Nyota Ihefu wazuiwa kikosini

IHEFU wajanja sana asikwambie mtu, kwani imesikiliza kwa umakini baadhi ya timu ligi kuu zinazowinda mastaa wake na kushtuka mapema kuwakumbatia ili kuendelea kubaki kikosini msimu ujao. Timu hiyo ambayo imekuwa na soka safi na la ushindani kwenye ligi, wapo mastaa ambao wameonekana kuwatoa umate baadhi ya timu kutaka saini zao. Hadi sasa wachezaji watano kuwindwa na baadhi ya timu ikiwa ni Yahya Mbegu na Nicolas Wadada (Singida Big Stars) Raphael Daud ‘Loth’ (Geita Gold) na Andrew Simchimba na Mwaita Gereza Kagera Sugar. Meneja wa timu hiyo, Lulanga Mapunda alisema taarifa hizo wanazisikia lakini benchi la ufundi halijalala kihivyo isipkuwa wanaendelea kupambana kuhakikisha hawaachi mtu. Alisema wanajitahidi kuwashawishi mastaa wao walioonesha kingo kubaki kikosini msimu ujao lakini kuwasilisha mapendekezo kwa uongozi ili kuwaongezea mikataba kwa wanaomaliza. “Sisi tunapambana vijana wetu kubaki nao msimu ujao, tunaamini tutafanikiwa kwa sababu tunaishi nao vizuri kimsingi ni kuongea na uongozi kuhakikisha haondoki mtu, mengine ni mazungumzo tu,” alisema Mapunda. Hata hivyo meneja huyo aliongeza kuwa baada ya mapumziko mafupi, tayari timu imerejea mazoezini kuendelea na maandalizi ya mechi mbili zilizobaki kuhakikisha wanashinda. “Tulitoa mapumziko ya siku tatu na tayari tumenza tangu Ijumaa kwa ajili ya kumalizia mechi mbili zilizobaki, tunahitaji ushindi ili kuhitimisha ligi kwa heshima,” alisema meneja huyo.