapa, lakini kwenye mashindano ya taifa hawajaleta timu, ili tutalishughulikia," alisema Isangi akitoa maelekezo kwa makamu wake, William Kalaghe katika kushughulikia hilo. Akizungumza kwenye ufunguzi wa mashindano ya msimu huu leo katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, amesema, "Wachezaji hawajatendewa haki, nawapongeza viongozi walioleta wachezaji, wenyeviti wa mikoa waliomba nafasi kuwatumikia watu, kama kiongozi huleti watu kwenye mashindano wewe nawe hutufai. "Mbio sasa ni pesa, mchezaji unapofanya vizuri unajitengeneza rekodi, unanufaika na kuiletea nchi yako sifa, mnapaswa kufuata nyayo za kina Bayi (Filbert bingwa wa zamani wa dunia wa mita 1500," bosi huyo wa RT amewambia wachezaji walioshiriki. Mgeni Rasmi, Charles Maguzu ofisa kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) aliyemwakilisha katibu mkuu, Neema Msitha, pamoja na mambo mengine, aliwataka wachezaji kuyatumia mashindano ya taifa kuimarisha muda wao kwa ajili ya mashindano ya kimataifa. Katika mashindano hayo, Kusini Unguja ilitwaa medali zote sita kwenye fainali ya kurusha tufe ikiongozwa Samil M Sururu aliyerusha umbali wa mita 12 na sentimita 89 na Naifat A Hassan aliyerusha mita 9:90 na kutwaa medali za dhahabu kwa wanawake na wanaume. Medali ya fedha ilichukuliwa Mohamed I Mtwana aliyerusha mita 11:98 na Hafidh A Hamadi akihitimisha tatu bora akirusha umbali wa mita11:51. Fatma Hussein aliyerusha mita 9:19 alimaliza wa pili kwa wanawake na Shadya Ame aliyerusha mita 9:02 akihitimisha tatu bora. Nyota wa Dar es Salaam, Emmanuel Josephat ameshinda medali ya dhahabu kwenye mita 10,000. Nyota huyo ambaye hiyo ni mara yake ya kwanza kushiriki mashindano hayo alisema mazoezi ndiyo yamembeba, akibainisha kwamba wapinzani aliowazunguka hawakuwa na uvumilivu wa miguu. "Tulipoanza mbio niliachwa kama mita 70 na aliyetangulia ambaye baadae nilimzunguka, sikutaka kushindana naye sababu mizinguko ilikuwa bado, tulipofika mzunguko wa saba, nilibadilika na kuongeza kasi hadi kuwa bingwa," alisema nyota huyo wa Dar es Salaam, aliyetumia dakika 31:31:56. Patrick Rwechugula wa Kilimanjaro aliyetumia 32:01: 45 alikuwa wa pili na Jackson Mganga wa Dar es Salaam aliyetumia dakika 33:17:84 alihitimisha tatu bora. Kwenye mita1500, Steward Mbaya aliyekimbia kwa dakika 3:59:98 alitwaa ubingwa na Damian Christian aliyekimbia jwa dakika 4:00:99 alimaliza wa pili, wote kutoka Mbeya wakati Fidelis Mwakalamba wa Mbeya aliyekimbia kwa dakika 04:20:03 akihitimisha tatu bora. Kwa wanawake, Salma Charles wa Singida (dakika 4:53:61), Salome Masele wa Shinyanga (5:09:75) na Jesca Raphael wa Tabora (5:19:36) walikamata nafasi ya kwanza hadi ya tatu. Mashindano hayo yatafungwa kesho kwa fainali za relay ya mita 400, kurusha mkuki na kisahani, mita 200, 400, 5,000 na 800 na triple jump kwa wanaume na wanawake na mita 10,000