"Nyerere Cup" Mashindano ya wavu Kuanza Oktoba 10, timu 11 zathibitisha kushiriki.

MICHUANO ya Nyerere Cup kwa mchezo wa mpira wa wavu inatarajiwa kuanza oktoba 10 hadi 14 mwaka huu katika Uwanja wa Hindumandal, Mkoani Kilimanjaro ambapo timu 11 za mataifa mbalimbali zimethibitisha kushiriki. Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu mkuu wa Chama cha mchezo wa Wavu Tanzania (TAVA), Laurence Safari amesema kwa kawaida mashindano hayo hufanyika kila mwaka na huandaliwa na chama hicho kumuenzi aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Julius Nyerere. "Rais Nyerere enzi za uhai wake amefanya mambo mengi makubwa hapa nchini,alikuwa mpenzi mkubwa wa michezo,hivyo TAVA kwa kutambua na kuthamini mchango wa kiongozi huyo, huendesha mashindano haya ya mpira wa wavu yenye nia ya kumuenzi" Alisema Safari. Wakati huohuo Katibu wa kamati ya mashindano ya mchezo huo, Riziki Godwin amesema Septemba 30 mwaka huu utakuwa mwisho wa klabu kuthibitisha ushiriki wao ambapo wenyeji Tanzania itawakilishwa na klabu 13 za wanawake na wanaume ambapo vilevile wanatarajia kupata idadi kubwa zaidi ya Klabu kutoka kanda tano barani Africa. Riziki amezitaja Klabu zilizothibitisha kushiriki michuano hiyo kuwa ni DCI, GSU, Kenya Forest, Nairobi Water Services, KCB, Airport Police, Pipeline, USIU zote kutoka Kenya, APR (Rwanda) na Rukinzo (Burundi) huku Klabu kutoka mataifa ya Misri, Uganda, Somalia, Djibouti,Sudan zikisubiliwa kuthibitisha ushiriki wao. Kwa upande wake Katibu wa mchezo huo Mkoani kilimanjaro, Renovatus Sixmund amesema Licha ya kwamba mashindano hayo yatafanyika lakini bado wanauhitaji mkubwa wa wadhamini hivyo wanahitaji kuungwa mkono kwa atakayeguswa kuwasapoti huku akiwaalika mashabiki na wapenzi wa mchezo huo kuja kwa wingi kushuhudia burudani hiyo itakayofanyika kiwanja cha Hindumandal kilichopo katikati ya mji wa Moshi.